Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mufindi Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MAHMOUD H. MGIMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu aliyenipa afya nipate nafasi ya kuchangia kwenye ajenda hii muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nichukue fursa hii kumshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Mpango pamoja na Naibu Waziri na wasaidizi wao kwa ujumla kwa kazi kubwa wanayoifanya katika Wizara yao. Lakini namshukuru tena Mheshimiwa Dkt. Mpango, amesema kwenye maandiko yake kwamba atatuzingatia na kuufanyia kazi ushauri wetu. Nakuomba Mheshimiwa Dkt. Mpango, haya tunayozungumza kama Wabunge wenzako uyachukue na kuyafanyia kazi kama ulivyoahidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu unaanza kujielekeza kwenye hali ya kiuchumi. Mheshimiwa Dkt. Mpango amesema uchumi wa Tanzania unakua, ni kweli kwa maelezo yake uchumi wa Tanzania unakua. Lakini unapotaka kuangalia vigezo vya kukua kwa uchumi, lazima tuangalie na hali halisi ya Mtanzania, je, iko sawa, inaenda sambamba na ukuaji wa uchumi anaouzungumza Mheshimiwa Dkt. Mpango? Ukiangalia utaona mambo yako tofauti, tunazungumza uchumi unakua, lakini hali za Watanzania zinaendelea kuwa mbaya siku baada ya siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Dkt. Mpango, kwa hiyo inawezekana vigezo ulivyovitumia kusema uchumi wa Tanzania unakuwa ni tofauti na vile ambavyo tunavifikiria sisi. Kwa mfano, kupata hela ni tatizo, lakini leo hii ukipata pesa unaweza ukashindwa hata kujua umetumia kununua nini, purchasing power inazidi kushuka siku baada ya siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka Mheshimiwa Dkt. Mpango atuambie, tuko kwenye inflation period au deflation period. Kwenye deflation period kama upatikanaji wa pesa unakuwa mgumu, automatically unawasaidia wale waliokuwa na pesa kidogo kuweza kununua vitu vingi katika circulation, lakini mtu anakuwa na hela ndogo aliyoipata, uki-change shilingi 10,000 hata hujui imefanya nini. Kwa hiyo, Mheshimiwa Dkt. Mipango mimi nakuomba uliangalie jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tujiangalie, tupo kwenye depression au tuko kwenye recession period. Hayo mambo yote mawili tunatakiwa tuyaangalie kwa wakati mmoja...
MWENYEKITI: Anaitwa Dkt. Mpango, siyo Dkt. Mipango.
MHE. MAHMOUD H. MGIMWA: Dkt. Mpango, tupo kwenye depression au tuko kwenye recession period, mimi naona kama tunakwenda kwenye depression, tunatoka kwenye recession kwenda kwenye depression. Kwa hiyo ninamuomba sana Mheshimiwa Dkt. Mpango aliangalie jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imejitahidi kwenye suala la bureau de change, lakini bado tuna tatizo kwenye dollarization, bado matumizi ya dollarization yanaendelea kutawala katika nchi hii na shilingi ya Tanzania inaendelea kushuka siku baada ya siku. Sasa unatuambia uchumi unapanda, shilingi inashuka, uki-compare unaona hapa kuna tatizo. Kwa hiyo, vigezo ambavyo Mheshimiwa Dkt. Mpango amevizungumza tunaona haviendani na hali halisi ambayo iko mtaani. Kwa hiyo namuomba sana Mheshimiwa Dkt. Mpango aangalie na haya mambo ambayo yanawahusu Watanzania wa kawaida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika document yake hii ya Mpango mzima hawajazungumzia hali halisi ya wakulima ambao nchi hii asilimia 67 mpaka 72 ni ya wakulima. Kwa hiyo, unakuta mpango mzima wa maendeleo wa nchi hii umewaweka kando wakulima na hawa wakulima ndiyo wanaotuweka hapa madarakani. Kwa hiyo, ninaona hapa kwenye eneo la kilimo kwa ujumla kuna tatizo. Kwa hiyo namuomba sana Mheshimiwa Dkt. Mpango aliangalie na hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tuliahidi kwamba tutatengeneza Kiwanda cha Mbolea hapa nchini kule Mtwara lakini mpaka leo kiwanda hicho hakijatengenezwa. Kingeweza kutengenezwa kiwanda kile cha mbolea kule Mtwara nina uhakika mbolea ingekuwa chini kuliko ilivyo sasa hivi. Tulikuwa tumekwenda kwenye mpango wa bulk procurement, bei imeshuka kidogo, lakini tungekuwa tumetengeneza kiwanda chetu hapa nchini bei ingekuwa chini zaidi na nina uhakika kwamba haya ambayo wakulima na Wabunge wengi tunalalamikia yasingekuwa kama ilivyo sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano tunajiuliza, kwa nini wenzetu wa Zambia wanauza gunia la mahindi shilingi 20,000 kwa nini sisi tunauza shilingi 35,000? Kwa hiyo tuna maana kwamba mbolea kule iko cheap zaidi kuliko kwetu, lakini sisi tuna access ya kutengeneza mbolea hapa ndani ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hata ule uchumi wa viwanda ambao ndugu yangu, Mheshimiwa Jafo, anauzungumzia sana, tunaomba uliangalie eneo hili sensitive la wakulima kwamba kile kiwanda cha mbolea tulichokizungumzia ambayo raw material tunayo ya kutosha kule Mtwara kingeanza as soon as possible tuwasaidie wakulima walio wengi katika eneo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi namuomba sana Waziri wa Fedha atakapokuja atuambie kile kiwanda ambacho tumekivumilia miaka mingi kwa nini mpaka leo hakijaanzishwa na sababu zipi zinazopelekea kutokuanzishwa kwake. Sasa matokeo yake ni kwamba kila siku tunakuja na miradi mipya ambayo haina tija. Unaanza mradi wa zamani to a level fulani unafika unauacha unakuja kwenye mradi mpya. Kwa hiyo hapa ni tatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumzia suala la mahindi, na mimi nataka ni- declare interest, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Kilimo. Kwenye kilimo tumelizungumzia na bahati nzuri leo Mheshimiwa Waziri amelizungumza na baadhi ya Wabunge wanaotoka kwenye maeneo hayo. Kamati yetu tulikaa na Mheshimiwa Waziri siku tatu kuzungumzia tatizo la mahindi, tumbaku na mbaazi na tukatoa directive kwamba Mheshimiwa Waziri aje hapa kwenye Bunge lako Tukufu aeleze mkakati wa Serikali kuhusu mahindi yatauzwaje, mbaazi itauzwaje na tumbaku itauzwaje, lakini amekaa kimya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na sisi Wajumbe wa Kamati tulikuwa tunategemea yale ambayo yanaulizwa na Waheshimiwa Wabunge yangekuwa yameshazungumzwa hapa Bungeni kabla na Wabunge wakatoa maazimio ya pamoja. Kwa hiyo, wakulima wetu wanakwenda mwezi wa 11 wanaanza kupanda mahindi, hawajui nini wafanye hata kama tumekubaliana leo kwamba tunataka kufungua masoko, bado ni tatizo. Aje hapa kwenye Bunge lako Tukufu atoe tamko la Serikali kwamba kuanzia leo watu wauze mahindi yao popote wanapotaka ili waweze kupata haki zao za msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme, kama nilivyosema hapo awali, kila siku Serikali ina mawazo mapya. Tulikuwa tunategemea tutatengeneza umeme kwa kutumia makaa ya mawe, wenzetu wa Mchuchuma, Ngaka, Kiwira. Lakini mpango huu upo zaidi ya miaka 30, sasa tukijiuliza kwa nini tunaenda kwenye mipango mingine wakati mpango huu ambao ulikuwa umeshaanza tumeuacha. Kwa hiyo unakuta hata baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wakisema kuna baadhi ya miradi imekuwa biased, watu wanaamua kwenda kwenye miradi mingine wanaacha miradi mingine, hili litatuletea matatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri atuambie kwa nini wameamua kuacha mradi wa umeme. Sweden kuputia Kampuni yao SIDA Grand walikubali kutoa hela, dola milioni 60, kwa ajili ya kusaidia kutengeneza transmission line ya kutoka Makambako mpaka Ngaka, lakini Serikali imekaa kimya. Na tatizo la pale ni transmission line tu na umeme ule ni cheaper kuliko umeme mwingine wowote. Kwa hiyo, tunataka kwenda kwenye vyanzo vingine vya umeme wakati tulikuwa tunaweza kupata umeme wa rahisi ambao Serikali ilikuwa haiingizi hela yoyote kama alivyosema Mheshimiwa Nape pale, kwa nini twende kuingiza hela kwenye miradi ambayo haina tija katika nchi hii?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi naomba tuangalie na mje na majibu kwa nini mradi wa umeme wa Ngaka mpaka sasa hivi haujaanza kazi. Kwa nini mradi wa uchimbaji wa chuma mpaka sasa hivi haujaanza kazi kule Liganga. Hii inakatisha tamaa sana, tunaona kwamba kuna baadhi ya maeneo wanapewa priority ya hali ya juu na kuna baadhi ya maeneo hawapewi kitu chochote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukija kwenye maeneo ya barabara, tunatakiwa tuendelee kufungua barabara. Kuna barabara ya kutoka Kinyanambo A kwenda Isalavanu, Madibira mpaka Rujewa, ni barabara imezungumzwa karibu katika awamu tano. Toka mwaka 2000 ile barabara inazungumzwa, na ni barabara muhimu sana kiuchumi. Kwa watu wanaotoka Mbeya wakiamua kukatisha kwenye barabara ile wanapunguza zaidi ya kilometa 75 kuliko wakipita barabara ile ya kupitia Makambako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwenye uchumi hili ni jambo zuri sana. Lakini kila siku wanasema tutaanza kesho au kesho kutwa, lakini ukianglia katika mpango wake na ile barabara is very sensitive, inapitia kwenye mbuga za wanyama, inapitia kwenye maeneo ya kilimo kikubwa cha mpunga, inapitia kwenye kilimo kikubwa cha mahindi, inapitia kwenye maeneo ya madini, wameiacha haijaanza kushughulikiwa. Kwa hiyo kuna walakini hapa.
La pili, unakuta barabara ya kutoka Mafinga kwenda Mtiri mpaka Mgololo. Barabara ile ina zaidi ya viwanda vikubwa kumi ambavyo vinatoa kodi zaidi ya shilingi bilioni 50 lakini Serikali haitaki kuijenga kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, hili ni tatizo; watu ambao wanachangia hela nyingi kwenye nchi hii wanasahaulika. Kwa hiyo, mimi namuomba sana Mheshimiwa Waziri mipango yake awe anaangalia na watu wana-contribute nini katika Taifa hili, sio ajielekeze kwenye maeneo tu ambayo anayaona yeye. Watu wanachangia hela nyingi kwenye Mpango wa Taifa lakini matokeo yake ni kwamba hatupeleki kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefanikiwa kwenye eneo la umeme lakini bado kwenye eneo la maji. Mheshimiwa Waziri amezungumzia eneo la maji Dar es Salaam tu, ina maana watu wa Tanzania wengi wanakaa Dar es Salaam. Katika Mpango wake mzima ameonesha kwamba maji yanatakiwa yaende kwa wingi katika Mkoa wa Dar es Salaam, kwa nini kwenye Mikoa, Wilaya, Vijiji na Majimbo mengine yasiende? Kwa hiyo kama tulivyofanya kwenye maazimio ya Bunge lililopita kwamba tuli-ringfence kwa ajili ya kupata umeme wa uhakika, sasa hivi nguvu zetu zielekezwa kwenye eneo la maji ili maji yapatikane katika maeneo mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kwenye Kamati yetu tumependekeza hata Bunge lililopita tuongeze shilingi 50 kwenye kila lita ya mafuta ili maji yaende kwenye maeneo yaliyokuwa mengi, lakini tukikwambia utasema kwamba tutaongeza inflation rate, hatuwezi kuongeza inflation rate kwa utaratibu huo. Kwa sababu sisi kama Wabunge tumekubali na tutakuwa tayari kwenda kutetea hoja zetu, kwamba tuna sababu za msingi za kuongeza shilingi 50 kwenye maji ili maji yaende kwenye maeneo mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.