Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. LUCY F. OWENYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kupata nafasi ya kuchangia. Maji ni uhai, wanadamu, wanyama, mazao kila kitu kinahitaji maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wengi tumekuwa tukilalamikia upatikanaji wa maji katika Jiji letu la Dar es Salaam, tukumbuke Jiji hili ndilo kioo cha nchi yetu, lakini tatizo la maji ni kubwa. Hata baadhi ya maji yanapopatikana siyo salama na safi. Baadhi ya maji yanayotoka yamechanganyika na kinyesi sababu ya miundombinu mibovu na mingine imechakaa, pamoja na Serikali kujitahidi kubadilisha baadhi ya mabomba. Je, ni lini Dar es Salaam watapata maji safi na salama kwa ajili ya kunywa? Tumeshuhudia kipindipindu na magonjwa mengine ya kuhara hayaishi Dar es Salaam sababu inachangiwa zaidi kutokuwa na maji salama na safi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu maji taka, bado mfumo wa maji taka ni tatizo Dar es Salaam hata hapa Dodoma. Kipindi cha mvua tumeshudia ndiyo wakati mashimo ya maji taka yanafurika na kusababisha kwanza mji mzima kunuka, kusababisha kulipuka magonjwa na kadhalika. Je, Serikali ina mpango gani wa kupanua mifumo ya maji taka sababu iliyopo ilikuwa inahudumia watu wachache, kwa sasa Jiji limeongezeka watu wengi zaidi ya milioni nne lakini mfumo ni ule tangu enzi za ukoloni
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Wilaya ya Moshi; pamoja na Wilaya hii kuwepo chini ya Mlima Kilimanjaro lakini bado wananchi wanaotoka kata za Mbokomu, Old Moshi, Kiboriloni, bado kuna tatizo kubwa la upatikanaji wa maji. Mradi wa maji vijijini ulikuwepo lakini maji yake yalitoka na siyo zaidi ya miezi sita. Wanaoteseka ni watoto wa shule badala ya kusoma, wanatumiwa na walimu kwenda kuteka maji na akina mama wanatembea mbali wanabeba maji vichwani, hii ni kurudisha maendeleo nyuma. Je, mpango wa kuleta maji ya uhakika vijijini utakamilika lini badala ya haya maji ya kisiasa?
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu umwagiliaji mpaka sasa wakulima wetu wengi walikuwa wanategemea mvua na hawa wapo zaidi ya asilimia 80. Bado Wizara haijatoa elimu ya kutosha jinsi ya kuvuna maji ya mvua kwa kujenga mabwawa, kujenga mifereji ya kudumu ili waweze kupata maji kwa ajili ya kilimo. Serikali ituletee mikakati na mipango ya kuwawezesha wakulima ili waondokane na kilimo cha kutegemea mvua na kilimo hiki ni cha msimu lini waanze kilimo cha umwagiliaji ambacho kitakuwepo misimu yote? Bila hivyo viwanda tunavyotangaza vya usindikaji vitafanya kazi gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Halmashauri ya Moshi Mabogini, Wajapani walianzisha kilimo cha umwagiliaji, kilimo cha mpunga walijenga mpaka miundombinu ya maji na kilimo kule kiliendelea vizuri sana, lakini tangu Wajapani waondoke kilimo kile ni kama kimekufa. Wizara imeshachunguza ni kwa nini maji yale yamepungua?
Mheshimiwa Naibu Spika, uhifadhi wa mazingira na vyanzo vya maji; miaka ya 1960 na 1970 wananchi walielewa maana ya utunzaji wa vyanzo vya maji. Mfano, Mkoani Kilimanjaro zao la kahawa lilishamiri sana kwa kutegemea umwagiliaji na kutumia mifereji ya asili. Walipanda miti na walivitunza vyanzo vya maji, lakini kwa wakati huu vyanzo vingi vimekauka. Miti inakatwa ovyo, wananchi wanalima pembeni mwa mito na Serikali inaona makosa yote haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni wakati muafaka sasa kwa Serikali kurudisha wanafunzi kuwa na vitalu vya miti. Viongozi wa vijiji wahakikishe miti inapandwa na hawalimi kando kando ya mito na kusimamia kwa nguvu zote vyanzo vya maji vifufuliwe.