Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Esther Lukago Midimu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia. Kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanazozifanya. Kwa namna ya pekee nampongeza Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anazozifanya. Kwa muda mfupi amefanya kazi na zimeonekana, Mwenyezi Mungu ambariki sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kutekeleza ahadi ya kuleta maji kutoka Ziwa Victoria mpaka Mkoa wa Simiyu na Wilaya zake tano za Busega, Bariadi, Itilima, Maswa na Meatu, na hela tayari zimeshakuja, wananchi wana imani na Rais wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali yangu sikivu maji yakifika Mkoa wa Simiyu iweze kusambazwa kwenye shule za msingi na sekondari pamoja na vituo vya afya na zahanati. Nasema hivyo kwa sababu wanafunzi wanahangaika sana, muda mwingi wanachota maji usiku, asubuhi wakienda darasani wanashindwa kusoma wanasinzia tu, ni bora Serikali itoe kipaumbele katika mashule yetu yapate maji ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Mkoa wa Simiyu ni wachapakazi wazuri na ni wakulima wazuri, nina imani maji yakifika watalima kilimo cha umwagiliaji, njaa itakuwa ni ndoto katika Mkoa wa Simiyu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali yangu kwa ajili ya kutuletea shilingi bilioni 1.6 kwa ajili ya ukarabati wa mabwawa Wilaya ya Itilima na mabwawa yale ni Mwamapalala, Nobora, Sunzula, Sawida, Chinamiri na Lugulu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali yangu sikivu sasa iweze kusambaza maji kwenye kata ili kutimiza azma ya Mheshimiwa Rais ya kumtua mwanamke ndoo kichwani. Iweze kusambaza kwenye kata zifuatazo, kata za Nkuyu, Migato, Mwaswale, Mwamtani, Nkoma, Kindilo na Sawida. Maeneo haya niliyoyataja wanawake wanahangaika sana, muda mwingi wanaupoteza kutafuta maji kuliko kufanya kazi za maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ukizingatia wanaochota maji ni wanawake si wanaume. Mwanamke anachota maji usiku, saa zingine anakutwa na matatizo huko njiani. Naiomba Serikali iweze kuzingatia hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.