Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sumve
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa nafasi hii. Nianze kwa kuiunga mkono bajeti ya Serikali, lakini pia niunge mkono taarifa ya Kamati ya Bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikiliza sana mwasilishaji wa upande wa pili, anasema bajeti ni mbaya sana haijawahi kutokea, lakini humu mimi ni wa muda mrefu kidogo bajeti hii ni bajeti ya karne haijawahi kutokea, bajeti ni nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashauri tu wenzangu, tunaweza tukawa wavivu wa kusoma, ni vizuri twende tusome ukurasa kwa ukurasa mtari kwa mstari kwa mstari. Tusirukie kusema kwamba bajeti hii ni mbaya, siyo mbaya hata kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna msemo wa kiswahili unasema ukiwaona adui zako wanachukia jambo lako endelea nalo, lakini ukimwona analifurahia liache haraka iwezekanavyo. Kwa hiyo, hii ni jambo jema sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na timu yako. Bajeti hii haijawahi kutokea, ni bajeti nzuri nzuri nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini waswahili wanasema kama una shughuli mahali, kuna harusi au kuna jambo fulani unaalika akina mama kwenda kuchambua mchele. Katika kuchambua mchele unaondoa zile chuya na michanga midogo midogo unabakiza mchele. Sasa wenzangu wanachagua mpaka na mchele badala ya kuchagua mchanga na chuya. Ni vizuri tukajitahidi kwenye bajeti hii tukachagua yale mabaya ambayo ndiyo yanatakiwa yaboreshwe lakini ninyi mnachukua yote kwa pamoja. Tujifunze hii ni bajeti ya Serikali yetu na ninyi mmekuja na mbadala yetu lakini hizo figure mlizotaja hazina uhalisia hata kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri nikuombe labda safari nyingine vitabu hivi tuwe tunavipata mapema kidogo kwa sasa hatuwezi kulinganisha kwa sababu imesomwa pale lakini hatuwezi kuona popote pale. Kwa hiyo, niombe sana bajeti hii Waziri wa Mipango sisi kama CCM ni bajeti yetu, lazima tuiunge mkono kwa sababu ina mambo mengi sana kuhusu wananchi wetu na hata wananchi wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanakimbilia kusema unajua hii tozo ya shilingi 40 kwenye magari, nilikuwa naongea na Mheshimiwa Shabiby hapa kuna mama mmoja ametoka kumtaja Mheshimiwa Shabiby, anasema katika ongezeko hili la shilingi 40 kwa lita moja, yeye ndiyo mwenye mabasi, hakuna hata senti tano itakayoongezeka. Sasa wewe humiliki hata bajaj au baiskeli unasema itaongezeka, itaongezeka wapi? Mwenye mabasi yake anasema hakuna senti tano itakayoongezeka. Kwa utaratibu wa Chama cha Mapinduzi, bajeti iliyopikwa vizuri ongezeko la shilingi 40 kwa lita moja ingekuwa ni vizuri zaidi tungeshauri badala ya kulalamika kama ambavyo sasa mimi nashauri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu liko suala la kuwatua ndoo akina mama kuhusu suala la maji, nishauri na nikuombe kwenye tozo tuna shilingi 50 tuchukue hii shilingi 40 tuiongeze kwenye shilingi 50 ili tupate shilingi 90 ziende zikahudumie maji vijijini. Hii shilingi 50 tayari ipo na sababu kuna ongezeko hili la Sh.40 kwa lita moja, shilingi 50 na shilingi 40 unapata shilingi 90, tuziweke pamoja hizi ziende zikahudumie maji vijijini na hiyo ndiyo itakuwa suluhisho la kuwatua ndoo akina mama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye maeneo mengi, nakumbuka asubuhi katika swali namba 368, 369, 370, haya maswali yalikuwa yanahusu maji, kila Mbunge alisimama mpaka ukawa unatuhesabu lakini ukashindwa kutuchukua wote kwa sababu wengi tulikuwa tunataka kuuliza kuhusu swali la maji. Kwa hiyo, niombe sana Waziri wa Fedha, Waziri wa Maji, Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti mtakapokwenda kule kwenye Finance Bill tafadhalini sana sana muangalie suala hili kwa sababu bila maji tutakuwa hatujawasaidia akina mama. Nikushauri sana sana na naomba nirudie hii, kwetu sisi kama wana CCM na hili nalisema wazi kwa sababu maji vijijini kwa akina mama ndiyo kete yetu ya CCM lazima tuibebe. Hamsini, arobaini, tisini naomba tuziunganishe tuzipeleke kwenye maji ili kusudi tupate maji kwa ajili vijiji vyetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyo vijiji vingi kule kwangu vinahitaji maji na suluhisho kubwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha haipendezi sana tunalo Ziwa Tanganyika, Nyasa, Victoria lakini ukienda Kigoma na wilaya zake zingine hazina maji lakini maji yako Ziwa Tanganyika, ni wakati sasa tuamue. Vivyo hivyo kwa Ziwa Nyasa, Victoria lazima tuweke nguvu. Vilevile tunayo mito mingi imetuzunguka, naomba tuamue sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini Serikali ya Chama cha Mapunduzi chini ya Jemedari Mkuu, John Pombe Magufuli ambaye leo amewaonesha Watanzania, wapo watu walikuwa wanadhani kwamba anatania, sasa leo wamesikia na wameona kwa macho yao kwamba watalishughulikia suala hili. Sisi kama Watanzania, Waheshimiwa Wabunge hapa nafikiri kitu ambacho tungefanya ni kuomba Serikali kama navyoiomba sasa kama kuna mikataba ambayo haitunufaishi sisi tuilete hapa haraka iwezekanavyo ili tuirekebishe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kwa mapato yale kwa kiasi kile kilichotajwa na kama sikosei Waziri wa Fedha sijui ndiyo yule pale Dkt. Mpango nafikiri ulikuwepo umesikia wale wataalam wanasheria wamesema kwamba hapa tunapunjwa badala ya kumi tunachukua mbili. Kama mikataba hii ina matatizo, mimi nashauri tena Waheshimiwa Wabunge wa itikadi zote na vyama vyote tumuunge mkono Mheshimiwa Rais kwa sababu pesa zile zikipatikana, matrilioni yale yanayotajwa ambayo yanaweza kusaidia bajeti tano mara moja mbali ya hizi, miundombinu ya barabara, maji, reli, vitu vyote nafikiri vitakamilika kwa sababu tunaweza hata kukopesha nje. Niombe sana Waheshimiwa Wabunge…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.