Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Omari Mohamed Kigua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kuchangia Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka wa fedha 2018/2019 katika maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu miradi ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi, eneo hili ni muhimu ambalo Serikali ililipa umuhimu mkubwa sana. Ili Serikali ijipunguzie mzigo wa kubeba miradi mingi mikubwa ambayo yote ina dhamira ya kuliletea Taifa maendeleo, mimi sioni sababu kwa nini Serikali isichukulie mradi wa Daraja la Kigamboni na Mradi wa Mabasi ya Mwendo Kasi Dar es Salaam kama kielelezo cha mfano. Tatizo lipo wapi? Inaonekana wazi kuna hofu katika eneo hili ambayo haina msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo mifano duniani ambako nchi nyingi zimepiga hatua kupitia utaratibu huu. Naomba Serikali iwekeze katika sekta ya barabara, hospitali, kilimo, usafiri wa anga, reli pamoja na usafiri wa maji kupitia public private partnership (PPP) hii njia pekee itafanya nchi isonge mbele, kwani nchi yote ni kubwa na kila mkoa, wilaya na jimbo ina changamoto tofauti, tusipochukua hatua itachukua miaka kama si karne kutimiza matarajio ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu sekta ya kilimo, mifugo, uvuvi, wanyamapori na misitu, hili pia ni eneo ambalo Serikali anabidi kuweka msisistizo ili kufanya nchi iongeze Pato la Taifa. Yapo maeneo mengi ambayo yana fursa, kama yangetumika vema basi uchumi ungeongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengi ya nchi yetu hasa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini yanalima sana mahindi. Hivi ni lini Serikali itatoa utaratibu wa kuhakikisha kuwa eneo hili linakuwa eneo maalum kwa ajili ya uzalishaji wa mazao ya mahindi ili nchi izalishe kwa ajili ya ndani, pia ili tuweze kuuza nje ya nchi? Hili linawezekana tukiweka utaratibu wa kulima kwa njia ya kisasa. Wananchi wa maeneo haya kupata pembejeo za kisasa, mikopo ya riba nafuu na kupatiwa ruzuku kama nchi nyingine duniani wanavyofanya. Hii pia itafanikiwa katika sekta nyingine za mifugo, uvuvi, wanyamapori na mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu bomba la mafuta kutoka Hoima (Uganda)- Chongoleani (Tanga), niipongeze Serikali kwa mradi huu mkubwa ambao utatoa fursa kubwa ya kiuchumi katika nchi na hasa katika mkoa wetu wa Tanga ambapo bomba la mafuta litapita katika Wilaya nyingi ikiwemo Wilaya ya Kilidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona Serikali itatengeneza barabara ya kiwango cha lami kutoka Handeni hadi Singida ambapo barabara hii itapita. Jambo hili ni zuri sana na niipongeze Serikali. Ni dhahiri kwa ukubwa wa mradi huu na thamani si busara eneo la bomba linapopata kuwa na barabara mbovu. Niiombe Serikali itenge fedha kwa mwaka wa fedha 2018/2019 ili ijenge barabara hii kama ilivyokusudia. Aidha, barabara hii ni kiungo muhimu cha mikoa minne ya Tanga, Manyara, Dodoma na Singida na zipo shughuli nyingi tu za kiuchumi kwa barabara hii. Wakati muafaka umefika kujenga barabara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA), uanzishaji wa Wakala wa Barabara ya Vijijini utasaidia kufungua mawasiliano ya barabara za vijiji vyote; hii itasaidia sana kutimiza uchumi wa wananchi wote. Ni wazi maeneo mengi ya nchi yetu hususan barabara za vijiji vyote bado yana changamoto za kutopitika. Niishauri Serikali iimarishe Wakala wa TARURA kwa kupatiwa wataalam wa kutosha na iongeze ujuzi wa kutosha hasa katika barabara hizi, hii itasaidia sana kuunganisha barabara za vijiji na barabara kuu. Aidha, wakala huyu wapatiwe vitendea kazi vya kutosha vinginevyo utendaji utazorota.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.