Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na mimi leo kupata nafasi jioni hii ili kuweza kuchangia katika hotuba ya bajeti. Mengi yamesemwa na naomba niishukuru Serikali, nina kila sababu ya kuishukuru Serikali kwa sababu mawazo mengi ambayo yalitolewa na Kamati ya Bajeti na kutolewa na Bunge yamezingatiwa.
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilivyopata fursa ya kuongea ITV nilisema hivi, kwa nchi zetu zinazoendelea, bajeti kama hii iliyoandaliwa utategemea iandaliwe kipindi ambacho nchi inaenda kufanya uchaguzi mwaka unaofuata. Hata hivyo, kwa Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli uchaguzi wala hatutarajii kwamba upo mwakani, kwa hiyo, ni bajeti ambayo inaenda kuwakomboa Watanzania kwa nia ya dhati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maboresho mengi tumetoa na Serikali imezingatia, naomba nisitumie nguvu katika kuchangia kwa sababu naamini Serikali ni sikivu. Naomba niboreshe baadhi ya maeneo machache ambayo yapo kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango ili waweze kuyatilia mkazo na marekebisho yaweze kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo ambalo naomba nijikite kwa kuanzia ni kuhusiana na VAT katika huduma uwindaji. Asilimia 18 inatozwa pale ambapo muwindaji anaenda kulipia block (block fee) eti nayo anatozwa VAT. La kushangaza zaidi hata pale anapolazimika kusafirisha trophy kupeleka nje ambayo amekatia leseni na ameruhusiwa awinde, wakati kwa mujibu wa sheria VAT on export hakuna kitu kama hicho, lakini kwa mwindaji tunataka atozwe asilimia 18, naomba Serikali mkatizame. Kama hiyo haitoshi hata pale ambapo ametozwa penalty lakini katika penalty hiyo nayo tunaweka na 18% VAT, sheria hiyo haipo. Kwa hiyo, naomba Serikali kwa ujumla wakalitizame kuanzia mwanzo mpaka mwisho ili marekebisho yafanyike twende kwa mujibu wa sheria inavyotaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusiana na taasisi na mashirika ya umma. Ni takwa la kisheria kwamba wanatakiwa kuchangia asilimia 15 ya growth revenue kwenda Serikali Kuu. Kinachoshangaza, kwa mujibu wa Sheria ya Kodi kwa maana ya Income Tax, anapoandaa hesabu zake anatakiwa aoneshe kile kiasi ambacho alishatoa kupeleka Serikalini lakini jambo la ajabu ni kwamba akiandaa hesabu ikifika TRA wanasema hawatambui, kama vile Serikali haijapata hata senti tano, wanairudisha kama siuo allowable deduction, kwa hiyo, kunakuwa na double taxation. Naomba Serikali mkalitazame hili, halina tija kwa mashirika yetu, inaua mashirika yetu bila sababu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hii hoja ya shilingi 40 ya tozo ambayo Kamati na naamini na Wabunge wote hata upande wa pili wanalitamani kimya kimya kwa sababu inakwenda kupunguza kero kubwa ya maji na hasa maji vijijini. Kwenye Kamati yetu ya Bajeti tumependekeza kwamba asilimia 70 ya pesa hizi ambazo zinakwenda kupatikana zikatibu kero ya maji vijijini na asilimia 30 ndiyo iende kutibu kero ya maji mijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini hili halina mjadala, naamini hata upande wa pili wakiulizwa watapigia kura ya kuunga mkono suala hili. Kwa sababu hakuna hata mmoja, awe anatoka mjini, awe anatoka vijijini, tatizo la maji ni tatizo la kitaifa. Kwa hiyo, tukubaliane ndugu zangu kwamba ni vizuri katika hili tukaungana, hii tozo ambayo inapatikana ikatatue kero ya maji vijijini na mijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niiombe Serikali, wakati Mheshimiwa Waziri anawasilisha bajeti yake amesema kwamba anaondoa road license lakini katika ile sticker ya road license kuna kiasi fulani cha fire extinguisher aje atuambie, nayo imeondolewa? Maana kama haijaondolewa itakuwa ni kero, kwa sababu ninyi wenzangu wote mashahidi, hakuna hata siku moja ambapo eti hiyo fire extinguisher imeweza kusaidia, sanasana ni stickers tu zinatolewa inakuwa ulaji. Naomba nayo iondolewe, ni kero kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama hiyo haitoshi, kuna zile stickers za Wiki ya Nenda kwa Usalama. Lengo lilikuwa zuri kwamba tunataka magari ambayo yanatembea barabarani yawe ni yale magari ambayo ni road worthy, lakini sisi sote ni mashahidi, tumekuwa tukiuziwa stickers gari hazikaguliwi. Kwa hiyo, nayo ni vizuri iondoke, ni kero, haitusaidii chochote, inasaidia wachache ambao ni wajanja wajanja, ikiondoka hiyo itakuwa imetusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika wasilisho la Mheshimiwa Waziri anasema kwamba excise duty ya ngano inapungua kutoka asilimia 35 kwenda asilimia kumi. Naomba tuulizane Mheshimiwa Waziri, hali ya sasa ikoje, kwa sheria ilivyo leo hii asilimia 10 hiyo anatozwa yule ambaye anaagiza ngano anakuja kuisaga tukijua kwamba wananchi watanufaika. Sasa kwa kuondoa kwa hawa wengine brokers, huisaidii Serikali wala humsaidii mwananchi wa kawaida. Ni kama vile tunataka wawepo middlemen ambao watakuwa wanaagiza ngano halafu wanakuja wanawauzia wenye viwanda waende kusaga. Mheshimiwa Waziri, naomba ulitizame, ni bora hiyo ibaki vilevile iwe chanzo cha mapato ila wale ambao wanaagiza kwa ajili ya kuja kusaga tukijua kwamba bei ya mkate itakuwa imeshuka itatusaidia lakini hiki chanzo kiendelee kwa sababu kinasaidia katika kuongeza mapato kwa upande wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili linalosemwa kuhusu suala la property tax, ni vizuri tukakumbushana Waheshimiwa Wabunge, sisi sote tulikuwa tunalalamika kwamba chanzo kisichotokana na kodi makusanyo yake yamekuwa hafifu, tukakubaliana kwamba ni vizuri kama TRA wanakusanya hawakusanyi pesa hiyo iende Mfuko Mkuu, ni wajibu wa TRA ikikusanya pesa hizo zizirudie Halmashauri maana ndiyo wenye hayo majengo, ndiyo msingi wake upo hapo, lakini si kwamba eti Serikali Kuu ichukue kama ni chanzo chake, la hasha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tukubaliane tangu mwanzo kwamba pesa hiyo ikikusanywa inatakiwa irudi kwenye Halmashauri husika ili yale majukumu ambayo Halmashauri inatakiwa iyafanye yaendelee kufanywa na Halmashauri. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri hili upigie mstari kabisa isije ikaonekana kwamba sasa tunanyang’anya vyanzo upande wa Serikali za Mitaa kwenda Serikali Kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima la ushuru wa mazao, nimefarijika sana ilikuwa kutoka asilimia tano sasa inakwenda asilimia tatu. Naomba nisisitize, asilimia tatu hii iwe kwa mazao yote, isiwe kwamba eti kuna mazao ya biashara na mazao ya chakula maana itakuwa ni vigumu sana kuweza kujua ni wakati gani mahindi yanakuwa zao la biashara na wakati gani mahindi yanakuwa zao la chakula, hapo tutakuwa tunatengeneza mwanya wa rushwa bila sababu. Kwa hiyo, kimsingi ni vizuri hicho kiasi kikapungua lakini iwe sawa kwa ama mazao ya biashara au mazao ya chakula na tafsiri iko rahisi kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Waheshimiwa wengine wanasema kwamba tunaipunguzia Halmashauri uwezo wa kukusanya, lakini ukiipunguzia Halmashauri uwezo wa kukusanya hicho ambacho kingekusanywa na Halmashauri kikawa kwa mwananchi wa kawaida, mwananchi huyu wa kawaida maana yake disposable income inakuwa imeongezeka, atakwenda kufanya spending katika mambo mengine na kodi yetu tutaipata. Ni nani asiyependa wananchi wetu wakawa wana pesa mifukoni mwao? Kwa hiyo, ni wazo jema mimi naliunga mkono sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe ni shahidi kwamba hatukulala mpaka saa nane na naamini na mengine tutaendelea kushauriana na Serikali, yale ambayo hawakuyachukua wataendelea kuyachukua kwa sababu naamini Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla ni wasikivu na naamini na wenzetu wa upande wa pili hakuna sababu ya kuja na pages 200, tuje na pages chache…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.