Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Rev. Peter Simon Msigwa

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Iringa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuturudisha tena Bungeni salama na ninaamini maneno ya Mheshimiwa Spika kwamba ulinzi utakuwa salama katika maeneo yetu ya Dodoma.

Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango nadhani kama Wabunge tumekushauri kuhusiana na jinsi ambavyo mliamua kutoa vyanzo vya mapato (own source) kwenye Halmashauri zetu ambavyo kimsingi vimeathiri sana maeneo mbalimbali. Kwa mfano, mlitoa ile property tax Manispaa yangu ya Iringa tulikuwa tukijiwekea bajeti ya kukusanya shilingi milioni 700 lakini hela iliyorudi kutoka TRA ni shilingi milioni 182 na hatujapata maelezo, TRA hawana hiyo capacity, hawana manpower ya kukusanya hiyo hela wakati sisi tulikuwa tunakusanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile mmechukua hela ya mabango ambayo tulikuwa tumejipangia kwenye bajeti kukusanya karibuni shilingi milioni 357, hiyo hela bado haijapatikana na kwa kukosekana kwa hela hii, tumeshindwa kutengeneza chumba cha uchunguzi katika Hospitali yetu ya Wilaya ya Frelimo, tumeshindwa kujenga wodi ya wagonjwa katika eneo linaitwa Itamba katika Manispaa yangu, na hizi ni athari ambazo tulizisema toka mwanzo kwamba tulikuwa na uwezo wa kukusanya baada ya nyinyi kutoa hivi vyanzo mme-cripple maendeleo yetu kama Manispaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni mifano inawezekana na wenzangu kwenye maeneo yao kuna matatizo kama hayo, ningeomba kama inawezekana katika mpango huu mngerudisha hivi vyanzo vya mapato vibaki katika maeneo yetu. Ninavyozungumza Manispaa yangu ya Iringa ni moja ya Manispaa bora kabisa mpaka maeneo mengine wanakuja kujifunza namna ya usafi, namna ya kupanga Mji, lakini mkiendelea kutu–cripple namna hii mtaturudisha nyuma, nadhani hata Naibu Waziri alikuwa DC pale anajua jinsi Manispaa ya Iringa ilivyo nzuri, ikiongozwa na CHADEMA katika Mkoa wetu wa Iringa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite katika eneo moja kubwa, katika kitabu chako ulichotuletea ukurasa wa 35 umezungumzia kuhusu utawala bora. Kwangu hayo uliyoyazungumza kwenye utawala bora naweza kusema hii ni hardware hujazungumza software. Utawala bora niliotaka uzungumzie wewe umezungumzia kuhusu mahakama ambazo zitajengwa ambazo zinataka kujengwa, kwangu mimi hiyo ni hardware. Mimi nataka tuzungumzie component, characteristics za utawala bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili nchi yetu iweze ku-flourish lazima utawala bora uonekane kwa vitendo. Katika hotuba ya Kambi ya Upinzani ukisoma ukurasa wa tatu tumezungumza vizuri sana, naomba ninukuu: “Misingi ya uwajibikaji katika kutekeleza mipango ya maendeleo ipo kikatiba na kisheria. Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ya mwaka 1977 inalipa Bunge mamlaka ya kujadili na kuidhinisha mpango wowote wa muda mrefu au wa muda mfupi unaokusudiwa kutekelezwa katika Jamhuri ya Muungano na kutungia sheria.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kuwa na mipango mizuri kama Serikali yenyewe haiko accountable, inakwepa accountability. Kipindi cha nyuma Serikali ilikuwa inapaswa iwe inaleta namna inavyotekeleza bajeti kila baada ya miezi mitatu, juzi hapa tumepitisha sheria ambayo asubuhi leo tumeambiwa kwamba imeshapitishwa kwamba tutakuwa tunaletewa utekelezaji wa Serikali kila baada ya miezi sita, na sasa hivi tumeshaanza mpango wa mwaka unaokuja wakati utekelezaji wa Serikali muda uliopita hatujaupata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakuwa hatuna uwezo wa kusema tunaisimamia Serikali kama Serikali yenyewe inakwepa accountability. Nasema hivyo kwa nini, mfano mzuri kama tunapanga vizuri matumizi yetu ya fedha Waziri wa Maliasili ambaye amebadilishwa juzi alikuja Iringa kule tulikuwa tunahamasisha mambo ya utalii huku Southern Circuit na mojawapo ya mambo ambayo tuliyajadili ilikuwa ni pamoja na kuuboresha uwanja wa Nduli kwa sababu Iringa imekaa ki- strategy.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mbuga ya wanyama ambayo tuna-attract watalii na maeneo mengine, tukazungumzia kuhusu barabara, lakini kwa sababu Serikali haitaki kuwa accountable, imechukua hela ambazo hazikuonekana popote kwenye vitabu vyako ulivyotuletea hapa ikaenda kupeleka Chato shilingi bilioni 39 mnajenga uwanja wa ndege Chato, mnaacha mahali kama Iringa ambapo pamekaa kimkakati na Wizara ya Maliasili wamesema pale pamekaa kimpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano inaonekana ni ya ubinafsi mkubwa sana, Mwalimu Nyerere angekuwa mbinafsi..

T A A R I F A . . .

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa yake naipuuza na kama ninavyompuuza mwenyewe, siichukui. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia Chato, nimezungumza mipango kama tuna-synchronize, Iringa imekaa kimkakati kwamba tukijenga kiwanja cha ndege kuna tija tutakayoipata kutokana na kiwanja cha ndege. Kujenga kiwanja cha ndege Chato tunataka tupate nini? Tulikuhoji muda uliopita hatukupata majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano inaonesha ubinafsi wa hali ya juu, kama Mwalimu Nyerere angefanya hivyo Musoma ingekuwa Ulaya, lakini Mwalimu alikuwa anafanya mambo kimkakati, hatuwezi kusema tunataka tujenge, tupanue uchumi wa viwanja kwa upendeleo wa namna hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, hili la Serikali inatakiwa ilete matumizi ndiyo dhana nzima ya Wabunge kuwepo hapa, tukiua dhana nzima ya Bunge kuisimamia Serikali, Bunge linakuwa halina maana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana nimezungumza kwenye briefing nimesema ukisoma historia kwa wale wanaosoma historia, nenda Ufaransa, nenda Uingereza, kwa nini waliwaua wale wafalme? Ni kwa sababu kodi yao walikuwa wanaitumia pasipo kusimamiwa, Bunge likaanzishwa ili liwe ni mlinzi wa Serikali. Sasa vifungu vyote hapa tumenyofoa kwa maana ya kwamba tunali-cripple Bunge, Serikali inaanza kujifanyia kama inavyotaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hazina ya nchi hii siyo mali ya mtu mmoja. Hazina ya nchi hii ni mali ya Watanzania na sisi ni tax payer representative, tukiacha kuisimamia Serikali ifanye inavyotaka tuna deceit the whole purpose ya kuwa na Bunge. Bunge siyo kuja kuvaa suti hapa, Bunge ni kuisimamia Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapozungumzia good governance kuniambia kumejengwa mahakama, nimezungumza hiyo ni hardware, components za good governance kuna accountability. Serikali ya Awamu ya Tano inakataa accountability, haitaki kufuatiliwa, hamtaki tujue mmetumia kiasi gani na kuwepo kwa Bunge ni kutaka kujua Serikali imetumia kiasi gani na imetumia kama tulivyopanga kwa mujibu wa sheria. Kwa hiyo, hauwezi kuniambia good governance hapa kama hatuwezi kufuata sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Awamu hii ili tuzijue characteristics of good governance unaweza uka-google tusaidiane haya ninayoyasema, hii ni UNDP ilitoa mwaka 1997, inasema lazima kuwe na participation. Mme-cripple Halmashauri ambazo ndiyo hela zikienda kule chini wanashiriki watu kuanzia chini, sasa hakuna hela, wamekuwa crippled.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima kuwe na rule of law, good governance, human rights, democracy. Katika nchi hii hakuna democracy, watu wakitaka kuzungumza, wakitaka kuhoji wanakataliwa, tunawezaje kuutekeleza Mpango huu kama haya mambo hayapo? Ili Mpango uweze kutekelezwa ni lazima haya mambo yawepo nazungumzia good governance. Hii good governance it is not about Upinzani tu, good governance ni kwa wote, kwenye maeneo ya Manispaa zetu wote, haya mambo hayapo, ukienda mbele inasema hakuna upendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, asubuhi Naibu Waziri anajibu hapa maeneo mengine wanaambiwa kwamba ninyi kwa sababu mlinipa kura hamtabomolewa, maeneo mengine ma- bulldozer yanaenda yanabomolea watu, kutakuwa na good governance hapo?

KUHUSU UTARATIBU . . .

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nasoma good governance, kuna utawala bora kwenye hiki kitabu, kwa hiyo nimejikita hapo na haya maneno ninayozungumza Waziri alisema hivyo, mimi nayanukuu maneno aliyosema Rais alipokuwa Kanda ya Ziwa alisema ninyi hamtabomolewa kwa sababu mlinipa kura. Nimesema kwenye characteristics za good governance lazima kusiwepo na upendeleo. Ukienda Kimara, ukienda Tabora huko bulldozer yanapita yanabomoa nyumba kwa nini tunajitoa ufahamu? (Makofi)

Kwa hiyo Mheshimiwa Mhagama anaongea kitu kingine mimi nazungumzia nukuu za Mheshimiwa Rais alizosema, jamani hamkusikia haya mambo? Ndiyo ninayoyazungumza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo la kunajisi Bunge nalitoa, lakini mtuambie kama hatuwezi kumnukuu Rais, Rais hatuwezi kumnukuu?

Mheshimiwa Rais alisema waliojenga kwenye mito wasiondolewe wakati Mwenyekiti wetu hapa mmebomoa kwake, sasa tusiseme haya maneno? Haya ndiyo nayasema good governance, hii hela tunayoitoa hapa ni pamoja na kuhakikisha Polisi wanafanya kazi vizuri, Usalama wa Taifa wanafanya kazi vizuri. Ninachosema, tulipata taarifa kwenye vyombo vya habari kwamba wale waliompa kura watasamehewa na wengine watabomolewa. Huo ndiyo msimamo wangu, hiyo haikataliwi.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Mipango, kama kweli tunataka mipango hii itekelezwe lazima tuwe na good governance. Tuko kwenye nyakati ambazo usalama wa raia hauko vizuri, tuko kwenye nyakati ambazo watu hawana uhakika na maisha yao, kwa hiyo, tunapozungumzia kupanga mipango mwenzangu Mheshimiwa Bobali amezungumza hapa kwamba tusije na kauli tu kwamba sasa hivi tunasema viwanda. Utawala uliopita wa Awamu ya Nne ilikuwa Big Results Now ambayo imevunjwa juzi juzi na niliwahi kusema nilikuwa hapa hapa, nikasema Big Results haitatokea kwa sababu tu ya kubandika vibao kwamba Big Results, milango yote ya Halmashauri iliandikwa Big Results, lakini hiyo Big Results haikuonekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haikuonekana! Mbona ninyi wenyewe mnaiponda Serikali iliyopita! Leo tumekuja na kelele za viwanda, kuwa na viwanda ni jambo jema hakuna mtu anayekataa. Lakini kama alivyosema Mheshimiwa Bobali, hivi viwanda lazima tuwe na mipango mkakati, lazima tuwe na maeneo ambayo tunaamini yatatusaidia kuleta mipango mikakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumlinda Mbunge mwenzetu ambaye alipata mateso makubwa sana kwa hawa watu wanaoitwa wasiojulikana. Kwa masikitiko makubwa wale wahalifu, wale ambao walikuwa wapo tayari kutoa uhai wa mwenzao kwa matakwa yao ambao hawajulikani mpaka leo ambao siyo mhimili huu, siyo Serikali, siyo Mahakama sijaona zimepiga kelele za kutosha kwa kitendo kibaya alichofanyiwa mwenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba Wabunge wote kwa umoja wetu tusikubali mateso aliyoyapata mwenzetu miongoni mwetu yeyote aje ayapate kwa sababu ni kitu ambacho Mungu hapendi. Sisi sote hapa ni ndugu, mwisho wa siku tunaijenga Tanzania, tusimame wote kwa pamoja kulaani. Waasisi wa nchi hii hawakutufundisha mambo yanatokea sasa hivi katika nchi hii. Kuona maiti kwenye viroba, kupigana, kuchukizana, kununiana, haya mambo hatukujifunza, tunayaona katika Awamu ya Tano haya mambo yanachipua, tuyakatae wote kwa pamoja kama Bunge ili kwa pamoja tushirikiane, tuhakikishe nchi ya viwanda tunayoitaka, tuweke mikakati ambayo tutakubaliana wote kwa pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana.