Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru sana kuniruhusu nichangie hoja hii iliyoko Mezani kuhusu Bajeti na hasa mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka huu wa fedha 2017/2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijikite kwenye madini. Madini popote duniani ndiyo inayotoa tathmini ya utajiri wa nchi. Kwa hiyo, kabla ya mafuta, madini yalikuwa ndiyo kipimo cha utajiri wa nchi. Kwa hiyo, matapeli na waaminifu wamejikita kwenye madini. Kwa hiyo, Serikali yetu ijue kwamba kwenye migodi yetu hapa kuna makundi ya aina mbili; wako watu waaminifu sana na wako wahalifu. Hawa wahalifu wanangojea fursa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uelewa wangu mdogo, biashara hii ya madini, hasa kwa wenye migodi, wana malengo yao na malengo yao ni kuwa matajiri. Utajiri huo wanaupata kwa aina mbili. Kwanza kwa kuuza madini yenyewe, lakini pia kufanya biashara na migodi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa makampuni haya, aidha yananunua mitambo kutoka kwenye kampuni tanzu au kampuni mama, kwa hiyo, matumizi ya mitambo ambayo kwa mfano mgodi ulianza kuchimba uwekezaji mkubwa wakapata na holiday ya kutolipa kodi, lakini wakanunua mitambo ya kuchimba labda mita 100; kwa kipindi chote hicho watapata hasara. Gharama ya mitambo na dhahabu wanayoitoa, hawalipi kodi. Baada ya mita 100 watawekeza tena kutoka mita 100 na kuendelea na hivyo hivyo hawatapata faida, watapata hasara. Kwa hiyo, kodi haiwezi kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mambo matatu ambayo ni muhimu sana ili nchi iweze kufaidika na madini, la sivyo itabaki na mashimo ya madini. Madini yote yataondoka. Mambo haya matatu, la kwanza, ni lazima Serikali iwe na hisa kwa niaba ya wananchi wake katika kila mgodi ambao unafanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwa kuwa na hisa, Serikali itakuwa na Wajumbe wake wa Bodi, lakini pia itakuwa na wafanyakazi wa Bodi, kwa hiyo, watajua kiasi gani madini yanachimbuliwa na kiasi gani yanauzwa nje. Kwa sisi kuwa nje, tunawaachia wale wote madini ya kwetu na wachimbe wapeleke nje, hatujui kiasi gani cha madini kinachimbuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala la pili, nalo ni ulinzi. Sasa hivi migodi yetu yote ina viwanja vya ndege na ndege zinatua pale na kuondoka na madini na haziji Dar es Sa- laam wala haziendi Mwanza wala Tabora, zinakwenda nje ya nchi. Matokeo yake tunabaki na mashimo makubwa ya madini kule, lakini hatuyaoni madini yale.

Katika taarifa ya Tume iliyotolewa leo na tunashukuru leo karibu Watanzania wote tuna msiba baada ya kujua kiasi gani tumeibiwa, hata furaha ya kuchangia inakuwa taabu kidogo. Madini yote yameenda nje, tumebakia na mashimo, lakini hatuna chochote tulicholipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya tatu ambayo ni mbaya zaidi ni hii ya kutofuata local content. Makampuni haya yote yanakuja kutoka nje, yanakuja na makampuni ya ulinzi, kazi ambayo ingefanywa na makampuni ya nchini hapa. Wanakuja na makampuni ya ulinzi kwa sababu hawataki Watanzania tujue ulinzi ule, kiasi gani mali inatoka? Kwa kufanya hivyo, miaka yote hii ambayo makampuni haya yamechimba yamekuwa na makampuni yao ya ulinzi na kwa hiyo, mali iliyotoka nje hatujui.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, ni manunuzi. Manunuzi imekuwa ndiyo unapofanya mizania ya kulipa kodi ili uonekane kama unapata faida, wanajaribu kupanga kiasi gani tumepata na kiasi gani tumetumia na miaka yote miradi mingi ya migodi imeonesha kwamba wamepata hasara badala ya faida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa kungojea sisi tupate mapato, kampuni zioneshe mapato, ndipo tudai kodi TRA waende, tumekuwa tunapata hasara badala ya kupata faida. Manunuzi haya kama sisi tungekuwa na nafuu ya kujua kiasi gani gari moja la kuchimbia mgodini linauzwa; na je, dumper lile shilingi ngapi? Tungeweza kujua kwamba tunadanganywa. Kwa vile tuko nje, hatuwezi kujua kiasi gani tunadanganywa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili la ulinzi wa mali migodini lipo kisheria. Makampuni haya na siyo haya tu, hata ya gesi na mafuta yamekataa katakata kutumia makampuni ya Tanzania na wWanazo sababu. Mimi nimekuwa Mwenyekiti wa Makampuni ya Ulinzi kwa miaka 15 na nimejitahidi sana kupata makampuni ya Tanzania yakalinde kwenye migodi, imeshindikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu kubwa ni kwamba wanasema Kampuni za Tanzania hazina viwango, hazina sheria, hazina kanuni na hazina miongozo. Ndiyo maana nilipokuja Bungeni humu jambo la kwanza nililolifanya ni kuleta Muswada Binafsi wa Sheria ya Sekta ya Ulinzi Binafsi ili hiyo Sheria iunde Mamlaka ya Kampuni za Ulinzi Binafsi, ambapo mamlaka hiyo ndiyo itakayodhibiti uwezo wa kampuni. Kampuni ambazo zinalinda migodini, nyingine hazina uwezo kuliko kampuni za Tanzania, lakini hatuna mizania ya kupimia kwa sababu hatuna Mamlaka ya Kampuni za Ulinzi Binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufanya hivyo, ni lazima tusonge mbele. Serikali iliniomba mimi rasmi kwamba, tunaomba Muswada wako huo tuulete sisi, lakini huu ni mwaka wa pili, na mimi naona kama tunachelewa. Yaliyosemwa leo katika taarifa ile ya Tume ya Pili ya Mheshimiwa Rais inasikitisha, ni kama vile mali imechukuliwa wenyewe wamelala au hawapo. Tungekuwa na macho yetu kule, tungekuwa na Sheria ya Ulinzi ya Binafsi, maana haiwezekani tukapeleka majeshi kwenda kulinda migodi ya watu binafsi au polisi kulinda migodi ya watu binafsi. Duniani kote migodi hii inalindwa na kampuni za Sekta ya Ulinzi Binafsi, lakini kwa kufuata sheria iliyopo na mamlaka iliyopo. Umefika muda sasa Serikali ilete Muswada hapa utakaosaidia sisi kuweza kudhibiti migodi yetu kwa macho ambayo tunayaamini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nirudi Jimboni kwangu. Tunayo matatizo makuwa sana Jimboni kwangu, hakuna maji. Tunakubali kwamba kutakuwa na Mradi wa kutoka Ziwa Victoria, lakini nikisemea Mkoa mzima, huo mradi haufiki Urambo, haufiki Kaliua, haufiki maeneo yote ya Jimbo langu; na chini ya ardhi ya Jimbo langu kuna mwamba. Kwa hiyo, visima vingi vilivyochimbwa vimekufa, zimebakia sehemu chache zenye chemchem kama vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali yangu, nimegharamia kwenda kuchunguza wapi maji yapo? Pale maeneo machache ambayo tumepata maji, Serikali iniunge mkono ije ichimbe maji kwa faida ya wananchi wangu. Tuna taabu ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siwezi kusimama hapa kila siku nagombana na Waziri wa Maji, nagombana na kaka yangu Mheshimiwa Kamwelwe. Naomba nipate ahadi sasa kwamba watakuja kuchimba vile visima hata vitatu, vinne kwa faida ya Jimbo langu. Wananchi wangu wananishangaa sana, kama nimegharimia mamilioni kuwaleta watu wapime maji, maji yakapatikana, kuchimba imekuwa taabu! Mimi napata taabu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni upande wa mawasiliano. Wilaya yangu ni mpya, haina barabara za ndani. Ili uje Tabora Mjini lazima uende Nzega ukapite kule kwenye barabara ya lami ndiyo uje mjini. Imekuwa gharama kubwa; watu wanapanda baiskeli, halafu wanaacha baiskeli wapande magari kwenda mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hili suala la barabara za ndani liangaliwe sana katika bajeti. Ipo barabara moja tu ya Tabora - Mambali ambayo ilikuwa iwekewe lami kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, sasa imewekewa iwe TANROADS, lakini barabara zote ndani hakuna. Tunatembea kwa miguu kama mwaka BC huko!

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali yangu inisikie na haya ambayo nimeyasema kuhusu madini, yachukuliwe kwamba ni mambo muhimu sana. Mambo matatu; manunuzi, ulinzi, kwamba ije Sheria ya Sekta ya Ulinzi Binafsi, lakini pia mambo yanayohusu hisa za Watanzania ndani ya migodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyeki, naunga mkono hoja. Ahsante sana.