Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa shukrani za dhati kwa Waziri mwenye dhamana, Mheshimiwa William Lukuvi pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Angeline Mabula, sambamba na timu nzima ya Wizara chini ya Jemadari Kayandabila.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe malalamiko yangu kuhusu hatua ambazo zinachukuliwa na Idara ya Ardhi Kanda ya Kaskazini; tunalo shamba letu la Mnazi Sisal Estate ambalo kwa sasa linamilikiwa na mwekezaji wa Kenya kupitia kampuni ya Le-Marsh Enterprises ambayo inamiliki mashamba matatu yenye hati zifuatazo; tittle No.44144, ekari 562; tittle No. 17146, ekari 1188, pamoja na tittle No. 11247,
ekari 2442.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Lushoto ilitoa barua ya Notice of Revocation yenye Kumb. Na. LDC/ L.10/VOL.111/245-09/12/2016 kwenda kwa Kamishna wa Ardhi Kanda ya Kaskazini. Naomba nitoe masikitiko yangu kuwa barua hii inakaribia kumaliza mwaka lakini hadi sasa hakuna kinachoendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikichukua hatua za ufuatiliaji mara kwa mara kwenye Ofisi ya Kanda, lakini mara zote nilikuwa napata ushirikiano hafifu, ikiwemo mara ya mwisho, Mheshimiwa Waziri tulivyofanya mazungumzo, walitujibu kuwa kuna matatizo ya kiufundi kwenye taarifa ya notisi. Hili kwetu tunaliona kama ni hujuma kwa kuwa barua za Kiserikali hujibiwa kwa taratibu zake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama walivyo wawekezaji wote wababaishaji huyu Le Marsh Enterprises ni miongoni mwao na amekuwa akiwahadaa wananchi, Halmashauri na sasa anaonekana na baadhi ya Maafisa wa Ardhi Kanda, wanamlinda hivyo kusababisha chuki kubwa kwa wananchi husika wa Kata za Mbaramo, Mnazi, Lunguza ambao wanazungukwa na mashamba hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuna nia ya kumuonea mtu lakini tunahitaji kuona wananchi wanafaidika na rasilimali zao na pia kuona mapato ya Halmashauri yanapatikana bila kikwazo chochote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hitimisho; mwekezaji katika Mashamba ya Katani ya Mnazi ameshindwa kwa kiasi kikubwa kuyaendeleza mashamba anayoyamiliki. Kati ya ekari 4192 ni ekari 500 tu ndizo ambazo ameziendeleza kwa kupanda mkonge na kuvuna, ekari 1942 mkonge upo porini, kwenye vichaka hautunzwi kabisa. Ekari 1023 ni msitu mtupu ambao unatumiwa na wafugaji wa jamii ya kimasai kama malisho ya mifugo yao. Pia mmiliki huyo hajalipia kodi ya ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.