Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Manyoni Magharibi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi nichangie katika Mpango huu wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2018/2019 pamoja na Mwongozo wake wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya mwaka 2018/2019.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapongeza juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali yangu, Serikali ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika jitihada zake za kuhakikisha rasilimali za nchi hii zinanufaisha wananchi wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niipongeze Serikali kwa jitihada za kusogeza huduma karibu na wananchi ikiwemo hili kubwa la Serikali kuhamia Dodoma ambapo ni katikati na Makao Makuu ya nchi hii. Kuna kazi nyingi zinazofanywa na Serikali ni njema kabisa, lakini pia kuna changamoto kadhaa. Sasa mimi nijielekeze sasa hivi katika changamoto, lakini pia katika kupongeza yale ambayo yamefanywa mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais na Serikali yake na Mawaziri wake ambao tuko nao hapa wamejitahidi na wameonesha dhamira ya kweli katika ujenzi wa reli katika kiwango cha standard gauge ambacho leo mkandarasi wa pili ameshasaini mkataba, reli hii itasogea hadi karibu na Mkoa wa Singida, kule Makutupora. Mimi nikiwa Mbunge wa Mkoa wa Singida, mikoa ya katikati ni mikoa ambayo inanufaika sana na itanufaika na ujenzi wa reli hii ya kati kwa kiwango ambacho ni cha standard gauge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tunazo changamoto pamoja na jitihada kubwa sana za Serikali kutaka kuunganisha mikoa yake ifikike kwa njia ya barabara. Mkoa wa Singida ukiwa mmojawapo kuunganishwa na Mkoa wa Mbeya, lakini pia na Mkoa wa Simiyu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mpango nimeona jitihada zinazofanywa na Serikali katika kuhakikisha miundombinu hii inafanyika, lakini niombe jicho la tatu katika barabara za Mkoa wa Singida kuunganishwa na Mkoa wa Mbeya. Barabara inayotokea Mkoa wa Singida kuunganishwa na Mkoa wa Simiyu kupitia Daraja la Sibiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, njia kuu na uti wa mgongo wa uchumi wa nchi yoyote duniani miundombinu ikiwa rafiki ni rahisi mwananchi kutoka sehemu moja na kwenda sehemu nyingine, itarahisisha ulipaji wa kodi na hata kuirahisishia Serikali kukusanya maduhuli na kodi mbalimbali kupitia wananchi hawa wanapowezeshwa katika kuhakikisha wanasafiri na kupeleka mazao yao katika masoko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jitihada za kufanya Makao Makuu Dodoma ningeomba sana Serikali iangalie barabara inayotoka Mkiwa kwenda Rungwa hadi Makongolosi. Kuna ahadi ya Serikali ya kuijenga barabara ile katika kipindi hiki, lakini kumekuwa na ukimya ambao hatuuelewi. Sisi Wabunge ambao tulienda kuwaambia wananchi kule kwamba Serikali yenu sikivu ya Chama cha Mapinduzi, mimi nikiwa Mbunge wake, tumeiomba na imekubali kujenga barabara na hata Mheshimiwa Rais alipokuja pale aliendelea kutoa ahadi hii, lakini kumekuwa na ukimya ambacho tunapata kidogo mashaka, tunaomba basi mje mtuambie mmefikia wapi katika kujenga barabara ile kutoka Mkiwa kuelekea Rungwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiki ni kipande pekee ambacho kimebaki kikubwa chenye urefu mkubwa, barabara hii ambayo leo bado ni kilometa 413. Ni barabara pekee ambayo ni ndefu, lakini barabara ya zamani, barabara ambayo ina uchumi mkubwa sana katikati yake kuna reserve za wanyama na maeneo mbalimbali, lakini na wakulima wengi wazuri wako maeneo haya ambayo tunatarajia kuleta na kuuza mazao hapa Dodoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine ambalo tunahitaji tuiombe Serikali yetu ilifanyie kazi kwa bidii sana ni suala la umeme vijijini. Kuna maeneo mengine kazi imefanyika vizuri na nipongeze jitihada za Mawaziri husika kwa kazi wanazozifanya, hasa Mheshimiwa Kalemani, lakini na Naibu ambaye ameteuliwa hivi karibuni, naona jitihada zake zinaweza zikatupeleka pazuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu umeme vijijini Mkoa wa Singida, mkandarasi alitangazwa, lakini baadaye akapotea. Tulipofuatilia tukaambiwa kwamba, yule mkandarasi kuna sifa zilipungua, walishindwana naye, kwa lugha ya sasa tunasema alitumbuliwa. Sasa alipotumbuliwa ndiyo wamepata mkandarasi mwingine, leo wananchi wa Mkoa wa Singida hatujafika popote, hakuna hata kijiji kimoja ambacho unaweza ukasema REA Awamu ya Tatu nayo imeanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe basi Serikali yangu ya chama changu basi iwaangalie wananchi waaminifu wa Mkoa wa Singida katika umeme vijijini. Ni eneo pekee ambalo lina tatizo sana vijiji, vingi havijafikiwa na umeme na mimi naamini mkifanya hivi itatusababisha sasa na wananchi wa Singida, maeneo yote ya Mkoa wa Singida na hata Mkoa wa Dodoma bado wakandarasi hawa wanaonekana hawajafanya kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna ahadi zetu kwa wananchi wetu kuhakikisha tunaboresha huduma za afya katika vijiji vyetu kwamba tujenge zahanati kila kijiji. Wananchi wameanza kujenga kwa juhudi, Serikali zao za vijiji na wakati mwingine tunaiomba Halmashauri au Serikali itusaidie kufunika yale maboma, lakini tuliahidi kila kata kujenga kituo cha afya. Hili naomba sana katika mipango tunayokwendanayo nalo tulizingatie, ni miongoni mwa mambo ambayo ninaamini yatatufanya tuwe na jambo zuri la kufanya huko mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maji vijijini ni changamoto kubwa sana. Vijiji vyetu vingi na hasa mikoa kame hii ya Dodoma na Singida hatuna mabwawa, basi tufanye juhudi za makusudi angalao basi malambo madogo madogo katika maeneo mbalimbali. Tumekuwa tukisema hapa Wabunge tunaotoka katika mikoa hii kwamba, kungekuwa na mito basi angalau, hatuna mito, mito ile ni ya msimu mvua ikinyesha baadae jioni imekauka, njia rahisi ya kusaidia wananchi ni kuchimba visima. Halmashauri zetu tunajitahidi, Serikali basi ituunge mkono katika hili ili wananchi wetu wengi nao wapate huduma hii. Ninaiomba Serikali mlitolee jicho la tatu kuona vijiji vyetu vingi vinapata huduma hii ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na wenzangu katika kuona kwamba, sasa gesi hii ambayo ipo kwenye Mikoa ya Kusini imefika Dar es Salaam. Ni wakati sasa wa kuona na kujipanga na kuona tunafanyaje ili gesi hii ipite mikoani ikiwezekana ifike hadi Mwanza kwa kupita Dodoma, ikija Morogoro – Dodoma – Singida pengine Simiyu au Shinyanga ikafika mikoa ya Kanda ya Ziwa ambapo kuna viwanda vingi. Naamini watu wanashindwa kujenga viwanda maeneo mengine kwa sababu tu pengine ya miundombinu, likipita bomba la gesi tukawekeza katika gesi, nchi hii ninaamini kule mbele hatutakuwa na changamoto kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wawekezaji wako wengi wana nia ya kuwekeza, lakini changamoto hizi za miundombinu ikiwemo matatizo ya umeme, kukatika-katika kwa umeme kunasababisha watu wapate uwoga wa kufanya hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango basi muangalie mipango madhubuti ya kuhakikisha bomba la gesi linakwenda hadi Mwanza pengine na Mikoa ya Kaskazini na hata Mikoa ya Kusini kama Mbeya na maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leo nilikuwa na haya machache yanatosha. Ahsante sana.