Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Ummy Ally Mwalimu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza na mimi niseme naunga mkono hoja. Lakini pili, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kusimamia vyema raslimali zetu za nchi.

Mheshimiwa Spika, kadiri tunavyosimamia fedha za nchi maana yake tunawekeza pia katika kuboresha huduma za jamii ikiwemo huduma za afya. Nitoe mfano bajeti ya dawa ya Serikali mwaka 2015 ilikuwa shilingi bilioni 24 mwaka 2016 shilingi bilioni 251, mwaka 2017 tunazungumzia takribani shilingi bilioni 269; kwa hiyo kuna watu wanatakiwa waangalie uhusiano wa hatua ambazo tunachukua katika kusimamia raslimali za nchi, lakini pia katika kuboresha huduma za jamii ikiwemo huduma za afya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kupitia jitihada za Mheshimiwa Rais tumeona kwamba kwa mara ya kwanza hakuna Mtanzania mgonjwa atakuwa analala chini kwa sababu tu ya ukosefu wa vitanda au magodoro. Endapo mgonjwa atalala chini ni kwa sababu hospitali au kituo hicho hakina sehemu ya kuweka vitanda au magodoro, hizi zote ni juhudi za Mheshimiwa Rais, Dkt.John Pombe Magufuli.

Mheshimiwa Spika, tumeona kwa mara ya kwanza Mheshimiwa Rais akisambaza vifaa katika halmashauri zote nchini haijawahi kutokea katika historia ya Tanzania. Tumeona kwa mara ya kwanza ambulance zaidi ya 67 Mheshimiwa Rais akizisambaza nchi nzima, haijawahi kutokea katika historia ya Tanzania.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naomba sasa pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha, kaka yangu Dkt. Mpango na Naibu Waziri, wifi yangu Dkt. Ashatu Kijaji na wataalamu wa Wizara ya Fedha kwa kazi nzuri waliyofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Sekta ya Afya tutanufaika sana na bajeti hii ambayo inapendekezwa. Kwa mfano Suala la kuendelea kutoza ushuru wa forodha wa asilimia 10 katika sukari ya viwandani maana yake ni kwamba tunawekeza katika utengenezaji wa dawa, viwanda vya dawa vinatumia pia sukari ya viwandani. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mpango tunakupongeza sana kwa sababu asilimia 80 ya mahitaji yetu ya dawa tunayanunua kutoka nje ya nchi. Kwa hiyo, sasa hivi tunataka kuhakikisha kwamba dawa zinatengenezwa ndani ya Tanzania, hii ni hatua nzuri na tunaipongeza sana.

Mheshimiwa Spika, lakini pia tunapongeza bajeti hii kwa sababu imefuta ada ya kuanzisha maduka ya dawa. Tumesema MSD haiwezi kuwa na dawa aina zote kwa asilimia 100; kwa hiyo, lazima yawepo maduka binafsi ya dawa. Mheshimiwa Mpango tunakupongeza kwamba umefuta ada ya kuanzisha maduka ya dawa maana yake dawa zitapatikana katika vijiji, katika mitaa yetu na katika makazi yetu. Dawa si biashara, dawa ni huduma tunawapongeza sana Wizara ya Fedha kwa kuliona suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ambalo tunaona sekta ya afya tutanufaika sana na bajeti hii ni suala la kuwatambua rasmi wafanyabiashara wadogo wadogo wamachinga, mama ntilie, maana yake tutakapowatambua ndiyo pia itakuwa rahisi kwetu kuwafikia katika huduma za social security (huduma ya hifadhi ya jamii) na hapa nazungumzia bima ya afya. Endapo wafanyabiashara hawa wadogo tutaweza kuwatambua maana yake pia itakuwa rahisi kwetu sisi kuwafikia na kuwahimiza wajiunge na bima ya afya.

Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa ya kupata huduma za afya kwa Watanzania ni suala la gharama ya fedha, kwa hiyo tunahimza wananchi wote wajiunge katika mifuko ya bima ya afya ili sasa iwe rahisi kupata dawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho ambalo nilitaka kupongeza bajeti hii ni suala pia la kufuta tozo katika mabango ambayo yanaonesha zahanati, sehemu za huduma, vituo vya afya na hospitali, hili ni jambo zuri kwa sababu litakuwa pia ni rahisi kwa wananchi hasa kwa wakati wa dharura kuhakikisha kwamba wanapata huduma za afya kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizi sasa nijikite katika kujibu hoja tatu ambazo zimetolewa na Waheshimiwa Wabunge.

Hoja ya kwanza imeongelewa na Mheshimiwa Lucy Mayenga, naye alikuwa anazungumzia kuhusu utendaji kazi wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, na kwamba kuna kampuni inaitwa Techno Net Scientific Limited ambayo inaingiza kemikali bila kufuata sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunamshukuru sana Mheshimiwa Lucy Mayenga, tunakubaliana kwamba ndiyo changamoto hii ipo lakini tumeibaini na sasa hivi tayari Mkemia Mkuu wa Serikali anashirikiana na vyombo vingine vya dola kuhakikisha kwamba tunampeleka mahakamani haraka iwezekanavyo Kampuni hii ya Techno Net Scientific ambayo inajihusisha na shughuli za kuhifadhi na kuuza kemikali za viwandani na majumbani wakati usajili wake umeisha toka tarehe 30 Aprili, 2016. Kwa hiyo, Mheshimiwa nikuthibitishie kwamba uchunguzi umekamilika na ndani ya muda mchache tutampeleka mahakamani mhusika.

Mheshimiwa Spika, nitumie Bunge hili kutoa onyo kwa wote wanaojihusisha na kuingiza kemikali za viwandani na majumbani kuhakikisha kwamba wanazingatia sheria.

Mheshimiwa Spika, mwezi wa tisa tulikuja Bungeni tukaleta sheria ya kuibadilisha Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali iwe Mamlaka (Authorty) maana yake ni kutaka kuipa nguvu na uwezo wa kuweza kusimamia shughuli zake mbalimbali ikiwemo kusimamia kemikali za viwandani. Kwa hiyo, Mheshimiwa Lucy Mayenga nikusihi dada yangu kwamba ndugu yangu tusiifute hii ofisi kwa sababu licha ya kusimamia shughuli za kemikali, lakini pia ina majukumu mengine ya kuhakikisha inasimamia Sheria ya Teknolojia ya Vinasaba, lakini pia inajihusisha na sheria zinazohusika na vilelezo za sampuli katika makosa ya jinai na Mheshimiwa Mwingulu anaitegemea sana katika kukamilisha mashauri mbalimbali ya kijinai ikiwemo Mahakamani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la pili ambalo limeelezwa na Mheshimiwa Mbunge Aeshi Hilaly ni suala la uvutaji shisha, kwamba je shisha ina madhara gani? (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)