Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Manyoni Magharibi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii na mimi nichangie Wizara hii ya Fedha na Mipango katika kufanya nchi yetu iende. Nitumie nafasi hii kuwapongeza Waisalam wenzangu wanaoendelea na mfungo huu wa mwezi Mtukufu mwezi wa Radhamani, nawaombea Ramadhani Mubarak. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara hii ya Fedha kwa juhudi na kazi nzuri ilizoonesha hasa katika suala zima la kusimamia kulipa deni letu la nje. Wizara ya Fedha imesimamia kwa ukamilifu kwa mwaka uliokwisha na naomba sasa waendelee kusimama imara kuhakikisha nchi hii inaaminika baadaye ili tuweze kufanya maendeleo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze pia Wizara ya Fedha kwa usimamizi wao madhubuti sana ambao ulikutana na changamoto mbalimbali katika kusimamia mashine hizi za elektroniki (EFDs) kwa wajasiriamali wahakikishe wanazitumia ili kurahisisha makusanyo ya kodi za Serikali. Ni ukweli usiopingika kwamba Wizara hii ina mafanikio kiasi kikubwa na niwapongeze sana. Nataka kushauri Serikali yangu na Wizara hii tujaribu kuweka sera ambayo itaeleweka juu ya watu wetu, Serikali tusiwe na sera za mlipuko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa ambalo nataka kulisemea na hata Mheshimiwa Waziri amelionyesha katika ukurasa wa 41 kwamba sasa tunatoa nafasi kubwa kwa sekta binafsi kusaidia katika uchumi na hasa kuweza katika maeneo mbalimbali. Tukikumbuka kule nyuma Serikali ilikuwa ikifanya biashara kupitia mashika yake ikiwemo RTC, NMC na hata mashirika kama GAPEX, badala ya mashirika haya kulipa kodi yalikuwa yanachukua ruzuku kutoka Serikalini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipoondoka kule nilitegemea kwamba sasa Serikali haitajiingiza tena katika biashara, kuna viashiria vidogo vidogo vinaoonesha kwamba Serikali inataka ijaribu kuingilia katika biashara. Niombe sana Mheshimiwa Waziri ang’ang’ane hapo alipoonesha ukurasa wa 41 kwamba sasa sekta binafsi itawekeza maeneo mbalimbali na ametolea mifano ambayo iko hai, gari za mwendo kasi pale Dar es Salaam lakini barabara ya Dar es Salaam Chalinze ambayo inategemea iwe ya kutoza toll kwa maana ya road toll.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejifunza kutoka nchi mbalimbali walioendelea waliachia sekta binafsi, Serikali kwa uwezo wake haiwezi kufanya kila kitu, lakini sekta binafsi inashindwa kuja katika nchi hii kwa sababu ya kutokuwa na uwazi katika sera za nchi. Hatuna sera, akija Waziri huyu ana tamko lake, akija huyu ana tamko lake. Tukiweka hilo itatusaida na wadau mbalimbali kutoka nchi mbalimbali miongoni mwetu Wabunge na hata wananchi na wafanyabiashara mbalimbali wanaweza kuleta watu wa kuwekeza katika maeneo mbalimbali kama tu tutakuwa na Sera ambayo itaeleweka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vitu vya kuimarisha ili sekta hii binafsi ambayo tunaitegemea isaidiane na Serikali katika kuboresha maendeleo ya nchi yetu ikiwemo miundombinu, maeneo mbalimbali ni lazima tuboreshe, Benki ya TIB. Mheshimiwa Waziri ameonesha kwa vipengele vifupi tu ukurasa wa 49 na ukurasa wa 90. Naomba sasa juhudi za makusudi benki hii ya TIB ndiyo mkombozi wa sekta binafsi, kwa sababu benki hii itahusisha mwekezaji yeyote anaweza kwenda pale na akapewa mkopo ambao ataulipa kwa kile alichowekeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, benki hii inasuasua, mtu akihitaji mkopo mkubwa Waziri mwenyewe ni shahidi na ameonesha katika kurasa hizi kwanza benki haijawa sawasawa. Kwa hiyo tumwombe sana Mheshimiwa Waziri asimame imara kuisaidia nchi yako. Tuna mategemeo mkubwa na yeye lakini safu yake na Mheshimiwa Naibu Waziri na Katibu Mkuu wa Wizara yake, tunaamini kwamba wataisaidia Serikali hii ya Awamu ya Tano kwenda na fikira ambazo Mheshimiwa Rais anadhani na anafikiri ni vizuri kwamba siku moja baada ya kipindi chake nchi hii itakuwa imesimama yenyewe kwa miguu yake, lakini inasimamaje kwa miguu yake?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka tuondokane na fikra za kwamba Serikali inaweza kufanya biashara, Serikali kazi yake ni kusaidia miundombinu, kurahisisha mambo yaende ili sasa sekta binafsi nayo ichukue nafasi. Mfano ni huo kama nilivyotolea pale Dar es Salaam. Tulivyojenga miundombinu ya barabara. Leo mtu kutoka Kimara mpaka posta haizidi dakika 40. Ni mfano kama huo na iko mifano mingi ambayo itawekezwa. Hata Mheshimiwa Mwijage anapokuja na viwanda vyake vile vya mwendo kasi kama Serikali tutaifanya benki hii ya TIB iweze kuwa na nguvu basi wale wajasiriamali tukiwemo Wabunge kama anavyosema viwanda vidogo tunaweza tukawekeza, kupitia benki hii tunaweza kwa mawazo yake Mheshimiwa Mwijage. Mheshimiwa Waziri wa Fedha akisaidiana kama Serikali na Mheshimiwa Mwijage naamini hili linawezekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze pia Wizara hii, mashirika wanayoyasimamia yakiwemo mashirika ya hifadhi ya jamii, yameonesha mfano nzuri sana katika kuwekeza. Nimwombe Mheshimiwa Waziri asimamie hilo, sekta binafsi na sekta ya umma lakini wanawekeza katika sekta binafsi naamini siku moja yatakuja kuwa mwarobani wa shida zetu na ajira za vijana wetu ambao wako na wanaosoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kidogo katika huduma ya mfuko wa huduma ndogo za fedha, ukurasa 202, Mheshimiwa Waziri ameonesha kwamba watakopesha wajasiriamali vikundi vidogo vidogo vile bilioni 20, sijui wamefikia wapi, sijui wanakwenda kweli, au ndiyo tunakwenda kisiasa. Niwaombe sana wale watu wetu wa SACCOS za vijijini wana dhamira njema na kama tutawawezesha tutaondokana na mpango huu wa kuitegemea Serikali ituletee viwanda vya kutengeneza chaki kule katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo cha Mipango ndiyo kitu ambacho naamini kama kitaweka mipango iliyo sawasawa, chuo hiki kinatengeneza wataalam ambao wanaamini wao wataenda kufanya kazi tu Serikalini. Ni vizuri tukabadilisha mfumo na mawazo ya watu wanaotokana na chuo hiki waweze kuangalia na sekta binafsi ili waweze kutoa utaalam wanaoupata. Nchi hii ili iweze kwenda mbele kama nilivyosema ni lazima sekta binafsi kwa asilimia kubwa nayo ihusishwe. Mifano kwa nchi zote ambazo zimeendelea, leo tunalitolea mfano Taifa la India, wamehusishwa sana wananchi pia watu ambao wako nje ya nchi ile ambao wana nguvu ya kiuchumi wameitwa, wamekuja kuwekeza maeneo mbalimbali na sisi tunayo fursa hii, lakini Chuo cha Mipango kikifanya kazi hii kwa weledi naamini hili linawezekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali yangu pia kwa jitihada zinazosimamiwa na Wizara hii hasa katika suala la kulipa wazabuni ambao walikuwa wanahudumia katika taasisi za Kiserikali kama Magereza na maeneo mengine, leo wameanza kulipa. Naomba sana Mheshimiwa Waziri waongeze juhudi kuhakikisha wale watu ambao walikuwa wanadai, wana madeni mbalimbali katika mabenki, wengine nyumba zao zimetaka kuuzwa na nyingine zimeuzwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili watu hao waondokane na hali hii, kwa sababu walikuwa wanaisaidia Serikali yetu, wakisaidia watu wetu, wakisaidia wafungwa wetu na pia Majeshi yetu, leo kwa kuwa wameonesha dalili ya kuwajali naomba tu waongeze nguvu ili watu hawa nao waweze kulipwa kwa wakati ili kesho na kesho kutwa mpango uende vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na nashukuru kwa nafasi hii ambayo umenipa.