Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Ally Abdulla Ally Saleh

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Malindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nitaanza na makinikia ambayo kidogo yameelekea kama kutugawa huku ndani kiasi ambacho juzi Mheshimiwa Abdallah Ulega alisema kwamba sisi ni UNITA na kwa kwa sababu hakukatazwa na hakuna kiongozi yeyote aliyemwambia afute kauli hiyo nataka niulize maswali matatu/manne.

Nani UNITA zaidi au upande ule ambao wanafuta matokeo ya uchaguzi na wanaweka watu wasio halali? Nani UNITA zaidi wanaofuga mazombi ambao kila siku wanapiga raia? Nani UNITA zaidi ambao wanatunga sheria za kuzuia watu wasitoe maoni yao na wanafungia magazeti? Nani UNITA zaidi ambao wanaweka Masheikh kwa miaka minne hata bila kesi kufanyika? Hilo nimemaliza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili nilitaka kusema kwamba hii makinikia imekuja ili kutupunguzia uwezo wa kuchangia katika bajeti yetu hapa. Mimi sioni kama ni bahati mbaya kitu ambacho kiko nje ya Bunge kimeletwa hapa ndani kimetupunguzia uwezo wetu wa kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana nilihudhuria kwenye kongamano moja ambalo linasema hapa Tanzania watoto 30.2 wenye uwezo wa kwenda shule hawaendi shule, hatujadili hapa tunaona kama kitu kidogo tu. Jana tumesikia kwamba, asilimia 34 ya watoto wa Kitanzania wana utapiamlo, tumeacha kulizungumzia hapa! Lakini pia, tumeacha kuzungumzia kwamba bajeti yenyewe imekuja na mashimo mengi ambayo yanapaswa yajazwe, pia bajeti yenyewe imekuja ikiwa imetekelezwa chini ya asilimia ndogo ya ile ya mwaka jana, imetutoa katika mood na tumeanza kuzungumza mambo mengine ambayo hayakuwa na umuhimu kuyazungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mambo ya bajeti nina mambo mawili matatu, kwanza ni Deni la Taifa. Mimi siyo katika wanaoamini kwamba deni letu linanyumburika, sijui linafanya kitu gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana nilisema na kusema kweli rate ya mwaka jana imeongezeka mwaka huu kwa hivyo, bado nina maoni kwamba Deni la Taifa linapaswa likabiliwe inavyopaswa na sio kuona kwamba linahimilika kwa hivyo tuliachie liendelee. Mwaka jana nilisema na mwaka huu narudia, ziko nchi zilikuwa zikisema hivyohivyo kwamba deni linahimilika lakini zimesambaratika, Greece, Venezuela, Peru na wengine, hilo la pili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, mwaka jana nilisema na mwaka huu nasema tena. Bado sioni faida ya Serikali ya Muungano kwa Zanzibar katika mambo makubwa. Nilisema mwaka jana kwamba katika miradi kielelezo basi angalao mmoja uwepo Zanzibar. Hii nasema kwa sababu Zanzibar tuko watu 1,200,000 ukipeleka mradi ambao unaajiri watu elfu tano, elfu sita, maana yake umeajiri work force yote ya Zanzibar, lakini bado Serikali ya Muungano inaona kwamba bado haitaki kufanya wajibu, mimi nahisi ni wajibu, inaona haina wajibu kwa Zanzibar. Lakini Zanzibar itafanyaje mambo makubwa wakati uchumi wake unazuilika na upande huu? Kodi zake haziwezi kukusanywa kama inavyotakiwa? Lakini itakavyokuwa vyovyote vile uchumi wa Zanzibar ni uchumi mdogo hauwezi kufananishwa na uchumi wa Bara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ninachotaka kusema ni kile ambcho Mheshimiwa Ulega alisema siku mbili tatu nyuma, nampa credit yake. Alisema kwamba Rais Magufuli anafaa sasa aelekeze kwenye ku-invest kwenye mambo ya bahari, lakini hata leo Mheshimiwa Adadi alisema jambo hilo. Sisi tumezungukwa na nchi ambazo ni land locked, Rwanda, Zambia, sijui wapi, wote wale, tungekuwa tumejijenga kwenye bahari tuna meli za kutosha, tuna uwezo, tungelamba cargo zote za nchi hizo, sio tu wakati wa kuodoa, lakini hata wakati wa kuingiza, hilo moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jingine ni suala la aqua culture. Wiki tatu nyuma nilisema katika Wizara ya Maliasili kwamba bado hatujatumia blue economy na kitu kimoja ambacho kina utajiri mkubwa sana, narudia tena ni bahari, kuanzia Bahari Kuu kule mpaka pembezoni humu. Kwa kuwa watu wengi wameshazungumzia Bahari Kuu, mimi nazungumzia hapa pembezoni; nilisema utajiri wa hapa pembezoni uko katika fukwe pale, kwa maana ya kufuga vitu kama kamba, kufuga vitu kama kaa, ambazo ni billions of dollars. Nchi kama Vietnam ambayo tuna urafiki nayo, nchi kama China, hawashibi kwa mazao ya bahari. Chochote utakachozalisha wewe wanaweza kukichukua kama vile ambavyo India ukizalisha chochote kile cha beans hizi, chochote kile watakichukua. Kwa hiyo, nasema tena Mheshimiwa Waziri, hilo tulifanye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia lilizungumzwa leo suala la afya. Tungewekeza katika afya kiasi cha kutosha tukawa na hopitali ambazo ni kubwa ni za maana, watu wasingekuwa wanakwenda India. Tuna majirani zetu hapa chungu nzima wangekuwa hii ndio India yao wanakuja kwetu. Serikali najua hii haitafanya kazi muda huu, itandike misingi yakuwezesha hilo lifanyike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kwenye suala la elimu. Suala la elimu wenzetu mfano Northern Cyprus moja katika kipato chao kikubwa ni kwenye elimu au nchi nyingine. Tumekuwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kina brand moja nzuri sana kupita kiasi duniani, lakini kimeshindwa kukua nje ya Tanzania kimebaki hapa hapa, wakati wenzetu kama Marekani utakuta American University iko Misri, iko Lebanon, iko wapi. Na sisi kama tungejipanga vizuri tungeweza kutumia eneo letu hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Mheshimiwa Mama Rwakatare jana alisema hapa au juzi, kwamba kuna kodi nyingi kwenye elimu kiasi ambacho hatuvutii watu kutoka nje. Nchi kama Cyprus watu kutoka nje ni mataifa 144 wanakwenda kusoma Cyprus, wana wanafunzi zaidi ya laki mbili kutoka nje ambao wanasoma katika nchi yao. Tukifanya hii kama ni sehemu ya kipato, tukatengeneza vizuri, tukapunguza kodi, tukai-streamline, naamini inaweza kutusaidia sana kwenye mapato ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jingine ambalo linaweza kutusaidia ni kwenye diaspora. Mpaka sasa diaspora tunasema in general terms kwamba waje wawekeze. Je, tumeonesha maeneo gani wanaweza kuja kuwekeza? Tumetangaza wao kama diaspora watapata vivutio gani kuja kuwekeza? Kwa hiyo, ina maana kwamba kama tukijipanga vizuri tunaweza kutengeneza hiyo ikatusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine tunajenga reli. Reli kutoka inakotoka mpaka inakokwenda hapa katikati kungeweza kufanywa vitu vya kuweza kusaidia, ili local content iwe na maana, lakini kama tutajenga reli tu ili itoke mwanzo kama ilivyo sasa inatoka Dar es Salaam inakwenda mwisho wa reli Kigoma, hapa katikati hapana chochote kuwasaidia watu wafanye local content itakuwa haina maana yoyote. Kwa hiyo, nashauri kama tunajenga reli hii kubwa, tusilenge tu kwamba tutatoa makaa kutoka kule mpaka kuja huku, lakini pia katikati hapa kuwe na uwezekano wa kuwawezesha watu wafaidi kwa local content. Hali kadhalika katika hili bomba la mafuta linalotoka Uganda kuja Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, alizungumza Mheshimiwa Selemani Zedi hapa katikati watu wapate ajira. Sio ajira tu kwa maana ya vibarua, lakini what after that? Nashauri kwamba kama tunataka tuwatengenezee watu fursa nzuri ya maisha, basi tuwatengenezee local content ili waweze kusaidia, lakini kama tukizubaa hapa chakula cha wafanyakazi wa reli watakaojenga, Waturuki kitatoka Uturuki badala ya kuwawezesha wananchi wetu hapa wakasaidia. Chakula cha wafanyakazi ambao wanajenga hilo bomba kitatoka kwingine, tujipange katika haya ili tuweze kusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.