Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Philipo Augustino Mulugo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Songwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na mimi kwa kupewa nafasi dakika tano hizi za kuchangia Wizara Kuu ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina hoja ndogo sana leo, Mheshimiwa Dkt. Mpango naomba unielewe, nakuwa nazungumza kila siku kwenye hotuba zangu namna ambavyo Wizara yako, hususan pale Hazina, sijui kuna mfumo gani mnaoweka, jinsi mnavyopendelea kutuma fedha kwenye Halmashauri. Baadhi ya Halmashauri hatupati fedha, hata kama ni hizo hela ambazo mnakuwa mmekusanya ndogo baadhi ya Halmashauri hatupati fedha, tunalalamika kila siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nasema kila siku hapa, nina Wilaya mpya lakini sina maji, sina barabara ya lami, sina vijiji vyenye umeme kama vijiji vingine, sina kiwanda hata kimoja, hata Chuo cha VETA hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2013 niliambiwa nitafute eneo, tukatafuta eneo ekari 100 pale Mkwajuni na hatimiliki ipo, lakini mpaka leo hakuna mikakati yoyote ya kuniletea VETA pale Wilaya ya Songwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kila siku nasema, nina Wilaya mpya sina Hospitali ya Wilaya, sasa nataka kuona bajeti ya mwaka huu kama mnaniletea hivi vitu, kwa sababu sehemu nyingine wanavyo. Sasa mnapogawa fedha pale Hazina kwa nini hakuna Kamati Maalum ambayo angalau ingekuwa inatenga kwamba okay, hiki kinakwenda Same, Same wana hiki na hiki, labda hiki kinakwenda Halmashauri ya Tunduru, Tunduru hawana hiki basi hiki kiende kwenye Halmashauri fulani, yaani kuwe na relation fulani ya kuona kwamba Halmashauri nyingine wana hiki basi na hawa wapewe hiki, tungekuwa tunakwenda hivyo nchi hii ingeendelea hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kuna watu wanapewa ambulance hapa, wengine hata haijulikani tunapewa lini. Yaani unakuta kila siku wewe ni mtu wa mwisho tu. Jamani mnataka tuseme nini humu ndani, sisi wengine sio Wabunge? Naomba, nimelia Barabara ya kutoka Mbalizi kwenda Mkwajuni kilometa 90 tupate lami, hakuna, lakini ukija kwa Waziri wa Barabara hapa unakuta barabara inakwenda maeneo fulani. Wanazo barabara, lakini wana hospitali, wana majengo ya Wilaya, sisi wengine mtatupa lini vitu vyetu? Jamani, wote ni Watanzania tugawane keki hiyo, nalalamika kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Wizara hii hupati chochote, ukienda huku hupati chochote. Juzi nimelia habari za umeme hapa; nashukuru sana Mheshimiwa Dkt. Kalemani hapa amenitafutia watu wa REA nimekaa nao tumepanga vitu. Yaani mpaka useme ndio upate, usipolalamika hupati, kwa nini? Mnataka tuje tuanze kulia machozi humu ndani ya Bunge? Jamani, tunataka na sisi tupate keki ya Taifa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka juzi hapa, sijui ni mwaka gani, kuna Mbunge mmoja hapa alisema Serikali inapendelea, tena alisema wazi, nadhani alikuwa ni Mheshimiwa Zitto, na mimi nataka kusema Serikali inapendelea, kwa nini wengine hatupati wengine mnapata? Mikoa ya Rukwa, Katavi, Songwe na Kigoma, hatuna chochote, fedha zote zinakwenda mikoa mingine, kwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Dkt. Mpango, weka pale Hazina tume ndogo itakayokuwa inaangalia kwamba hiki kama kimekwenda mahali fulani basi trip nyingine wapate na wengine hivi, tugawane jamani, wote ni Wabunge humu ndani na wote ni wananchi, kila siku tunalia mambo hayo hayo, eeh, jamani. Tafadhali, ninaomba kwenye bajeti hii mnipe Hospitali ya Wilaya pale Songwe, ni mbali sana kutoka pale Songwe tunakwenda kuhudumiwa na Mkoa wa Mbeya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalia kila kitu, mimi nikisimama hapa kila siku ni malalamiko tu, hakuna siku ya kuja kusema jamani na mimi angalau nimepata hiki. Nataka na mimi niwe ni Mbunge ambaye nikisimama niseme Serikali nashukuru mmenipa hiki, sasa kila siku mimi ni kulalamika tu, hamnionei huruma? Kila siku tunalalamika tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafadhali naomba sana, Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, nataka kwenye bajeti hii mnipe maji. Mwaka kesho kwenye bajeti ya Serikali hapa mtanitambua kama hamjanipa hivi vitu. Tupatieni basi, ni hilo tu kwa leo. Ahsante sana.