Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Kamisheni ya Pamoja ya Bonde la Mto Songwe kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Malawi pamoja na Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Amani na Usalama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Hon. Richard Phillip Mbogo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Kamisheni ya Pamoja ya Bonde la Mto Songwe kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Malawi pamoja na Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Amani na Usalama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa hii nafasi. Kwanza nitoe tu hoja kwamba Wabunge na Bunge zima tuunge mkono hizi hoja mbili ambazo zimewasilishwa ya kuhusu Bonde na hili la Amani na Usalama.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na hili Azimio la Bonde la Songwe, napendekeza kwamba kwa ujumla wetu tuangalie umuhimu wa haya mabonde. Sehemu kubwa, watu bado hawajatambua kwamba umuhimu wa bonde uko kwa kiasi gani katika nchi, tunaangalia kuyalinda mabonde kwa kwanza kuangalia vyanzo vyetu vya haya mabonde ne mito yote. Tumekuwa na sehemeu kubwa sna ya uharibifu wa mazingira ambapo imepelekea mtu wa chini hafaidiki tofauti na mtu wa juu, kwa lugha nyepesi ya kigeni wanaita upstream na downstream users. Sasa kwa kuweka huu mkataba kati ya nchi mbili tunaona kwamba kutakuwa na usawa katika utumiaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala zima la Bonde hili pia linakwenda kutujengea ushirikiano mzuri kati ya nchi hizi mbili, kati ya Malawi na Tanzania, kwa hapo nyuma kuna maneno yalishapita ya mtaani ambayo yalikuwa siyo mazuri lakini tunatumaini sasa kwa Mkataba huu ambao umesainiwa na matumizi haya ya bonde na faida zake zote ambazo zimeelezwa na Waziri mwenye dhamana, tunatumaini kwamba tutafaidika kweli.

Mheshimiwa Naibu Spika, faida ya kwanza ambayo nimeiona kwanza ni ushirikiano ambapo tutakuwa kwa pamoja na ukiangalia katika mipaka yetu watu wanafanana tamaduni na lugha, kwa hiyo ushirikiano utaendelea kuimarika.

Lingine ambalo naona litakuwepo ni suala zima la kiusalama. Nchi mbili mnapokuwa mmeshirikiana katika shughuli za kiuchumi kama hili ambalo tumesaini maana yake tutakuwa na uelewa wa pamoja, tutakuwa na usalama kati ya nchi na nchi, kwa hiyo, tunapongeza sana Serikali kwa kufanya hii jitihada.

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ambacho ningesema ni kwamba tuhusishe pia Wizara yenye dhamana upande wa Mazingira, iendelee kupitia Sheria zake za Mazingira kuendelea kulinda vyanzo vyote ambavyo vinakwenda kwenye hili bonde, tumeona kwamba nchi sasa hivi imezungukwa sana na shughuli za kiuchumi ambazo hazizingatii sana Sheria ya Mazingira, ile mita 60 kutoka kwenye kingo za mito, mita 500 kutoka kwenye vyanzo vya maji na Serikali imekuwa inahimiza sana. Kwa hiyo, naomba sana Wizara inayohusika na mazingira waendelee kulinda haya mabonde yote katika nchi yetu ili vizazi na vizazi ambavyo vinafuatia viweze kufaidika.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hii nita-comment kidogo kwenye Commission, tuombe Wizara inayohusika iangalie Commission ambayo imeundwa, waangalie matatizo ambayo yamewahikutokea, kwa mfano TAZARA ambapo kwenye upande wa reli kati ya Tanzania na Zambia, waangalie changamoto zilizopo upande wa TAZARA na upande wa huku sasa hii Commission ambayo imeundwa zisiweze kujirudia na utendaji wake uwe wenye tija na ufanisi. Kwa hiyo, tunaomba sana na hata staffing yenyewe izingatie kama mkataba vile ulivyo na namna bora ambayo wataona ni ya kuboresha na itapendeza zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeelezwa faida nyingi na mimi napendezwa sana kuona kwamba litajengwa bwawa na tutaweza ku-control mafuriko ambayo huwa yanatokea na tutaweza kupata umeme, shughuli za kiuchumi zitaweza kufanyika. Naunga mkono na naomba Wabunge wote tuunge mkono Azimio hili ambalo ni muhimu sana kwa mustakabali wa maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuzungumzia Azimio hili la bonde la Mto Songwe, naomba nigusie pia na kuhusiana na kuridhia Itifaki, Amani na Usalama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kiujumla Tanzania ni nchi ambayo ilijengwa kwa misingi mizuri na hasa Rais wetu wa kwanza, Hayati Julius Kambarage Nyerere alitengeneza amani kubwa sana katika nchi yetu ya Tanzania na vitu vingi aliweza kuviondoa. Kwa mfano; aliondoa utawala wa Kichifu ikapelekea nchi inakuwa inatawalika vizuri, ukabila vyote hivyo vimekuwa vimesaidia sana Tanzania tumekuwa na amani.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nchi yetu Tanzania ilipokea sana Wakimbizi kutoka nchi za jirani ambazo ni Congo, Burundi, Rwanda yote yalitokea kwa sababu wenzetu hawakuwa na amani. Sasa kwa misingi ya maazimio haya ambayo yanaletwa na tayari tuko kwenye Umoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki maana yake tutajikita kwenye haya maazimio ambayo yatakuwa yamesainiwa kwa ajili ya amani na usalama.

Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu wanapokuwa hawana amani matatizo yale yanaleta migogoro katika nchi yetu ikiwa ni pamoja na kuja kwa wakimbizi, imetokea matukio wamekamatwa na silaha katika Kambi za Wakimbizi na wengine matukio ya kiujambazi, sasa kwa minajili hiyo kwa kulinda amani itatusaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo mengi ya nchi za jirani kuna Tume zimewahi kuundwa, kuna mojawapo Rais Mstaafu Benjamin Mkapa amekuwa Mwenyekiti, Hayati Nelson Mandela amewahi kuwa Mwenyekiti, marehemu Hayati Mwalimu Nyerere amewahi kuwa Mwenyekiti katika kusuluhisha nchi za jirani kwa kutokuwa na amani. Nchi nyingi duniani zinasumbuliwa na masuala ya ugaidi, kwa hiyo tunavyokuwa na umoja kama Jumuiya ya Afrika Mashariki, tutaweka msimamo wa kulinda amani na wananchi wake wote watakuwa kwenye hali ya utulivu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja zote hizi mbili na nawashawishi Wabunge wote tuziunge mkono. Ahsante sana.