Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Daniel Nicodemus Nsanzugwako

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Spika, nashukuru nami kwa kunipa nafasi hii. Kwanza naanza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango kwa hotuba yake nzuri aliyoitoa. Wale mnaokumbuka, kwa miaka 10, 15 iliyopita, hii ni hotuba ya pili kwa ubora. Hotuba ya kwanza ni ile ya wakati ule wa Mzee Mkapa aliyotoa Mzee Mramba kufuta kodi, Nuisance Taxes kama mnakumbuka mliokuwepo.

Mheshimiwa Spika, hotuba hii kwa ubora wake imejikita kuondoa matatizo na mizigo kwa wakulima wetu na watu wa kipato cha chini. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mpango hongera sana, kama nilivyokwambia siku ile, ulikuwa kwenye form vizuri na ulifanya kazi nzuri, hongera, tena hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine bila kusahau, unakumbuka wewe na mimi tulikwenda North Mara kipindi kile kwenye vurugu ya Mto Tigite wakati kuna zile tuhuma kwamba yale maji ya Mto Tigite yameua watu wengi sana kule. Naomba kwa namna ya pekee Waheshimiwa Wabunge wote kazi ambayo ameifanya jana Mheshimiwa Mzee Magufuli ni kazi ya peke yake kabisa. Unaibiwa, sasa ametokea jasiri kusema jamani tunaibiwa, tusiibiwe, huyo amekuwa mbaya? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema, nawe tumekusikia jana uliona ile nguvu iliyokuwepo pale, mmefanya kazi nzuri sana, hongereni. Tunaibiwa na kama alivyosema Mbunge mmoja, sasa basi, tusiibiwe tena. Maana mtu kama anakuibia, kwanza anakudharau. Nasi tunasema hao Wazungu waliokuwa wanatuibia, sasa basi tumeona. Tumsaidie Mheshimiwa Rais, rasilimali za Taifa tuzilinde. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wewe utakuwa shahidi yangu, wala siyo madini tu, wewe unajua ni maeneo chungu nzima. Ile spirit kwamba sasa tupitie maeneo yote yenye fedha, yanayozalisha fedha katika nchi yetu, tuyapitie yote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilibahatika mwaka 2009, niliongoza Kamati Ndogo kwenda Mwadui, tukiwa na Mheshimiwa Mzee Shellukindo kama mnakumbuka. Tulipofika pale Mwadui, Williamson Diamond, tuliyoyakuta pale ni mambo ya aibu. Wale De Beers wamekopea shares zetu kule London bila sisi wenyewe kujua. Tulikuwa na Mbunge wakati ule Bwana Mpendazoe, alikuwa ni Board Member kwenye ile group ya Williamson Diamond. Wanasema walikwenda London pale wakakuta hisa zilishauzwa na Serikali haijui.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nami nakubaliana nawe kuunda Tume Ndogo kwenda Mwadui pale kuona. Ni uchafu uliopitiliza kwamba shares zetu za Serikali ya Tanzania ndizo De Beers alikwenda kukopea na kuanzisha migodi, Niger na Namibia. Mambo ya aibu kabisa! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hii vita ni kubwa, nina hakika Mheshimiwa Rais peke yake haiwezi. Ni lazima tumuunge mkono kama Bunge, tusimame pamoja kulinda rasilimali za Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nitakuwa na machache tu. La kwanza, nianze na miradi ya kipaumbele. Mheshimiwa Waziri tangu bajeti iliyopita na bajeti hii tumezungumzia habari ya miradi ya vipaumbele. Mimi nataka nijikite kwenye miradi hii ya kipaumbele; nianze na mradi wa kujenga reli ya kati. Tumeanza vizuri, lakini bado tunawakumbusha na hasa wenzetu wa Hazina ambao ndio mnatoa fedha na kumshauri Mheshimiwa Rais, endeleeni kumkumbusha kwamba hii reli ya kati itakuwa na faida kubwa zaidi kama itaanza kwenda Kigoma kabla ya kwenda matawi mengine; na sababu ziko wazi; ni za kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kule Kigoma ndiyo kuna mzigo ambao utaifanya reli hiyo iwe na faida kiuchumi. Mzigo uko Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo ya Mashariki. Hilo tumelisema sana. Sasa kwa sababu kuna mkakati huo, nashauri, wakati anatafutwa Mkandarasi wa kujenga tawi la Tabora kwenda Mwanza, wakati huo huo atafutwe Mkandarasi kujenga tawi la kwenda Kigoma ili tuwahi ule mzigo wa DRC ambao utaifanya hii reli ya kati iwe na maana kiuchumi. Mzigo mkubwa uko DRC na kila mmoja anafahamu. Siyo DRC tu, hata hii Msongati ya Burundi ambapo kuna nickel nyingi, maana yake ni karibu zaidi na Bandari ya Kigoma, ni karibu kabisa na Station ya Uvinza ambayo iko katika Mkoa wa Kigoma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ambalo napenda nilisemee, Mheshimiwa Waziri alikwenda Korea ya Kusini wakasaini mradi unaoitwa North West Grid ambao unatoka Mbeya – Sumbawanga – Katavi – Kigoma – Nyakanazi.

Mheshimiwa Spika, sasa napenda wakati Mheshimiwa Waziri anajumuisha na kwenye kitabu chake ameuzungumza mradi huu, napenda kujua vizuri, huo mradi unaanza lini? Unaanzia wapi? Kwa sababu kutoka Tunduma pale mpaka Nyakanazi ni kilometa zaidi ya 2,000. Ni dhahiri kabisa kwamba huo mradi utakuwa na maana kama utakuwa hauna Wakandarasi wengi, mmoja atokee Tunduma aje Sumbawanga, aje Katavi na pengine mwingine atoke Nyakanazi kuja Kigoma. Nina hakika kama ni Mkandarasi mmoja itachukua miaka mingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunapozungumzia habari ya uchumi wa viwanda, maana yake ni pamoja na kuwa na umeme wa viwandani. Maana huu umeme wa REA ni mzuri, lakini ni dhahiri kwamba ni umeme ambao hauimarishi viwanda kwa sababu siyo umeme mwingi sana. Kwa hiyo, napenda sana kujua hilo kwa sababu yeye mwenyewe alisaini mkataba ule pale Korea Kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo napenda nilisisitize kwenye Mpango wa Kipaumbele ni pamoja na barabara. Kwanza hongera kwa barabara hii ya Tabora. Sisi tukisikia barabara ya kwenda Tabora, maana yake hiyo barabara inakwenda Kigoma.

Mheshimiwa Spika, tumeshukuru sana hii barabara ya Chaya – Nyahua, imepata fedha, tumeshukuru sana, maana yake inakwenda mpaka Kigoma. Tunashukuru pia kwamba juhudi ziko kubwa na tumeshapata fedha kujenga kipande cha Daraja la Malagarasi kwenda Uvinza kwa fedha za Kuwait Fund. Sisi kwetu ni faraja kubwa sana. Napenda hiyo juhudi iunganishwe na ujenzi wa barabara ya kimkakati ya kutoka Kigoma kwenda Nyakanazi. Barabara hiyo imetengewa fedha, lakini fedha kidogo sana, shilingi bilioni
19. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikurejeshe, Sera ya Ujenzi wa Barabara za nchi hii, tumeshakubaliana huko nyuma, Sera ya Ujenzi wa Barabara na Sera ya Chama cha Mapinduzi kwamba tutaunganisha mikoa na mikoa. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, waende kwenye misingi ya Sera ile kwamba mikoa ambayo haijaunganishwa na mikoa iwe ndiyo kipaumbele Waheshimiwa Wabunge. Mkoa wa Kigoma haujaunganishwa na Katavi, haujaunganishwa na Geita, haujaunganishwa na Kagera na pia haujaunganishwa na Shinyanga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lazima twende kwenye misingi hiyo. Hizi barabara nyingine za Wilaya kwa Wilaya, Tarafa kwa Tarafa, Kijiji kwa Kijiji zisubiri kwanza. Kwa sababu nchi hii lazima ufanye equalization, lazima Keki ya Taifa tunufaike nayo wote. Kama tunasema tunajenga kuunganisha mikoa kwa mikoa basi, iwe ndiyo kipaumbele na iwe ndiyo mtazamo wa Hazina na uwe ndiyo mtazamo wa Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho nizungumze habari ya vyeti fake, Mheshimiwa Waziri wa Utumishi yuko hapa. Nashauri tu, kazi nzuri sana imefanyika kubaini vyeti fake, lakini waende sambamba na kufanya kitu kinaitwa performance audit. Kuwa na cheti halali hakufanyi mtu awe bora. Ndiyo ile hadithi kwamba afadhali kuwa na cheti fake kuliko kuwa na akili fake. Fanyeni performance audit ya Watumishi wa Umma hawa tuweze kujua kwamba hawa watu kweli wana manufaa na wana tija katika uendeshaji wa shughuli zetu za Serikali.

Mheshimiwa Spika, la mwisho kabisa, pia nipendekeze jambo moja tu kuomba Wizara ya Kilimo, Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Mazingira kwa Mheshimiwa Makamba pale na Wizara ya Maji, waje na mkakati comprehensive wa namna ya kulinda mito yetu katika nchi hii. Mito inakauka, Ruaha iko threaten, Malagarasi iko threaten. Naomba sana, mje na kitu comprehensive kwa ajili ya kulinda mito mikubwa hii ili tuweze kuendelea kuwa na rasilimali za maji.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja hii na nasema ahsante sana kwa kunipa nafasi hii.