Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Hassan Elias Masala

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nachingwea

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kukushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia bajeti hii. Naomba niungane na wenzangu waliopita, kumpongeza Mheshimiwa Waziri, lakini pia naomba nimpongeze Mheshimiwa Rais wetu kwa kazi nzuri ambayo anaendelea kuwafanyia Watanzania, ya kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba nijielekeze katika maeneo makubwa manne. Eneo la kwanza ambalo nilitaka nichangie ni eneo la kilimo. Kwa niaba ya wananchi ambao nawawakilisha naomba nifikishe salamu zao za pongezi kwa kilio cha muda mrefu cha kuwaondolea adha kubwa ya tozo katika zao kubwa ambalo linatuletea uchumi mkubwa katika maeneo yetu, zao la korosho. Kwa muda mrefu tumekuwa tunalalamikia tozo nyingi ambazo zilikuwa zinapunguza bei ya korosho, lakini kwa sasa kupitia Rais wetu wakulima wa zao la korosho wamenufaika kwa kiasi kikubwa. Ndani ya Wilaya ya Nachingwea, Liwale na Ruangwa kwa mwaka huu peke yake si chini ya shilingi bilioni 46 zimeingia katika mzunguko wa fedha za wakulima. Hii ni kazi kubwa ambayo imefanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na hilo, naomba nizungumzie nakupongeza pia suala zima la kutoa pembejeo bure, sulfur pamoja na madawa mengine ili kuweza kukuza zao hili la korosho. Changamoto kubwa ambayo nilitaka nishauri kupitia kwa Waziri wa Kilimo na Wizara kwa ujumla ni suala zima la kuangalia pembejeo hizi zinapatikana kwa wakati gani. Mpaka sasa hivi ninapozungumza tayari wakulima wanahitaji kuona pembejeo zimeshawafikia, lakini bado kuna baadhi ya maeneo pembejeo kwa maana ya sulfur mikorosho imeshaanza kutoa maua bado sulfur haijafika. Kwa hiyo, niombe haraka iwezekenavyo Wizara ipeleke sulfur katika maeneo ya mikoa ya Lindi, Mtwara, ili wakulima waweze kupulizia mikorosho yao tuweze kuuwahi msimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hilo, pamoja na nia nzuri ya Serikali ya kutoa sulfur bure bado kuna changamoto ya uchache wa sulfur hii ambayo inaenda kutolewa kwa wakulima. Mpaka sasa hivi nazungumza kwa Wilaya ya Nachingwea peke yake ina mgao wa tani 1300, kwa idadi ya wakulima na uzalishaji wa Wilaya ya Nachingwea peke yake idadi hii ya pembejeo ambayo tunaenda kupata ni ndogo na haiwezi kukidhi mahitaji. Kwa hiyo naomba Wizara naomba Serikali iongeze idadi ya mgao ili wakulima wengi waweze kupata sulfur na pembejeo za kutosha ili waweze kuhudumia mikorosho yao tuweze kuingia katika Kilimo kwa ufanisi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu ambalo nilitaka nizungumze ni suala zima la maboresho ambayo tungependa yafanyike pia ili kumnufaisha mkulima. Tunahitaji tuone utekelezaji wa kuanza kazi kwa bodi ya mazao mchanganyiko. Ukiondoa korosho ambayo inatuletea uchumi mkubwa, bado tuna mazao ya mbaazi, tuna mazao ya choroko, lakini pia tuna mazao ya ufuta ambayo muda si mrefu tunaenda kuingia kwenye msimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda mrefu tumepigia kelele kuona bodi hii inafanya kazi lakini mpaka sasa hivi bado Serikali imekuwa na kigugumizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Wizara, naomba nishauri Serikali ione umuhimu wa Bodi ya Mazo mchanganyiko iweze kufanya kazi kuanzia mwaka huu ili iweze kusimamia bei ya wakulima wetu katika haya mazao mengine ambayo wakulima wetu wameitikia wito wa kulima kwa nguvu na kwa kiasi kikubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo ningependa nizungumzie, unapozungumza uchumi na unapozungumza kuiunganisha Tanzania, unapozungumza suala la viwanda, huwezi kusahau suala zima la umeme. Bado mikoa yetu ya Lindi na Mtwara ina matatizo makubwa ya umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka leo tunazungumza, Serikali imeonyesha nia ya kujenga kituo pale Mnazi Mmoja. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha atuambie wametenga kiasi gani na wana nia gani ya kwenda kuhakikisha mitambo ile inaanza kufanya kazi ili wananchi wa kule waweze kupata umeme wa uhakika, ambao wataweza kuzalisha kwa ufanisi na kutosimamisha shughuli za maendeleo ambazo mpaka sasa imekuwa ni kitendawili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu ambalo nilitaka nizungumzie ni suala zima la barabara. Nimepiga kelele toka mwaka jana, nimepiga kelele mwaka huu. Kwenye bajeti ya mwaka huu ya Wizara tumeahidiwa kutengewa bilioni tatu; lakini bado ningependa kuona Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha, kwa uchumi ambao mikoa hii inazalisha, tungependa kuona barabara ya Masasi - Nachingwea na Nganga, lakini pia sasa hivi tunazungumzia barabara ya Ruangwa, fedha hii ambayo imeahidiwa inaenda kupatikana kwenye fungu gani na lini fedha hii inaenda kutoka ili tuanze ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, ambayo nayo imekuwa ni kikwazo kikubwa cha maendeleo katika ukanda huu kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumza hayo naomba…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)