Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Mohamed Omary Mchengerwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rufiji

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakiri kabisa kwamba Seneta Ndassa amenifilisi kidogo ni kama vile ameingia kwenye hotuba yangu ya siku ya leo, kwa sababu nami sikupendezwa na mijadala, hususan ya siku ya jana ambayo ilikiuka kabisa Ibara ya 28 ya Katiba, ambayo inatutaka sisi Waheshimiwa Wabunge, au Watanzania wote kuwa na Utaifa. Pia inakiuka Ibara kadhaa ambazo nitapenda kuzizungumza hapo mbele, lakini nitajaribu kuzungumza kitaalam zaidi ya vile ambavyo Mheshimiwa Mzee Ndassa amezungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana wewe, tarehe 17, mwezi Oktoba, nilipata fursa ya kutembelea Lenin’s Mausoleum, ni kaburi la Vladmir Lenin, Baba wa Taifa la Kirusi na nilifanya hivyo kwa sababu mimi ni mmoja wa wapenzi sana wa siasa za ujamaa na nimesoma vitabu vyake vingi sana. Nilifanya hivyo pia kukumbuka dhima ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ya Ujamaa na Kujitegemea lakini pia ya kuchapa kazi na kuwaunganisha Watanzania kuwa kitu kimoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi napenda kusema kwamba Mwalimu Nyerere ni Baba wa Taifa letu kama alivyo Vladmir Lenin ambaye amehifadhiwa pale Moscow Kremlin
- Russia na anapewa uangalizi mzuri na wananchi wa Kirusi. Pia kama Watanzania napenda kunukuu maneno ya William Shakespeare aliyewahi kusema katika Hamlet moja, mbili mpaka 187; alisema kwamba: “He was a man take him for all in all, I shall not look upon his like again”

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami napenda nimnukuu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa sababu alituunganisha Watanzania bila kujali itikadi zetu pamoja na imani zetu za dini pamoja na ukanda na ukabila. Hayo yote nimeona niyaseme kwa sababu nami sikuridhika sana na mijadala hususan ya siku ya jana.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mtanzania asiyeona kazi nzuri inayofanywa na Rais, Dkt. John Pombe Magufuli huyo ni mgonjwa. Nasema kwa sababu yuko Mwandishi mmoja wa vitabu anaitwa Said Nusi, mwaka 2016 alitoa kitabu chake kinachosema Ujumbe kwa Wagojwa. Said Nusi alisema kwamba Mwenyezi Mungu ameshusha magonjwa kwa wanadamu na ameweka dawa yake katika famasia za ardhi na akawateua wanadamu kuweza kuwatibu walio wagonjwa kwa kuwapa uwezo yeye mwenyewe japokuwa yeye Mwenyezi Mungu ndiyo anatoa maradhi na yeye mwenyewe ndiyo wa kuyaponywa maradhi hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, uzalendo mkubwa anaoufanya wa kulinda rasilimali za Taifa hauwezi kupimwa na mtu yeyote katika nchi yetu hii na hauwezi kupingwa hata kidogo. Nami binafsi natambua maandiko yaliyowahi kutolewa na Shaaban Robert katika tenzi zake alizowahi kumsifu Siti Binti Saadi, kwa wale wasomaji wa vitabu watawiana na mimi. Itafika wakati Watanzania tutahitaji kuenzi mambo mazuri yanayofanywa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ambaye amekuja kutibu na akipigania rasilimali, kupambana na rushwa, ufisadi na mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kikubwa zaidi nimpongeze sana Rais huyu kwa kupambana kuhakikisha kwamba Ibara za tatu na tisa za Katiba ya Ujamaa na Kujitegemea inalindwa katika nchi yetu. Binafsi napenda sana kuamini katika ujamaa na kujitegemea na Tanzania bado tupo katika ujamaa na kujitegemea, hakuna anayeweza kupinga jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona niseme hili kwa sababu mwandishi wa vitabu Martin Harok aliwahi kusema na kunukuliwa kwamba siasa hizi za ujamaa na kujitegemea ambapo nchi yetu inafuata command economy ni moja ya siasa bora kabisa ambazo zinadhamiria kujenga dhamira moja ya Kitaifa yenye kutoa matokeo chanya, kuwa na National Goals na as a results of the National goals often defensive and generally ruthless commitment to a single goal, ambapo sasa hapa tunaona kuna viwanda, reli standard gauge pamoja na suala zima la Stiegler’s Gorge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya nane ya Katiba inazungumzia kwamba nchi ni ya wananchi na wananchi ndio wenye nchi hii ya Tanzania na Serikali ina mkataba na wananchi na tutapimwa 2020 wakati tunapokwenda tena kuomba kura kuelezea yale mambo mazuri tuliyoyafanya. Naomba ninukuu Ibara ya 9(g) ambayo inazuia Serikali na vyombo vyake vyote vya umma kwamba: “Kwamba Serikali na vyombo vyake vyote vya umma vitatoa nafasi zilizo sawa kwa raia wote, wake kwa waume, bila ya kujali rangi, kabila, dini au hali ya mtu.”

Pia Ibara ya 13(4) pamoja na Ibara ya 13(5) pamoja na Ibara ya 28 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimezuia ubaguzi na mijadala yote yenye dhamira ya kuwatenga au kuwabagua Watanzania kwa kufuata ukanda, ukabila au udini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mijadala hii kwa mujibu wa Ibara ya 28 ya Katiba inayotutaka Watanzania kulinda Utaifa, basi uizuie na iwapo Mheshimiwa Mbunge yeyote atazungumzia mambo haya ya ukanda basi azuiliwe na asiruhusiwe kuzungumza mbele ya Bunge lako hili Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku ya jana ilikuwepo mijadala mingi na mizito. Kwanza kabisa ni kuhusu ujenzi wa uwanja wa ndege wa Chato. Binafsi kuna watu ninaowaamini sana ndani ya Bunge lako hili Tukufu, sijawahi kuhoji hata siku moja uwezo wa Mheshimiwa Dkt. Mukasa, namwita Dkt. kwa sababu naamini ni mtu mwenye uwezo mkubwa, lakini sijawahi kuhoji uwezo wa ndugu yangu Mheshimiwa Innocent Bashungwa kwa sababu naamini ni watu wenye uwezo mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo lazima asimame mtu wa Kanda ya Ziwa kutetea uwanja wa ndege wa Chato, wananchi wa Jimbo la Rufiji tunaweza tukasimama na tukatetea vema kwa sababu maandiko yanasema a good defender is the one who knows how to defend. Wanasheria tunaamini kabisa kwamba Mwanasheria bora ni yule anayejua wapi pa kuitafuta ile sheria, a good Lawyer is the one who knows where to find the law.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona niliseme hii kwa sababu ukisoma Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ukurasa wa 55 mpaka 58 unazungumzia ujenzi wa viwanja vipya vya ndege, pia kuboresha viwanja tulivyonavyo. Hii ni Sera na Ilani ya Chama cha Mapinduzi, haihitaji mtu wa Kanda ya Ziwa kuitetea, ni Sera ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo Serikali inaelekeza mambo yake kutokana na Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanja vinavyojengwa ni vingi, siyo kiwanja cha Chato peke yake, tunacho Kiwanja cha Kigoma ambacho kitajengwa, kuna Kiwaja cha Mafia ambacho kitajengwa, kipo kiwanja cha Mtwara ambacho kitajengwa. Hii ni kwa mujibu wa Ilani lakini pia ni kwa mujibu wa mpango ambao umewasilishwa na Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna ujenzi wa reli, ujenzi huu unakwenda kusaidia uchumi kwa sababu dhamira ya Chama cha Mapinduzi ni kunyanyua njia kuu za uchumi ili kuwafanya Watanzania waweze kutoka kwenye uchumi wa kawaida na kwenda kwenye uchumi wa kati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze sana Serikali kwa mchakato wa ujenzi wa Bwawa la Stiegler’s Gorge, hii ni fikra ya Mwalimu mwaka 1956 Mwalimu Nyerere alidhamiria kwamba baada ya uhuru atajenga Bwawa la Stiegler’s Gorge ili kuweza kusaidia nchi yetu kuweza kupata umeme wa kutosha na kuweza kuuza nje ya nchi. Niwapongeze sana wananchi wa Jimbo la Rufiji, hususan wa Kata ya Mwaseni ambao wamelitunza bwawa hili kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2015 muda kama huu nilisimama mbele ya Bunge lako Tukufu na nikahoji ni kwa nini Wilaya yetu ya Rufiji, Kilwa pamoja na Kibiti tunakosa umeme kwa siku tunapata umeme kwa saa nne, wakati tunayo Stiegler’s Gorge. Mwaka 2016 nilihoji pia ndani ya Bunge lako hili Tukufu ni kwa nini nchi hii tunauza umeme ghali wakati tunayo Stiegler’s Gorge ambayo tunaweza kuzalisha umeme na tukasambaza nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunategemea kujenga reli ambayo inakwenda kutumia umeme, lakini pia tuna viwanda ambavyo vinajengwa kila siku. Nimpongeze ndugu yangu, Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Jafo kwa kuzindua mchakato wa ujenzi wa viwanda, viwanda hivi vitahitaji umeme na umeme huu ni wa Stiegler’s.

Mheshimiwa Spika, ninachoiomba Wizara ya Nishati ni kuzingatia umeme huu wa Stiegler’s Gorge uweze kuwanufaisha pia na wananchi wa Rufiji. Nimwombe Waziri wa Nishati atakaposimama hapa aseme, baada ya ujenzi wa Stiegler’s Gorge mchakato mzima upitie katika Wilaya yetu ya Rufiji ili Kata ya Mwaseni iweze kunufaika, wananchi wa Mloka na maeneo mengine waweze kunufaika, wananchi wa Kata ya Kipugila waweze kunufaika,wananchi wa Kata ya Mkongo waweze kunufaika, wananchi wa Kata ya Ngorongo waweze kunufaika na wananchi wa Jimbo zima la Rufiji waweze kunufaika kutokana na mradi huu mkubwa wa umeme kwa sababu wananchi wa Rufiji ndio waliolitunza bwawa hili toka mwaka 1956 mpaka leo hii. Haya ni maneno ambayo nimeyazungumza kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa miundombinu natambua dhamira ya Serikali ya kujenga miundombinu mbalimbali ili kuweza kuboresha njia kuu za uchumi, Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, tarehe 3 Machi, aliwaahidi wananchi wa Tarafa ya Ikwiriri kwamba kabla ya mwaka 2020 atajenga barabara ya Nyamwage kuelekea Utete. Niombe sana, kila Mbunge anatamani kuacha legacy atakapoondoka, mwaka 2020 nitakaposimama kuomba kura na mimi nitaacha legacy yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Rufiji tunasema, labda pengine hakuna mwingine yeyote zaidi ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli iwapo barabara hii ya Nyamwage kuelekea Utete itajengwa, Makao Makuu ya Halmashauri yetu. Rufiji ilianzishwa wakati wa mkoloni ni Wilaya ya sita wakati huo, lakini hatuna hata nusu kilometa ya barabara ya lami.

Mheshimiwa Spika, tunaamini kabisa Rais wetu akiijenga barabara hii ya Nyamwage – Utete aliyoahidi mwenyewe kwamba kabla ya mwaka 2020 barabara hii itakuwa imekamilika, lakini katika mpango sijaliona hili, kama kuna uwezekano walirekebishe ili wananchi wangu wa Jimbo la Rufiji waweze kunufaika na uchumi huu ambao wanachangia kupitia maliasili na utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo barabara yetu ya Ikwiriri kuelekea Kata ya Mwaseni, naomba sana, kwa kuwa Serikali inakwenda kujenga bwawa la Stiegler’s Gorge, hakuna namna tutaepuka kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba Serikali kutokana na makusanyo tunayoyapata, ianze kujenga barabara ya kutoka Nyamwage kueleka Utete ili wananchi waweze kupata barabara yao ya Halmashauri kwa mara ya kwanza toka tumepata uhuru. Pia barabara ya Ikwiriri kuelekea Mwaseni ni barabara muhimu sana, hali kadhalika barabara ya kutoka Bungu kuelekea Nyamisati katika Wilaya ya Kibiti ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niipongeze Serikali sana kwa kutuletea miradi mingi ya maji. Naipongeza Serikali na nampongeza Waziri wa Maji, baada ya kuteuliwa tu kuwa Waziri alifika Rufiji na kujionea miundombinu mbalimbali ya maji.

Mheshimiwa Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri wa Maji ahakikishe kwamba ile miradi anayotuletea ambayo nilimwomba mwenyewe inayokwenda katika Kata za Mbwara, Chumbi, Utete, Mkongo, Ngarambe, Kipugira na nyingine, basi iweze kukamilika kwa wakati ili mwaka 2020 tuweze kutamba kwamba tumeweza kuwafanyia wananchi jambo fulani ambalo litakuwa na manufaa kwao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kilimo, kilimo kimezungumzwa katika makaratasi, namwomba Mheshimiwa Dkt. Mpango, Rufiji tuna ardhi ya kutosha na wakati fulani tulipewa taarifa na Waziri wa Viwanda kwamba atatujengea kiwanda cha sukari katika Kata za Chumbi, Mbwara pamoja na Muhoro. Nimwombe Mheshimiwa Waziri, tunatambua wapo wawekezaji mafisadi waliochukua ardhi yetu wananchi wa Rufiji na kuishikilia ili kutafuta wawekezaji wapate cha kwao cha juu.

Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali na nimwombe Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwa ukali anaoufanya katika kujenga uchumi wa nchi yetu, anyang’anye ardhi hii mara moja ili tuweze kupata kiwanda hiki cha sukari kwa mara ya kwanza katika nchi yetu na kwa mara ya kwanza katika eneo letu la Rufiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Magufuli, anyang’anye ardhi hii ambayo imechukuliwa na mwekezaji mmoja mfanyabiashara aliyeimiliki na hataki kujenga kiwanda, amezuia Serikali kuweza kupata mwekezaji wa kujenga kiwanda hiki, ardhi hii iweze kunyang’anywa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia niikumbushe Serikali, Rufiji tuna square kilometers 500,000 ambazo ziko ndani ya Bonde la Mto Rufiji. Naiomba sana Serikali kuona namna ya kuboresha kilimo katika maeneo yetu ili wananchi wa Rufiji pia tuweze kunufaika na Serikali yetu na tuseme kwamba tunatembea kifua mbele kwamba Serikali ya Awamu ya Tano sasa imedhamiria kuunyanyua uchumi wa wananchi wa Rufiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirejee katika elimu. Sote kabisa tunatambua kilichotokea Rufiji na Kibiti kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja tumeshindwa kufanya siasa, wananchi wameshindwa kushiriki katika kilimo lakini kitu kikubwa ambacho kinatukwamisha ni tatizo kubwa la elimu.

Mheshimiwa Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri wa Elimu, kama ambavyo aliweza kutenga fedha za uboreshwaji wa shule za sekondari za Kibiti, Muhoro na sekondari ya Utete namwomba pia aone uwezekano wa kuboresha miundombinu ya shule zetu, hususan shule ya Sekondari ya Ikwiriri pamoja na miundombinu ya shule zetu mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua, ukiangalia takwimu tulizonazo leo hii katika maeneo ambayo yameathirika sana na elimu ni eneo la Rufiji, Kibiti, Kisarawe na maeneo mengine ya Pwani. Leo hii tuna watoto zaidi ya 300,000 nchi nzima ambao wanaacha shule bila sababu maalum. Nimwombe Waziri wa Elimu akisimama hapa atuambie mpango mkakati ambao Serikali itakuja nao wa kudhibiti utoro katika shule na kuacha shule mara moja.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri wa Elimu akisimama atuambie Serikali inafanya mchakato gani wa kubaini watoto ambao waliacha shule miaka kumi iliyopita na kuweza kujua wako wapi leo hii. Bila kufanya hivyo, watoto wengi leo hii wanaoacha shule, wanakwenda kujiunga katika vikundi mbalimbali vya kigaidi. Hii inatuletea shida kwa sababu vijana wetu wengi wanapotea na Serikali haielewi wamekwenda wapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana.