Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Stanslaus Shing'oma Mabula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyamagana

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi jioni hii. Nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kunipa afya, kwa sababu ya muda naomba nami kwa uchache sana nichangie Wizara hii muhimu kabisa, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze tu kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake kwa kazi nzuri wanayoifanya, katika kuhakikisha Tanzania ambayo tunatamani kuona imepangwa basi angalau wameanza na miji kadhaa ambayo kwa kweli kama tutafanikisha, tunaweza tukafikia hatua nzuri sana, kwa sababu tunafahamu upangaji wa ardhi unaendana na uimarishaji wa uchumi bora kwa maisha ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli uisiofichika kwamba ardhi kubwa ya Tanzania bado haijapangwa sawa sawa na miji mingi tuliyonayo karibu miji yote hata Mji wa Dodoma ambao ulikuwa umeshaanza kupangwa kwa namna fulani, sasa hivi tunakoelekea kama hakutakuwa na usimamizi mzuri, tutegemee Miji aina ya Manzese na hapa Dodoma itakuwepo mingi sana na maeneo mengine mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa MWenyekiti, nianze tu tena nirudie kumshukuru Mheshimiwa Waziri, nakumbuka mwaka 2014, moja ya Miji ambayo ilikuwa imetengewa mkakati wa kupanga Mipango Miji Kabambe, Mji wa Mwanza ulikuwa ni moja kati ya miji karibu 14. Fedha nyingi sana ya Serikali imetumika pale katika kuweka mkataba na kampuni moja SULBANA International wa zaidi ya dola milioni tano za Kimarekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa sababu kwa mwaka huu peke yake, ndiyo mwaka ambao kazi kubwa sana imefanyika. Hivi tunavyozungumza karibu asilimia 90 ya kazi hii na timu hii kwa kweli ndugu Waziri naomba niipongeze sana timu aliyoikabidhi kazi hii kwa sababu inafanya kazi nzuri sana. Matarajio yangu ni kwamba kazi hii itakapokuwa imekamilika kwa sababu Mwanza ndiyo inaonekana kuwa ya kwanza, kwa namna Watendaji na Watumishi hawa walivyojitoa kufanya kazi hii usiku na mchana itakuwa imetuzalishia matunda makubwa zaidi na itapunguza kero nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, iko shida moja tu Mheshimiwa Waziri lazima tukubaliane kwamba mipango hii kabambe ya uboreshaji wa miji, pamoja na jitihada nyingi hizi ambazo inafanya kama tutaiacha, kama baada ya kukamilika hatutaona umuhimu wa kuipeleka kwa haraka ili ikamilike, tunakusudia miaka 20 itakuwa imetosha kabisa kuhakikisha kazi hii imekamilika na projection zake ziko wazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema miaka 20 sasa hivi kwa Mwanza na Ilemela kwa maana ya Nyamagana na Ilemela ukitafuta makazi yako zaidi ya laki moja na sitini lakini wataalam wanatuambia miaka 20 ijayo tutakuwa na makaazi zaidi ya 520 wakati nyumba moja peke yake kuna wakaazi wasiopungua watano. Kadri miaka inavyokwenda watakuwa wanashuka kwa sababu tunaamini uchumi utakuwa umekua, elimu itakuwa imekua kubwa sana na kuzaliana kutapungua sana tofauti na sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, wito wangu kwenu ili hili liweze kufanikiwa vizuri ni lazima tuhakikishe, katika miji yote huu ndiyo mji wenye square metres za mraba 472 peke yake unaotakiwa kwenda kufanyiwa kazi, siamini kama unaweza kutuchukulia muda mrefu sana kuutengeneza Mji wa Mwanza ukawa ni moja kati ya Miji bora kabisa Tanzania kuliko ilivyo sasa. Tunaita Mji wa pili kwa ukubwa lakini ni kwa maandishi tu kutokana na uchangiaji wa uchumi siyo kwa muonekano wa mji kiuhalisia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo sasa, tunafahamu kwamba kwa nini sasa hivi tunalazimisha na tunasisitiza sana urasimishaji wa makazi. Utakubaliana na mimi kwamba tunahimiza urasimishaji wa makazi kwa sababu muda mrefu tuliacha ujenzi holela ukatokeza sana. Urasimishaji wa makazi tafsiri yake, tunataka tutoke kwenye makazi holela tuje sasa kuyafanya makazi haya yawe rasmi. Mheshimiwa Waziri atakubaliana na mimi, pamoja na jitihada zote hizi tunazofanya, namshukuru sana siku chache zilizopita amefanya ziara Mwanza, pale ametema cheche kali sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyozungumza na Mheshimiwa Waziri tayari invoice 19,000 zimeshaandaliwa na zaidi ya 3,000 zimeshakwenda kwa wananchi na 800 wameshalipa. Inaonekana kulikuwa na uzembe mkubwa. Kwa hiyo, tuendelee kutoa nafasi, lakini tuendelee kurudisha fedha hizi ambazo zinatokana na malipo ya ardhi, zitasaidia sana kuhakikisha kazi hizi zinakwenda haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu tunataka kuimarisha makazi yetu vizuri tunaondoa makazi holela, liko tatizo moja kubwa na tatizo hili ndilo linaloikabili nchi nzima. Katika maeneo ipo michoro ilishaandaliwa miaka 10, 20 au 30 iliyopita lakini hayajawahi kuelekezwa sawasawa na mwananchi hajawahi kupata elimu vizuri kwamba hii michoro ikishapita huruhusiwi kujenga chochote humu ndani. Matokeo yake maeneo yamevamiwa na leo ukitaka kwenda kumwondoa mwananchi ambaye ulimfanyia mchoro miaka 20 iliyopita na hukumpa utaratibu unakwenda kuonekana ni mvamizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na urasimishaji makazi haya tunaulizana, ninayo maeneo kwenye Jiji la Mwanza na Jimbo la Nyamagana, ukichukua maeneo ya Mtaa wa Ibanda, Mtaa wa Swila, Mtaa wa Bukaga, Mtaa wa Kasese kwenye Kata za Nyegezi, Kata ya Igoma na Kata ya Mkolani, yako zaidi ya makazi elfu mbili, wapo wananchi wengi, walishajenga siku nyingi, michoro imetengenezwa. Hakuna namna tunaweza kuwasaidia wananchi hawa pamoja na kutaka kupanga Mji wa Mwanza vizuri kama hatutafumbua tatizo hili kubwa. Kinachoonekana leo ili tuweze kufumbua tatizo hili ni kwenda kuvunja makazi ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatutaendana na kasi ya Mheshimiwa Rais anayoizungumza, hatutaendana na kauli ya Mheshimiwa Rais ya kuwasaidia wanyonge. Sasa ni lazima tumsaidie Mheshimiwa Rais, ni lazima tuoneshe njia watalaam huku wanasema, kwa mfano miaka karibu 25 iliyopita eneo la Mkolani, Mtaa wa Kasese kuanzia kona ya Nyegezi pale Nyegezi, unakuja Butimba, unakuja Mkolani watu walishapima miaka mingi, Halmashauri wanasema mchoro wao unaonesha barabara ni mita 100, TANROADS wanasema barabara yetu ni mita 60. Nani anaingia katikati hapa kutatua mgogoro huu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo watu kwenye mita zaidi ya 40, Halmashauri inasema hii ni buffer zone na watu wana miaka dahari mle ndani, leo wanatakiwa wavunjiwe nyumba zao, zaidi ya watu 1,600. Mheshimiwa Waziri najua yeye ni mtu wa huruma na hata akienda kwenye eneo hili mwenyewe anaweza kushangaa na akashangaa watalaam tulionao, kwa nini hawawezi kuchukua maamuzi mpaka wakubwa wafike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, nimeshazungumza na mama yangu, jirani yangu, dada yangu Mheshimiwa Angelina, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, amesema wataliangalia kwa makini na nimeshazungumza na Mheshimiwa Waziri vizuri na najua ameshanisaidia sana. Kwa hiyo, naendelea kuwaomba tunao wajibu wa kuwasaidia Watanzania. Mwanza tunayotaka kuitengeneza leo uwe mji wa mfano hatutaonesha kama ni mji wa mfano kama hatutatatua changamoto hizi, badala yake tutaendelea kujaza kero kwa wananchi na hii itakuwa siyo sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia tu nizungumze suala moja ambalo amelizungumza Ndugulile hapa asubuhi. Bado hakuna elimu hata kwa watalaam wetu kule chini, tunazungumza asilimia 30 ya fedha za kodi ya ardhi zinazokusanywa, leo ukitaka kuuliza, hata Watendaji hawajui kama zile fedha hazitakiwi kurudi tena lakini watendaji wenyewe wanajua bado tunadai fedha nyingi. Fedha hizi zikija zitasaidia kumaliza kero ya kupima ardhi kwenye maeneo mengi ambayo tumeshindwa kupima mpaka leo, hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri waliangalie. Kama ilishaamriwa hivyo na Bunge hili likapitisha sheria, uende waraka kule chini kwa Watendaji kwenye Halmashauri walifahamu hili, kwamba fedha hizi wanazolipa mpaka leo Halmashauri ya Jiji la Mwanza imeshakusanya kodi ya ardhi zaidi ya bilioni moja na milioni mia tisa thelathini na mbili, lakini tunategemea asilimia 30 ya fedha zile iweze kutusaidia kukamilisha shughuli nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana hata zoezi la urasimishaji makazi kuna wakati lilikwama kwa sababu vifaa vilikuwa hakuna. Mheshimiwa Waziri alivyoondoka hatujui fedha zilipatikana wapi, computer zikanunuliwa, kila kitu kikawekwa na kazi hii niliyomwambia zaidi ya wananchi 800 wameshafanyiwa malipo, ndiyo matokeo ya matumizi ya fedha. Lazima tukubali kutumia fedha ili tujenge miji yetu na plan hizi tulizonazo ziweze kufanikiwa. Hatuwezi kufanikiwa kama hatujaona umuhimu wa ardhi na matumizi ya ardhi haya ni lazima tuyafanye for public consumption, tukifanya ni ya kwetu binafsi hatuwezi kufanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, wananchi wa Jiji la Mwanza na Jimbo la Nyamagana wanayo masikitiko makubwa, yako maeneo yao wamekuwemo kwa muda mrefu lakini leo wanaonekana wavamizi, kwa sababu tu hatukuchukua hatua mapema, hatukutoa elimu mapema. Tutoe elimu, tuwaoneshe wananchi wapi panastahili na wapi pasipostahili, tutafanikiwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, nawapongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanayoifanya. Tuendelee kuijenga Tanzania na wananchi wanyonge wapate tiba. Ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.