Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. CONSTATINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba pia nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya na kuweza kupata nafasi ya kuchangia kwenye bajeti hii ya mwaka 2017/ 2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo wazungumzaji wengine waliotangulia wamesema, mimi ni miongoni mwa Wabunge ambao tunatoka kwenye maeneo ambayo uchimbaji wa dhahabu ni kazi kubwa kabisa ya maisha ya kwetu ya kila siku. Kwa hiyo, juhudi za Mheshimiwa Rais za kupambana na namna ambavyo madini haya yatakuwa na manufaa kwa wananchi sisi wananchi wa Jimbo la Geita Mjini na Mkoa mzima wa Geita tunazipa kipaumbele kikubwa na tunaziunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuishauri Wizara ya Fedha namna ambavyo inapoteza fedha nyingi kutokana na mikataba mibovu ambayo ilikuwepo. Nilipata nafasi ya kuchangia mwaka jana na sikuona mabadiliko yoyote yale wala hatua zilizochukuliwa. Kampuni nyingi zinazofanya kazi na migodi mikubwa ni kampuni za nje na migodi hii mikubwa imepewa uwezo inapotaka vipuli au bidhaa zozote inaweza kumpa yeyote aliyeko ndani au nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kampuni hizi zinazopewa kazi nyingi hazina ofisi Tanzania. Wanapokuletea orodha ya kampuni ili uweze kwenda kudai service levy wanakupa orodha ya kampuni ambayo ipo Canada, Australia, South Africa ambao hawana ofisi hapa, hawana license hapa wala hawana wafanyakazi. Lakini gharama ya manunuzi yao yameingizwa kwenye corporate tax, kwa hiyo, yanapunguza sehemu ya faida ambayo Serikali ingeweza kulipwa na ndiyo maana migodi mingi haiwezi kulipa kodi kwa sababu wanaweza ku-deal na kampuni iliyoko Canada ambayo ninyi Serikali hamna kumbukumbu nayo, haina ofisi, haina address, matokeo yake ni kwamba sisi tunapoteza pesa nyingi kwa sababu hatuwezi kwenda kudai service levy. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nataka kumkumbusha Mheshimiwa Waziri, niliseme hili mwaka jana na miongoni mwa makampuni haya ni makampuni ya bima. Kampuni hizi za bima zime-insure wanafanyakazi lakini wana- insure strong room, processing, mgodi mzima. Kampuni hizi kubwa za bima unapoomba ile orodha ya makampuni ya service levy hawakuletei kwa sababu hazipo Tanzania. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Waziri, hii ni sehemu kubwa ambayo tunapoteza pesa nyingi sana. Kama kampuni hii itakuwa ipo Dar es Salaam au ipo Mwanza watakuwa na ofisi, watalipa working permit, watalipia wafanyakazi wao na matokeo yake Serikali itapata fedha na itapata kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Halmashauri tunataka tupate hii service levy kama Serikali wanaona hii pesa ni ndogo hawana sababu ya kuyafanya makampuni yaje Tanzania, wayaache yakae nje. Sisi tunaomba watusaidie wawalazimishe sheria watu hawa wafungue ofisi Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, mwaka jana nilishauri hapa nikasema tatizo kubwa tunakwenda kwenye viwanda lakini ili viwanda viweze kufanya kazi lazima kilimo kwanza kipewe kipaumbele. Watu wengi wamezungumza kuhusu kilimo. Tatizo ninaloliona kwenye kilimo tangu tumeanza kuzungumza unaona transformation inayotupeleka kwenye kilimo ambacho kitalipa inakwenda kwa kasi ndogo sana. Mtu anayehamasisha viwanda ana kasi kubwa. Viwanda vinahamasishwa kwa kasi kubwa, raw material ni products za kilimo, lakini transformation ya kufanya kilimo kiweze kusaidia viwanda inakwenda kwa kasi ndogo ndogo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe tu mfano, sisi Geita tunalima mananasi, mbegu ya nanasi ambayo ingeweza ku- supply au kuuzwa nje kwa sababu tunaambiwa mananasi tuliyonayo yanafanana sana na madawa ya kienyeji wala huwezi kuuza nje. Ili tuweze kupata product ya nanasi ambayo inaweza kuuzwa nje nilidhani kwa sababu nchi inajua tunalima nanasi, tayari wangekuwa wamepeleka wataalam wakatupa mbegu za kisasa zile mbegu ambazo tunaweza tukauza yale mananasi nje, tukawa na soko ambalo lingeweza kuwabadilisha wakulima wa mananasi katika Mkoa wa Geita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu tumeanza kuzungumza kuhusu kilimo, wakulima wa mpunga wanalima kienyeji vilevile walivyolima miaka kumi iliyopita. Tunafikiria kuongeza ukubwa wa mashamba, sio ukubwa wa uzalishaji. Kwahiyo, matokeo yake, mbegu za mpunga zile zile ambazo tulilima miaka kumi iliyopita ndizo tunazozungumzia kuendelea kulima kwenye mfumo wa viwanda. Kwa hiyo, haiwezekani viwanda tunavyovizungumza vikaja viwaka productive kama hatuwezi kufikiria kubadilisha kabisa namna ambavyo tunalima. Ukienda kwa wakulima wetu wengine wanalima ukubwa wa shamba. Anaweza kulima ekari kumi akapata gunia tano za mahindi, lakini kumbe angeweza kulima heka mbili akapata gunia 60 za mahindi na eneo lingine akalima kitu kingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mabadiliko tunayotaka kwenye kilimo lazima yaendane na speed ya ujenzi wa viwanda tunavyovifikiria vinginevyo tunakwenda mahali tutajenga viwanda, halafu tutaagiza raw material kutoka nje. Alisimama hapa Waziri wa Kilimo akasema hata Bakhresa maziwa anayopaki kwenye pakiti mengine ni ya unga kwa sababu maziwa hakuna. Lakini leo utaona vita ya Serikali na mifugo, vita ya Serikali ya wafugaji ni kuhakikisha wale wafugaji wanafilisika badala ya kuwasaidia wale wafugaji waweze kutengeneza uzalishaji mkubwa wa maziwa ili Bakhresa apate maziwa. Bila kufanya hivyo, hata viwanda tunavyovihamasisha vije vitakuja vifungwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la pili nilitaka kuona mchango wa Idara ya Uvuvi kwenye uchumi wa Tanzania. Ziwa Victoria miaka kama 15 ya nyuma tulikuwa tunapata pesa nyingi sana za kigeni kutokana na uvuvi, taratibu taratibu productivity imeendelea kushuka sasa tunabuni mikakati mbalimbali kwa ajili ya kuwalinda wale samaki. Lakini tatizo kubwa lililoko Ziwa Victoria, lile ni ziwa, uvuvi ni mkubwa hakuna juhudi za ziada za Serikali za kuhakikisha kwamba tunapandikiza vifaranga vya kutosha kwenye Ziwa Victoria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe tu mfano, kuna maeneo mengi sana yemetengwa kwa ajili ya samaki kuzaliana na yale maeneo yaliyotengwa, Serikali ingeweza kuwa na mkakati kabambe wa kuingiza vifaranga hata milioni 100 kila mwaka vifaranga wa sangara unawaweka katika Ziwa Victoria, wakisaidiana na wale ambao wanazaliana kwa mfumo wa kawaida, samaki hawawezi kuisha katika Ziwa Victoria. Tatizo letu tunavuna tu, tunavuna tu matokeo yake badala ya kugundua kwa nini samaki wanapungua tunaweka masharti ya kuwaambia wavuvi wapunguze size ya nyavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema hapa wakati nachangia kwenye Wizara ile na bahati nzuri Waziri hakutaka kulijibu. Amefanya operesheni ya kukamata wavuvi wanaovua samaki kwa nyavu ambazo zina macho zaidi ya 26 lakini hiyo nyavu ambayo inatumika…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)