Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Naghenjwa Livingstone Kaboyoka

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa jina naitwa Naghenjwa au wale waliozoea wananiita Naghe Livingstone Kaboyoka, Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kupatiwa nafasi hii kutoa mawazo au maoni yangu machache kutokana na hotuba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Kwanza kabisa niseme kwamba Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi tunamfurahia kwa approach yake ya kwanza aliyoifanya alipokutanisha wafugaji wa Wilaya ya Same na Jimbo la Mlalo na wa kutoka sehemu zingine za Mkoa wa Tanga, akakaa na wafugaji, akaongea nao vizuri takribani wiki tatu, nne zilizopita. Amevunja rekodi na wafugaji wale walifurahi sana kwa mara ya kwanza kuweza kukutana na Waziri na kueleza matatizo yao na Waziri akawasikiliza na akaahidi kufuatilia na kuwapa ushirikiano mkubwa. Sioni kama kuna ubaya wa kumsifu mtu ambaye amefanya kitu kizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kifupi nataka tu niseme machache maana mengi yamesemwa katika Kambi ya Upinzani ambayo yalikuwa katika yale niliyotaka niyaulizie. Kwa uchache huo ninalotaka kuuliza ni kwamba naomba Waziri ajaribu kunieleza kwa vile Serikali yetu inaangalia kukuza viwanda na ninaamini kwamba sustainability ya viwanda inatokana na malighafi ya ndani ya nchi. Je, kumekuwa na mawasiliano na Wizara ya Viwanda kuona jinsi ambavyo viwanda vile vitakavyotumia malighafi, yale maeneo yatakayotoa malighafi wale wakulima wanasaidiwa ili kuwe na mikataba maalum ya kuonyesha kwamba watatoa mazao yatakayoweza kufaa katika viwanda vile ili viwanda vyetu viweze kuboreshwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nauliza hivyo kwa mfano, nikianza na viwanda vya ngozi, kwanza tunaona kiwanda kile cha Kawe kilikufa hatujui kama kuna mpango wa kukifufua ama vipi lakini wafugaji wameshaandaliwa ili waweze kufuga ng‟ombe wazuri watakaotoa ngozi nzuri itakayotumika katika viwanda vyetu? Maana kama hakuna uwiano au mahusiano ya kupanga mikakati kati ya Wizara hii na Wizara ya Viwanda sioni jinsi ambavyo viwanda vyetu vitafanikiwa kama Wizara ya Kilimo na Mifugo haikufanikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kadhalika upande wa mazao yale kama pamba, kama tunataka kuanzisha viwanda vya nguo, je, wakulima wa pamba wameangaliwa jinsi ya kusaidiwa kwanza kulima, kuhifadhi na kusafirisha mazao yale kwenda kwenye viwanda? Tumeshuhudia viwanda vya Mwatex, Kilitex, Urafiki vyote vikifa au vikisuasua na sasa tunataka kuanzisha viwanda ambavyo sijui kama vinaangalia hayo yote. Maana wenzangu wachumi watanisahihisha kwamba lazima tuwe na backward na forward linkages otherwise kila Wizara ikifanya kitu chake parallel hakika lengo hili halitafikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, for example nimeona Kambi Rasmi wakitoa maelezo kwamba ukame umeathiri upatikanaji wa mazao kipindi kilichopita. Je, Wizara ya Maji inahusishwa katika sehemu ile itakayowekwa viwanda ili maji yapelekwe kwenye zile malighafi tusitegemee kilimo cha mvua? Wenzetu wa Israel wanatumia sana teknolojia ya drip ambayo inatumia maji kidogo sana lakini inahakikisha mazao yao yanakuwa bora sana. Je, Wizara ya Kilimo ina mpango wa kuongea na Wizara ya Maji ili wawekewe maji kule ambako wanataka kuboresha mazao yale ili system ya drip angalau ifanyiwe utafiti na sample kama kutengeneza model ya shamba ambalo linatumia drip na kuona wale ambao hawatumii system hii na wale wanaotumia nani ambao wanapata mazao zaidi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana kabisa kwamba Wizara hii ni nyeti na kubwa sana ambapo Watanzania wengi wanaitegemea. Tunaamini kwamba hata wale wanaojiita mabaunsa bila chakula hawawezi kuwa mabaunsa, kwa maana hiyo njaa haina baunsa. Kwa hiyo, naamini kwamba Wizara hii itaongezewa fedha ili kusudi iweze kufanya vizuri na itatoa mchango mkubwa ambao utakuwa input katika Wizara zetu nyingine kama zile za Afya na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia kwamba muda si rafiki, napenda tu nijue kuhusu kiwanda cha tangawizi kule kwenye Jimbo letu la Same Mashariki ambacho kimekuwa hakianzi kufanya kazi pamoja na Rais wa Awamu iliyopita kwenda kukifungua mwaka 2012. Matokeo yake wakulima wengi wa tangawizi ambao waliongeza sana kilimo cha tangawizi wamepata hasara kubwa sana na kule sasa hivi tuna makaburi mengi ya tangawizi kuliko ya wananchi waliofariki kutokana na kwamba wakulima hawakuwa na jinsi bali kuzika zile tangawizi zao. Sasa tunapowaeleza wakulima waongeze kilimo wakati hatujui jinsi ambavyo viwanda vyetu vitawahudumia hatuoni ni kuwasumbua wakulima bure?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nataka nimuulize Mheshimiwa Waziri, ana habari kwamba Rais wa Kenya ameruhusu kilimo cha mirungi na kutenga dola za Kimarekani milioni mbili ili kilimo hiki kikuzwe. Tukizingatia kwamba tuko katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, je, pamoja na kwamba sisi tumezuia kilimo hiki tunahakikishaje mirungi hii haitaingia kwetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nafikiri ni vizuri Waziri wa Kilimo akawasiliana na wenzake Kenya kuona kwa nini wao wameruhusu zao hili. Naamini kwa vile wamejua lina faida sana na ni rahisi kuzuia madhara kama ukiruhusu zao hili kuliko ukilikataza halafu watu walime kwa kificho, watalitumia vibaya zaidi. Tuna mfano wa nchi ya Holland waliidhinisha maduka fulani kuuza dawa hizi za kulevya kwa kuamini kwamba wale watumiaji watatumia kidogo kidogo kuliko wakificha halafu watumie kwa wingi kwa wakati mmoja madhara yake yanakuwa makubwa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme hivi, namshukuru Waziri wetu kwa mikakati hii mizuri lakini pia azingatie maoni ya upinzani maana yatamsaidia kuboresha kilimo, ufugaji na uvuvi ambao ni tegemeo kubwa sana la nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka pia nijue, je, Waziri wetu wa Kilimo ana mahusiano gani kupitia labda Wizara ya Viwanda na hili Shirika letu la World Trade Organisation kuona kwamba na sisi masoko yetu yanafiki katika kiwango kizuri cha juu na tukapata upanuzi wa masoko nchi za nje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda nisisitizie upande wa uvuvi, hizi neti ambazo ni ndogo na zinaharibiwa kila wakati, kwa nini ziruhusiwe kuwa nchini kama zinaleta madhara makubwa? Nafikiri Wizara waangalie na kuona kwamba neti hizi zisiruhusiwe ili tusitie wavuvi wetu hasara ya kuwachomea neti walizozinunua kwa gharama kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.