Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Hon. Dr. Susan Alphonce Kolimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa uzima na afya njema, kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuchangia hoja iliyopo mbele yetu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchukua nafasi hii ya kipekee, kama wenzangu walionitangulia kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa uongozi wake madhubuti na makini unaoendelea kugusa si tu Watanzania, bali mfano wa kuigwa katika nchi za Bara la Afrika na Dunia kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kumpongeza sana na kipekee Mheshimiwa Balozi Dkt. Augustine Philip Mahiga, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kwa uongozi wake makini na kuhakikisha tunapata ufanisi mkubwa katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara anayoiongoza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa uongozi wake ndani ya Bunge hili. Aidha, napenda kuwapongeza sana Mheshimiwa Spika na Naibu Spika na kwa namna wanavyoongoza Bunge hili. Pia nampongeza Mheshimiwa Andrew John Chenge, wewe Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu na Mheshimiwa Najma Murtaza Giga kwa namna mnavyoweza kuonesha uwezo wenu mkubwa wa kuliongoza Bunge hili katika kipindi hiki. Pia nawashukuru sana Wabunge wenzangu wote kwa ushirikiano wao wanaoendelea kunipa, nawaombea kila la kheri katika utekelezaji wa majukumu yao hapa Bungeni na kwenye majimbo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee, napenda kuwashukuru wananchi wenzangu na wanawake wote wa Mkoa wa Njombe na kwa kipekee Jumuiya ya Wanawake Tanzania, Mkoa wa Njombe kwa imani kubwa waliyonipa na wanayoendelea kuonesha kwangu.

Nitaendelea kuwa nao karibu na kushirikiana nao kuleta maendeleo makubwa zaidi na naahidi kuwa sitawaangusha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuishukuru sana familia yangu, ikiongozwa na mume wangu mpendwa Dkt. George Yesse Mrikariya, kwa uvumilivu wao kwangu na kwa namna inavyonisaidia na kuniunga mkono katika majukumu yangu. Aidha, shukrani za dhati ziende kwa Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, viongozi, watendaji, wasaidizi wangu, Mabalozi, Wakurugenzi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa ushauri na msaada wao katika utekelezaji wa majukumu yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo, sasa nianze kujibu hoja mbalimbali zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge. Kwanza nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja hii ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na ni dhahiri kwamba michango yao itatusaidia sana katika kufanikisha shughuli za Wizara na kuimarisha ufanisi na utendaji wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nianze kwa kujibu baadhi ya hoja zilizotolewa na Kambi ya Upinzani na zitakazobakia Mheshimiwa Waziri ataendelea kuzijibu. Kambi ya Upinzani ilikuwa inataka kujua juu ya mpango mkakati wa Wizara na kama Wizara ina Mpango Mkakati wowote kuhusu utekelezaji wa diplomasia ya uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia mipango ya maendeleo ya Serikali ambayo inaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2020-2025 na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano hususan Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa mwaka 2016/2017 mpaka 2020/2021, unaojikita kwenye uchumi wa viwanda ambao utaiwezesha nchi yetu kufika katika uchumi wa kati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, mipango hiyo imekuwa ikiendana na mipango ya maendeleo ya Kikanda na Kimataifa kama vile Mpango wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa 2013/2014 - 2017/2018; Mpango Mkakati wa Maendeleo ya Ukanda wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC); Regional Indicative Strategic Development Plan (RISDP) wa 2005-2020; Agenda 2063 na Umoja wa Afrika pamoja na Mpango wa Maendeleo Endelevu wa 2030 wa Umoja wa Mataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utekelezaji wa mipango hii, Wizara imekuwa ikivutia uwekezaji, biashara na utalii na misaada kutoka nchi mbalimbali kupitia makongamano ya biashara ya uwekezaji na kushawishi wawekezaji wakubwa kuja kuwekeza nchini na kutangaza fursa zilizopo nchini kwenye sekta mbalimbali ikiwemo utalii, kilimo, madini, nishati na kadhalika. Ninyi wenyewe mmekwishakuona wawekezaji mbalimbali wamekuja Mikoa kama ya Pwani, Singida na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi ya Upinzani pia ilikuwa inataka tueleze kinaga ubaga hadi sasa kupitia diplomasia ya uchumi inavyoweza kujitangazia fursa zilizopo nchini kupitia Balozi zake kwa lengo la kuvutia uwekezaji wa kigeni, kuimarisha uhusiano wa kibiashara na mataifa mengine sambamba na kukuza sekta ya utalii nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vema ikaeleweka kuwa Sera ya Mambo ya Nje ni mwendelezo wa sera zote iliyojiwekea Serikali katika kujiletea maendeleo. Hivyo utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje unahusisha Wizara, taasisi zote za umma na sekta binafsi pamoja na wadau wengine ikiwemo Bunge hili. Maneno haya yalisemwa pia mwaka jana tukimweleza Waziri Kivuli wa Wizara hii lakini naona swali limajirudia vilevile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jukumu kubwa la Wizara yangu limekuwa siku zote ni kusimamia, kuratibu na kurahisisha utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje inayojikita kwenye diplomasia ya uchumi. Ni ukweli ulio wazi kuwa Wizara yangu hulifanikisha jukumu hili kwa kushirikiana na Wizara na taasisi zote pamoja na sekta binafsi. Hii inatokana na kuwa Wizara hii inahusika na masuala mtambuka ya Wizara tofauti kama vile kilimo, utalii, biashara, madini, elimu, afya na sekta nyinginezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fursa zilizopo nchini zinatangazwa na Balozi zetu ikiwa ni sehemu ya majukumu yao ya ubalozi. Balozi hizi huhudhuria makongamano ya uchumi, biashara, kilimo, elimu na kushiriki katika mialiko ya sekta hizo, hivyo, kupata fursa nzuri ya kuzitangaza fursa zilizopo nchini sambamba na kuweza kuvutia uwekezaji wa kigeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia majukumu ya Wizara na Sera yetu ya Mambo ya Nje pamoja na vipaumbele vya Taifa letu, Wizara iliandaa Kitabu Maalum (Ambassadors Handbook 2008) kinachoainisha majukumu ya msingi ya Balozi mbalimbali katika maeneo wanayowakilisha nchi yetu. Lengo likiwa ni kuhakikisha kwamba Balozi hizi zinadumu kwenye malengo ya Sera ya Mambo ya Nje inayoweka msisitizo kwenye diplomasia ya uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kambi ya Upinzani pia waliuliza swali kwamba ni kigezo gani wanatumia kuwateua Mabalozi na kwa nini inaonekana kwamba uteuzi wa Mabalozi hao unazingatia zaidi u-CCM na itikadi ya chama hicho badala ya kuzingatia zaidi utaalam, uzoefu, umahiri na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwakumbushe kuwa suala la uteuzi wa Mabalozi liko kwenye mamlaka ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushauriana na viongozi wengine mbalimbali ikiwemo Wizara. Uteuzi wa Mabalozi tangu na baada ya Uhuru umehusisha watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na kutoka Wizara na taasisi nyingine za Serikali na sekta binafsi kwa kuzingatia taaluma, uzoefu, weledi na uchapakazi wao. Ni busara hizo Marais wote watano wamekuwa wanateua Mabalozi kutoka kada za Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakuu wa Taasisi, Vyombo vya Ulinzi na Usalama, wasaidizi, viongozi wa Kitaifa na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakuwa hatutendi haki kama tutahitimisha kwa kusema kuwa viongozi wote hawa hawana sifa za kuwa Mabalozi baada ya kulitumikia Taifa kwenye nyadhifa mbalimbali muhimu kama hizo. Aidha, uteuzi umekuwa unazingatia matakwa ya eneo la uwakilishi kwa mfano utaona kabisa Mabalozi kutoka kada ya Vyombo vya Ulinzi na Usalama wanapelekwa sehemu zile zenye hitajio la aina hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mafunzo ya kuwajengea uwezo maafisa na kada yeyote ndani na nje ya Wizara hufanyika hapa nchini kwa kutumia vyombo vyetu vya nje na ndani kwa kulipiwa na Serikali yenyewe au nafasi hizo kutolewa na nchi na mashirika wahisani. Ni kwa msingi huo Wizara yangu inatumia kikamilifu fursa zote zinazojitokeza nje na ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala ambalo Kambi ya Upinzani pia waliuliza kwamba Wizara kwa muda mrefu sasa imeshindwa kutoa mafunzo ya diplomasia ya uchumi kwa maafisa wake badala yake kutegemea ufadhili kutoka nje na marafiki. Naona hii ni dhana potofu na tulikwishaizungumzia katika bajeti ya mwaka jana na nilifikiri labda pengine Waziri Kivuli ameelewa lakini naona niendelee kutoa elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu kupitia Chuo chake cha Diplomasia kilichopo Kurasini imekuwa ikitoa mafunzo ya Diplomasia ya Uchumi mara kwa mara kwa watumishi wa Wizara yangu na wadau wengine ili kuendana na mabadiliko ya kiuchumi duniani. Kwa Maafisa wa Mambo ya Nje ni lazima kujiunga na chuo hicho kama mojawapo ya sharti ya kupandishwa cheo. Aidha, Wizara pia imekuwa ikiwapeleka maafisa wake kuongeza ujuzi zaidi ya Diplomasia ya Uchumi kwenye nchi za China, Japan, Misri, Afrika Kusini, Uswis, Marekani, Urusi pamoja na nchi zingine kupitia bajeti yake na ufadhili wa nchi hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutafuta fursa za mafunzo nje ya nchi ni moja ya utekelezaji wa Sera ya Diplomasia ya Uchumi kwenye eneo la elimu. Aidha, chuo kimeandaa kozi fupi na ndefu za diplomasia ya uchumi kwa Waheshimiwa Wabunge na tayari chuo kimepeleka ombi kwa Wabunge Wateule wa Bunge la Afrika Mashariki walioteuliwa hivi karibuni ili nao waweze kushiriki katika kozi hiyo. Itakuwa ni upotofu kusema kwamba Wizara haijajipanga na haijatekeleza maelekezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Bunge lako Tukufu naomba kuweka kumbukumbu sawa kwa takwimu kwa mwaka wa fedha 2016/2017 watumishi 77 wamehudhuria mafunzo ya muda mfupi na wa kati na watumishi 14 wamehudhuria mafunzo ya muda mrefu ya Shahada ya Umahiri kupitia fedha za ndani na za wafadhili. Hivyo basi, mafunzo haya hayategemei ufadhili kutoka nchi marafiki peke yake kwa kuwa Wizara imekuwa ikitenga bajeti kwa ajili ya mafunzo haya kila mwaka na ukiangalia katika kila kitengo kuna bajeti ambayo inaonesha kwamba kuna mafunzo ya ndani na mafunzo ya nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Mheshimiwa Waziri Kivuli wa Wizara hii amesema hapa kwamba kwa miaka ya nyuma tumefundisha tu watu 32. Nataka niweke taarifa sawa, ile ilikuwa ni mwaka 2015/2016 ndiyo walikuwa wamefundishwa watu 32. Ili uweze kuelewa ni lazima ijue kwamba idadi ya watumishi ndani ya Wizara ile wapo wangapi na wangapi wanafundishwa kwanza, lazima waende kwa mpango. Huwezi ukapeleka wote 300 wakaenda shule wakati pengine hitajio ni watu 12, kwa hiyo, ni mipango mikakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo Kambi ya Upinzani wameulizia ilikuwa ni kwamba Wizara imechukua hatua gani katika kuvutia wawekezaji wakubwa kwenye sekta kilimo ambao asilimia 75 ya Watanzania wameajiriwa kwenye kilimo duni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema hapo awali, Wizara yangu ndiyo inayosimamia na kuratibu masuala ya mahusiano kati ya Tanzania na nchi nyingine duniani na mashirika ya Kimataifa. Kwa hiyo, tuna jukumu la kuratibu Wizara na taasisi nyingine kwenye masuala haya. Wizara imekuwa inatangaza fursa za uwekezaji na kuvutia wawekezaji kwenye sekta zote na siyo kilimo peke yake. Lazima ieleweke hiyo kwanza, mahitaji ni mengi ni lazima tuyashughulikie kwa pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kupitia ushiriki wa Mikutano ya Kimataifa, ziara za viongozi, makongamano ya kibiashara na uwekezaji, mikutano ya Tume ya Pamoja ya Kudumu pamoja na shughuli za kila siku za Mabalozi na Wizara yangu kwa ujumla huvutia wawekezaji kwenye miradi mikubwa ya kilimo katika kukuza sekta hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, katika Mkutano wa Jukwaa la Kiuchumi la Dunia kwa nchi za Afrika uliofanyika Dar es Salaam Mei, 2010, Tanzania ilichaguliwa kutumia Ushoroba wa Kati (Central Corridor) kuanzia Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania (SAGCOT) katika kuendeleza sekta ya kilimo. Ushoroba huu ulishindanishwa na nchi nyingine za Kiafrika na ukaibuka kuwa mshindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia SAGCOT, Tanzania imefanikiwa kuvutia makampuni makubwa kuja kuwekeza kwenye sekta ya kilimo nchini. Kwa sasa SAGCOT inaratibu miradi mbalimbali ya makampuni yasiyopungua 100. Miongoni mwa hayo, makampuni 80 yameshafanya uwekezaji na mengine yanaendelea kuwekeza. Makampuni 36 yameandika barua ya kukusudia kuwekeza na makampuni 20 yamefanya ubia wa kimkakati kwenye kuzalisha mazao mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile uwekezaji unaokadiriwa kuwa wa thamani ya jumla ya Dola za Marekani bilioni 1.2 umefanyika. Kwa mfano, mradi wa Shamba la Chai Iringa na Njombe (Unilever); mradi wa uzalishaji wa mchele Kilombero Plantantion (Morogoro); mradi wa kununua mbolea kwa wingi na kuifungasha hapa hapa nchini chini ya kampuni ya YARA; mradi wa maziwa

Asas Dairies (Iringa); mradi wa mbegu za viazi, Mtanga Food Limited (Iringa na Njombe) na mradi wa chakula cha kuku na uuzaji wa vifaranga, Silverland Tanzania Ltd (Iringa) ambapo mimi nashangaa na yeye anatoka huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hiyo inatarajia kuwaondoa kwenye umaskini wakulima wengi. Mpaka sasa zaidi ya Dola za Marekani 250,000,000 zinaendelea kuwekezwa kwenye uzalishaji wa mahindi, chai, viazi, soya, nyanya pamoja na huduma zingine za pembejeo. Haya ni matunda ya uratibu wa Wizara yangu katika kuvutia wawekezaji. Utasema kwamba akili ndogo inaongoza kubwa au kubwa inaongoza ndogo, ipi ni kubwa na ipi ni ndogo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushirikiano kati ya Tanzania na Mashirika ya Kimataifa kama vile FAO, IFAD, WFP pamoja na nchi marafiki imefanikisha misaada katika kuendeleza sekta ya kilimo nchini. Kwa mfano, IFAD imetoa msaada wa Dola za Marekani milioni 10 na mkopo wenye masharti nafuu na jumla ya Dola za Marekani milioni 56.6 kwa ajili ya kilimo cha miwa na uzalishaji wa sukari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utashangaa nimechukua muda mrefu, Waziri wangu amenituma niongelee hilo tu na yeye atasema machache, mengine tutayajibu kwa maandishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jitihada gani zinafanywa na Wizara katika kuchangamkia fursa za uchumi badala ya kusubiri nchi rafiki ambazo zenyewe zina ajenda zao. Wizara imeendelea kutafuta fursa za uchumi kwa kushirikiana na Wizara na taasisi zote za Serikali pamoja na sekta binafsi kupitia makongamano ya biashara na uwekezaji, mikutano ya kimataifa, Tume za Pamoja za Kudumu za Ushirikiano na mikutano ya ujirani mwema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, fursa zilizopo nchini zinatangazwa na Balozi zetu ikiwa ni sehemu mojawapo ya majukumu yake. Balozi hizo huudhuria makongamano, biashara, kilimo, elimu na kushiriki kwenye mialiko ya sekta hizo kwenye maeneo ya uwakilishi na hivyo kupata muda mrefu wa kuzingatia fursa zilizopo nchini sambamba na kuvutia uwekezaji wa kigeni. Hivyo, siyo kweli kwamba Wizara haichangamkii fursa za kiuchumi na badala yake kusubiri nchi rafiki zije. Huu ni mkakati, unaweza ukawaita wakaja na mkazungumza, mkamaliza mikakati yenu, lakini vilevile ukawafuata na tumefanya hivyo.