Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami naomba nitumie fursa hii kumpongeza Waziri mwenye dhamana pamoja na Naibu wake, wanafanya kazi nzuri sana, kazi ambayo haiwezi ikatiliwa shaka na Mbunge yeyote makini humu ndani.

Vilevile naomba nimpongeze Katibu Mkuu wa Wizara ndugu yangu Kayandabila nae anafanya kazi nzuri sana, tumeona jinsi tatizo la ardhi katika nchi yetu linavyozidi kutatuliwa siku hata siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizo kuna tatizo kidogo katika eneo langu la Halmashauri ya Lushoto, kuna Mwekezaji mmoja wa nchi jirani ya Kenya amemilikishwa mashamba matatu lakini ameshindwa kuyaendeleza.

Sasa katika Halmashauri yetu tuna uhaba mkubwa sana wa ardhi na ardhi hii hekari 4,019 zimekaa tu domant. Kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, kwamba huyu Mwekezaji anapita na anatoa lugha za kashfa mitaani kiasi kwamba anajifananisha kwamba yeye mmoja ni sawa na Watanzania watano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa tafsiri rahisi ya yeye mmoja na Watanzania watano ni kwamba hapo kuna Mheshimiwa Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Waziri mwenye dhamana na Mbunge. Kwa hiyo, sisi watano ni yeye mmoja. Sasa naomba nimwachie hilo Mheshimiwa Waziri aangalie namna gani tunafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shamba la kwanza lina hati namba 41/44,hekari 562; shamba la pili ni hati namba 17/ 146, hekari 1188; shamba la tatu ni namba 11/247, hekari 2,442; na tumeshatoa notice ya revocation kuanzia tarehe 14 Julai, 2016 na hakujibu na tarehe 9 Desemba, file limeshafika kwa Kamishna wa Ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Kamishna wa Ardhi Kanda ya Kaskazini kwa masikitiko makubwa yule mama ambaye alikuwa pale kabla hajahamishwa amekalia file na kila tukiuliza analeta sababu ambazo siyo za kiofisi. Jambo lolote la kiofisi linapaswa kujibiwa kwa nyaraka za kiofisi, lakini mama huyu kila wakati ukiuliza anatoa majibu kwamba file halijakamilika, sijui notice zimekosewa. Sasa haya ni mambo ya technical ambayo wananchi hawapendi kuyasikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, kwenye barua yetu Afisa Mteule wa Ardhi ameandika wazi kwenye hitimisho, mwekezaji katika mashamba ya katani Mnazi ameshindwa kwa kiasi kikubwa kuyaendeleza mashamba anayoyamiliki. Katika hekari 4,192 ni hekari 500 tu ndizo ambazo ameziendeleza kwa kupanda mkonge na kuvuna, hekari 1,942 mkonge uko porini kwenye vichaka hautunzwi kabisa. Hekari 1023 ni msitu mtupu ambao unatumiwa na wafugaji wa kijamii ya kimasai kwa malisho ya mifugo yao. Pia mmiliki huyu hajalipa kodi ya ardhi tangu 2004/2005 mpaka sasa na anadaiwa zaidi ya shilingi milioni 42.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wawekezaji kama hawa kwa kweli sidhani kama wana nafasi katika Serikali hii ya Awamu ya Tano. Namsihi sana Mheshimiwa Waziri tuchukue hatua stahiki. Wananchi hawa wa Lushoto kama nilivyotangulia kusema wana uhaba mkubwa wa adhi. Kwa hiyo ardhi hii ndio angalau tukipata na sisi tunaweza tukaingia na wenzetu hawa kuingia katika economic zone tukapata angalau mahali pa kuwekeza. Kwa hiyo, namsihi sana, namwamini Mheshimiwa Waziri, sijawahi kutilia shaka uwezo pamoja na mama yangu pale Angelina Mabula nawapongeza sana, ahsanteni sana.