Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Aeshi Khalfan Hilaly

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumbawanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. KHALFAN H. AESHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia Mpango wa Mheshimiwa Dkt. Mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza awali ya yote nataka niliweke Bunge sawa. Wabunge tulioko humu ndani tunatoka maeneo tofauti tofauti. Wako ambao wanatoka maeneo ambapo wanachi wanalima mahindi, karafuu, pamba au korosho. Ni wajibu wa kila Mbunge kuhakikisha anatetea maeneo anakotoka, lakini vilevile kuhakikisha anaitetea Tanzania nzima kwa ujumla kwa jambo analoliona haliko sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana nilisikia hotuba ya Mbunge mmoja akiponda Wabunge wengine wanaotetea maslahi ya wananchi wao. Imetokea na desturi mbaya sana ndani ya Bunge hili, wako watu wanaojifanya wao ni wema sana kuliko wengine, wako watu wanaojifanya wao wako karibu sana na viongozi wa juu kuliko watu wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kauli ya jana ya Mheshimiwa Musukuma kutupinga sisi Wabunge tunaotetea suala la wakulima wa mahindi lilitukera sana sana. Ukilala na mgonjwa utajua matatizo ya mgonjwa, inawezekana Mheshimiwa Musukuma anakotoka hakuna wakulima. Sisi tuna wakulima ambao tunatakiwa tuwatetee kwa nguvu zote, hili limetukera sana. Niwaombe tu Wabunge kama unachangia, changia yale unayoweza wewe kuyasema ndani ya Bunge usiwakere wenzako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye hoja sasa, nimepitia taarifa ya Mheshimiwa Mpango. Katika kurasa zake zote hakuna sehemu aliyomkumbuka mkulima na wenzangu wote wamechangia kuhusiana na kilimo lakini hawa wote waliotoka hapa, wale wote waliochangia suala kubwa linahusiana na kilimo na kilimo ndiyo uti wa mgongo. Asilimia 80 ya wananchi wa Tanzania ni wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo ambayo yanakera sana, Serikali haieleweki nini inafanya. Hili nimwombe Mheshimiwa Waziri Mkuu alisimamie. Serikali inapiga marufuku mazao yetu tusiende kuuza nje lakini haina uwezo wa kuyanunua mahindi yale. Sasa ifike wakati mkulima huyo ambaye anatupa kura nyingi sana sisi, mkulima huyo ambaye anahangaika sana kuhakikisha Taifa hili halipati njaa, basi tumkumbuke na kuhakikisha kama tunazuia mazao yasiende nje, basi tuyanunue, lakini kununua hatununui, kuwaruhusu kuuza nje hatuwaruhusu, matokeo yake tunataka kuzuia mfumuko wa bei kwa kumuumiza mkulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfuko wa kilo tano za mbegu ni Sh.12,500/= lakini leo gunia la mahindi ni Sh.25,000/ = mpaka Sh.30,000/= na mbolea ni Sh.65,000 mpaka Sh.70,000/=. Mkulima ili apate mbegu na mbolea ya heka moja anahitaji auze gunia zaidi ya 10, tunamwonea sana mkulima. Leo hii Mbunge mwenzangu alikuja na hoja akaomba mwongozo lakini kwa bahati mbaya alikosea Kanuni, kesho tutajipanga tena upya ili tuliamshe dude humu ndani, Wabunge tusimame kwa umoja kuhakikisha tunawatetea wakulima na Serikali ije na kauli kwamba kama imeshindwa kununua, basi iwaruhusu kuuza yale mazao yao. Kama tunaongelea Mpango wa Maendeleo na uchumi wa nchi ni lazima tuhakikishe tunamtetea na kumsaidia mkulima ili kilimo kile kiwe na tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuja na kauli mbiu ya Kilimo Kwanza, wananchi wakafurahi sana, wakaunga mkono kauli mbiu hiyo, lakini leo tumekuja na kauli mbiu nyingine mpya ya viwanda. Hata hivyo, bila kilimo viwanda havipo, sasa sijui tunakwenda wapi. Kila nikipitia hii hotuba yote ya Mheshimiwa Mpango inahusiana na kodi tu, tunakusanya kodi, tutakusanya kodi, hao tunaowatoza kodi kila siku wamechoka sasa hivi hawana kiasi chochote cha kulipa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri atusaidie, wako baadhi ya watu wanaoidai Serikali, wako wakandarasi wanaoidai Serikali lakini na Serikali inawadai kodi. Kuna tabia imejitokeza, huyo mfanyabiashara anayedaiwa kodi anazuiliwa biashara zake, anauziwa vitu vyake wakati na yeye upande wa pili anaidai Serikali kwa nini wasikae chini wakapiga hesabu zao na mwisho wa siku kama anaidai Serikali imkate deni moja kwa moja kuliko kumfungia biashara yake na mwisho wa siku anapoteza dira. Sasa kama tunataka uchumi mzuri, basi tuhakikishe na hawa wanaotudai tunawalipa ili waweze kuendelea na biashara zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaongelea uvuvi, katika mtu anayeteseka ni pamoja na mvuvi wa Lake Tanganyika. Mvuvi mmoja ana leseni zaidi ya 10 au 20, mvuvi huyo huyo akitoka Kirando akihamia wilaya nyingine anatakiwa akate leseni mpya, boti hilo hilo moja la uvuvi lina wavuvi 12 kila mvuvi ana leseni na kila mvuvi anailipia. Sasa wavuvi wanahama wanatoka Wilaya ya Nkasi wataenda Wilaya ya Tanganyika, wakitoka Wilaya ya Tanganyika watakwenda Lagosi, kote kule mvuvi analipia leseni.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, unaweza ukamkuta mvuvi ana leseni zaidi ya 100, hivi tunakwenda wapi? Kwa nini tusiweke utaratibu wa mvuvi mmoja kuwa na leseni moja kwa sababu ziwa lile ni letu wote, ziwa ni moja hakuna maziwa mengine pale Lake Tanganyika lakini huyu mvuvi tunamwonea siku hadi siku. Ifike wakati kama tunataka kuinua uchumi wa nchi hii basi na huyu mvuvi aangaliwe kwa jicho lingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimuulize tu Mheshimiwa Waziri wa Fedha, hivi Mheshimiwa Waziri amesomeshwa na mtu gani? Ni mvuvi, mkulima, mfanyabiashara au mtoza kodi? Nataka akija hapa aje anijibu kama alisomeshwa na mkulima lazima awe na uchungu na wakulima, kama alisomeshwa na wavuvi atakuwa na uchungu na uvuvi na hatimaye kwenye Mpango wake humu angewaweka watu hawa akawapa kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina wasiwasi inawezekana labda alisomeshwa na mtoza kodi maana humu ndani ni kodi, kodi; atakamua ng’ombe maziwa na hatimaye atakamua damu. Naomba sana akija kujibu hapa atusaidie, kwanza atuambie kama Serikali haina uwezo wa kununua mahindi iruhusu twende tukauze kokote tunakotaka. Huyu mkulima wanamwonea mno kila wakiamka wao ni kumbana tu lakini siyo wajibu wa mkulima kuhakikisha mwananchi hafi na njaa, ni wajibu wa Serikali kuhakikisha wananchi wake hawafi na njaa, sasa sisi leo ni kumbana tu ooh bwana chakula kimepungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tumeshindwa na Zambia, mahindi yanatoka Zambia yanakwenda Kenya on transit hapa, sisi tumebaki tunatazama tu tunasema kuna njaa, kuna njaa, kuna njaa. Naomba Waziri akija atuambie kama ana uwezo wa kununua mahindi atuambie atanunua mahindi, kama uwezo wa fedha hatuna turuhusu mahindi yaende yakauzwe nje kwa sababu nakumbuka kauli ya Mheshimiwa Rais ambaye sisi wote tunampenda na tunampigania alisema kwamba, mkulima auze mahindi kwa bei yoyote anayotaka, akiuza Sh.100,000/= au Sh.200,000/= sawa ni kama vile mvuvi au mfugaji ambaye hatumuingilii chochote kile kwenye mifugo yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina uchungu sana na mkulima. Juzi Mheshimiwa Waziri wa Kilimo alitudanganya hapa, Waziri huyu ni jeuri sana kwa sababu amesema ameanza kununua mahindi na sasa hivi wametenga shilingi bilioni 40 kuhakikisha mahindi yananunuliwa. Jamani mbona wanasema uongo kila siku? Hakuna hata chembe ya gunia moja lililonunuliwa kutoka Rukwa, Katavi na Mbeya halafu wanakuja kutuambia wametoa fedha za kununua mahindi, hivi kuna Mbunge asiyejua kinachoendelea ndani ya Jimbo lake? Nani? Kila kukicha ukiamka asubuhi meseji unazo kwa hiyo unajua kila kitu kinachoendelea ndani ya Jimbo lako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini leo Waziri wa Kilimo anadanganya kwamba ametoa fedha za kwenda kununua mazao, hakuna fedha yoyote iliyotoka kwenda kununua mazao isipokuwa wamekopa shilingi bilioni mbili kutoka CRDB na hatimaye wamezipeleka Njombe na Songea, sasa kule Sumbawanga ni Tanzania au ni Tanganyika? Kule Katavi ni Tanzania au Zambia? Kwa nini wanakuwa na ubaguzi wa hali ya juu at least wangegawa kidogo kidogo lakini hatimaye mahindi hawanunui, wanawadanganya wananchi, wanakaa wanawabeza wakulima.

Mheshimiwa Spika, kama kungekuwa na uwezo wa kutoka na shilingi hapa ningetoka nayo, lakini kwa Mpango huu kesho tutakuja na ajenda nyingine hapa, tutakuja na Kanuni nyingine mpya ili kuhakikisha kesho Bunge linasimama pamoja kuhakikisha Serikali inatoa kauli ya kununua mazao yale au kuyaruhusu yaweze kutoka nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache, naomba nisubiri majibu ya Mheshimiwa Waziri na baadaye naweza nikaunga mkono hoja au nisiunge mkono hoja. Ahsante.