Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Halima James Mdee

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Awali ya yote nitumie nafasi hii kumpongeza Waziri na timu yake kwa kazi nzuri ambayo amefanya Jimboni kwangu, anajua mimi siyo mtu wa kusifia sifia lakini pale ambapo mtu anakuwa anaonesha kitu cha maana lazima tumpe credit zake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyozungumza eneo la Chasimba ambalo lilizungumzwa sana Bunge hili, sasa hivi wananchi wameshapimiwa, Wataalam wa Wizara walikaa pale siku 30 wameweka kambi, hawakulipwa posho, walikuwa wanapika kama vile wako shuleni. Kwa hiyo kwa kweli nashukuru sana na wananchi wa Chasimba, Mtaa wa Basihaya wana-appreciate kazi nzuri mliyoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na sifa hizo ambazo nimezitoa Jimbo la Kawe bado lina changamoto nyingi sana, kuna migogoro ya ardhi mingi bado na Mheshimiwa Waziri nimpongeze kwa sababu hotuba yake ime-reflect maoni ya Waziri Kivuli wa miaka mitano iliyopita. Naona anachokifanya hapa ndicho kile ambacho tulikuwa tunamshauri afanye na ndiyo maana anapewa credit kwa sababu alijua kwamba Tanzania inajengwa na watu wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa namwomba katika muktadha huo huo wa kuchukua mawazo yetu kwenye masuala ya kuchukulia hatua watu ambao wanamiliki maeneo makubwa ya ardhi na hawayaendelezi asiwe na double standard. Kama kuna kada wa CCM haendelezi achukue, kama kuna kada wa CUF haendelezi achukue, kama kuna kada wa CHADEMA haendelezi achukue. Asipofanya hivyo na sisi tutakuja hapa tutamsulubu kwa ubaguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi yalizungumzwa masuala ya migogoro ya wakulima na wafugaji, tunategemea Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha hapa, atatueleza kwa sababu Wizara yake ndiyo Mama, hizi Wizara nyingine zinamtegemea yeye katika kuonesha mwelekeo. Kwa hiyo, tunatarajia majibu yake yeye yatatoa mwelekeo wa Taifa kwa kushirikiana na Wizara zingine, ili tujue tunaendaje kutatua migogoro hii kwa kuhakikisha tunaweka ama tunapanga matumizi bora ya ardhi. Kwa hiyo, nategemea atakuja na hayo majibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanja 20,000 ama mradi wa viwanja 20,000. Nasisitiza kama ambavyo nilisisitiza miaka kadhaa iliyopita, tunaomba ifanyike audit ya vile viwanja, kwa sababu tunajua sekta ya ardhi ilikuwa imegeuzwa sehemu ya wajanja wachache kujinufaisha kwa maslahi yao. Tukiweza kufanya audit katika hivi viwanja, tutajua nani anamiliki nini, tutajua viwanja vya wazi ni vipi na tutajua viwanja vya huduma za jamii ni vipi. Kuanzia hapo tutaweza kujua Serikali iliweza kufanikisha ama ilishindwa na turekebishe nini. Kwa hiyo, naomba sana atueleze kama hiyo audit itaanza kufanyika na ifanyike lini, atagundua madudu mengi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulizungumza suala la migogoro ya Jimboni kwangu, eneo la Nyakasangwe, Kata ya Wazo. Huu mgogoro ni wa muda mrefu, utatuzi wa huu mgogoro ulishaanza kufanyiwa kazi toka mwaka 1998 na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mheshimiwa Makamba. Kuna nyaraka zote tumezipeleka Wizarani kwake na barua ya mwisho tumepeleka tarehe 20 Januari, 2017.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro huu unahusu wananchi wasiopungua 4,000, tunamwomba Mheshimiwa Waziri, tulimaliza hatua mbalimbali za kisiasa na za kitaalam, tukafikia hatua ya kuanza kutambua wananchi kwa kushirikiana na MKurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, kwa sababu tunajua yeye ndiyo mamlaka yenye uwezo wa kushughulika na masuala ya ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunataka kufikia mwisho, hawa Viongozi vijana mnaowateua teua hawa wanaopenda kuuza sura, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, akaja akataka kuvuruga mambo wakati Ofisi ya Mkurugenzi na Viongozi waliopita wote wa Mkoa na Wilaya tulikuwa tumeanza kufika sehemu ya mwisho. Sasa yule dogo sishughuliki naye kwa sababu siyo saizi yangu, mimi nakwenda kwa Mheshimiwa Waziri. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu mimi na Mkurugenzi tumeshafika sehemu nzuri na wananchi, tumekaribia kumaliza tulete Wizarani, dogo anataka kuingilia, sasa tumemwandikia barua tarehe 20 Januari, 2017 tumeambatanisha nyaraka zote, tunaomba Ofisi yake ilitafutie ufumbuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunataka kulimaliza, juzi amekuja mtu ama Mtaalam Mshauri anazunguka eneo la Nyakasangwe, Kampuni ya Nari, anasema yeye ametumwa na Kiwanda cha Wazo na kwamba Kiwanda cha Wazo kilipewa mamlaka ya kufanya utafiti ama leseni ya kufanya utafiti na kwamba lile eneo inasemekana lina madini, kwa hiyo wameanza kufanya survey na kuweka alama na kuzua taharuki kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hili suala nimeshakabidhi Wizara ya Nishati na Madini. Kwa hiyo, wakati Mheshimiwa Waziri ananipa majibu yake kama Waziri wa Ardhi natarajia vilevile Waziri wa Nishati na Madini anayekaimu ambaye ni Naibu sasa, atatoa majibu ili wananchi wangu waache kuishi kwa taharuki, hilo la Nyakasangwe nimemaliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Boko kwa Somji, nimesema leo naenda Kijimbo jimbo zaidi kwa sababu wananchi wa Kawe ndiyo wananiweka mjini. Suala la eneo la Boko na lenyewe liko Wizarani kwake ni mgogoro wa muda mrefu sitataka kuongea kwa kina hapa, lakini tokea mchakato wa upatikanaji wa hili eneo, toka kipindi kile cha sheria za Mkoloni, taratibu hazikufuatwa. Nitampelekea Mheshimiwa Waziri kabrasha ili aweze kulifanyia kazi kwa sababu kuna matapeli pale wanazunguka, wanasema ooh, tunataka tulipwe fidia, sisi ni wamiliki halali wakati mmiliki halali alishakufa, wakati Serikali iliishataifisha eneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa namwamini Mheshimiwa Waziri katika kufanya maamuzi wala sina shaka katika hilo na ardhi ni mali ya umma, tusiruhusu wajanja wachache ambao walitumia ombwe lililokuwepo, wakati watu wengine wanaongoza Wizara ya Ardhi kuweza kuvuruga mustakabali wa wananchi. Kwa hiyo, naomba suala la Boko kwa Somji tulimalize ili basi kama ambavyo tulivyopima Chasimba, tupime Nyakasangwe, tupime Boko kwa Somji maisha ya wananchi wangu yaende kuwa mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana tulikuwa tunazungumza kuhusiana na suala la ardhi, umiliki wa ardhi na nafasi ya mwanamke katika umiliki wa ardhi, nimwombe Mheshimiwa Waziri wanawake wanatengeneza asilimia zaidi ya 80 ya labour force ya kilimo, tunaomba sheria zinazowakandamiza hawa wanawake, zisipofanyiwa marekebisho Sheria za Kimila, hata kama tuwe na sheria nyingine nzuri kwa kiwango gani hawa wanawake hatutawasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakuomba kwa dhati, kweli Sheria ya Ardhi Namba 4 inasema haki, Sheria Namba 5 inasema haki, lakini sheria zetu zinatambua Sheria za Kimila. Sasa kama haya mambo ambayo yanamilikiwa kimila yasipokuwa formalized, tutakuwa tunafanya biashara kichaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, tuangalie haya mambo kwa kina, tusaidie wanawake ili tuweze kujenga Taifa letu kwa usawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, leo nimekuwa mpole kidogo, nashukuru na nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi anayoifanya.