Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, hizo dakika zangu mbili zilizoliwa ulinde. Kwanza kabisa naomba niunge mkono Hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni. Hata hivyo kwa kuwa muda ni mchache naomba nijielekeze kwenye hoja mahsusi katika Wizara hii. Kwanza kabisa naomba niende kwenye mgogoro wa ardhi katika vijiji vinavyozunguka hifadhi ya Tarangire.
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro hii imezungumzwa muda mrefu lakini inavyoonekana hakuna mafanikio. Nimwambie Mheshimiwa Waziri kwamba leo hii nimekuja na document ambayo inaonesha Sheria iliyounda vijiji hivyo na GN ya Serikali. Naomba nimkabidhi kitabu hiki ili aende akatatue mgogoro wa Gijedabou, Gedamara na Ayamango. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye shamba la mwekezaji Hamir Estate iliyofutwa umiliki wake na Mheshimiwa Rais mwaka 2015, Novemba. Shamba hili lilifutwa na Mheshimiwa Rais tarehe 4 Novemba, 2015, lakini cha kushangaza mwekezaji huyu pamoja na kusitishwa umiliki wa shamba hili bado anaendelea kulitumia shamba hili, jambo ambalo linaibua mgogoro mpya kwa wanakijiji na wananchi wa Bonde wa Kiru. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, shamba hili wakati Mheshimiwa Rais analifuta, hakukuwa condition yoyote iliyowekwa, hakuna maelekezo yaliyoelekezwa kwamba lipelekwe kwa wananchi au liende wapi. Sasa tunaomba Mheshimiwa Waziri hili jambo alifanyie kazi, shamba limefutwa, tujue linakwenda kwa wananchi au linakwenda wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Mheshimiwa Waziri mwenye Wizara husika sasa atuletee sheria mpya ya kubadilisha matumizi ya ardhi. Kwa mfano, sasa hivi kumekuwa na sheria inabadilishwa matumizi ya ardhi ya kilimo inakuwa ardhi ya makazi, hii imeleta mgogoro. Kwa mfano Babati Bonga ilikuwa ni matumizi ya kilimo, Arusha Usa River kulikuwa ni matumizi ya kilimo, leo ukikuta ni majumba matupu. Vile vile mfano mzuri, unaweza ukahamisha watu wakakaa jangwani ukawapelekea maji na wanaweza kuishi, lakini huwezi ukapelekwa jangwani ukalima ukaivisha mazao. Sheria hii iletwe hapa iingizwe katika moja ya sheria ya matumizi ya ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na nyaraka hizi Mheshimiwa Waziri naomba nimkabidhi barua ya ubatilisho wa umiliki juu ya shamba la huyu mwekezaji Hamir Estate kitalu namba 1396 eneo la Bonde la Kiru, Wilayani Babati.
Naomba nimkabidhi nyaraka hizi kwa sababu muda wangu hautoshi ili aone ni jinsi gani yeye anadanganywa. Mgogoro wa Bonde la Kiru umekuwa ni VICOBA vya baadhi ya viongozi. Mgogoro huu ni wa tangu mwaka 1998, mwaka 2009 mfanyakazi wa mashamba ya Kiru mchana kweupe saa kumi alikatwa shingo akaletwa Mrara; leo hii tunasema tunashughulikia mgogoro. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi namjua Mheshimiwa Waziri anafanya kazi, hata haya matokeo ya hili shamba kufutwa ni pamoja na juhudi zake. Kwa sababu ameanza, aende akamalizie hii ngoma. Amepongezwa sana lakini haimaanishi kwamba mimi simpongezi lakini kuna mambo mengine yanatuumiza. Hiki kitabu ukiangalia kuna magofu ya nyumba za watu, watu wanaishi kwenye nyumba za nyasi hawaruhusiwi kuendeleza makazi yao, hawaruhusiwi kulima miaka 11. Hebu ajichukulie sasa, ni miaka 11, wewe ni baba na una watoto sita, chakula chako ni cha kuombaomba, inakuwaje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri Waziri atakuwa amenisikia kwa haya machache, naomba Mheshimiwa Waziri nimkabidhi hizi nyaraka. Naunga mkono hotuba ya Kambi Rasmi. Ahsante.