Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

Hon. Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda sana kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetupa nguvu na uzima kwa kuweza kuhakikisha tunachangia mchango huu. Nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kunipa dhamana na kuniamini kuweza kuhudumu tena katika ofisi yake nikiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Rais kwamba sitamuangusha na nitazidi kumuomba Mwenyezi Mungu siku zote aweze kunipa nguvu na uzima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sana kumshukuru kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango na dada yangu, Naibu Waziri, kwanza kwa kazi kubwa wanayofanya. Leo hii tunajadili Mpango, lakini mimi katika ofisi ninayoiongoza naomba kutoa shukrani za dhati sana kwa Wizara ya Fedha kwa kazi kubwa inayofanya na nishukuru kwa sababu imeendelea kuiwezesha ofisi yangu kwa kipindi chote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mjadala huu wa Mpango wetu, kikubwa zaidi ni kuangalia jinsi gani tutamwezesha mwananchi wa kawaida kuweza kukuza uchumi wake. Mpango wetu wa Taifa unaeleza dhahiri kabisa kuhusu chombo ambacho kiko katika ofisi yangu, tumekianzisha mwaka huu kiitwacho TARURA. Malengo yetu ni kwamba ikifika mwaka 2020 tuwe na mabadiliko makubwa sana katika suala zima la miundombinu ambayo hiyo itawawezesha wananchi kukuza uchumi wao kupitia malighafi au mazao yanayozalishwa katika maeneo yao. Nishukuru ofisi hii kwa jinsi ilivyojipanga kwa sababu katika mwaka huu wa fedha peke yake takribani shilingi bilioni 573 tutazielekeza katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa bila kuwa na mipango mizuri, mambo hayo hayawezi yakafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kwa kiwango kikubwa, nikijielekeza katika sekta ya elimu ambayo nimesikitika sana kwa sababu nimeona baadhi ya Wabunge wenzetu humu ndani wengine wakibeza jambo hili kubwa sana lililoanzishwa na Serikali ya Awamu ya Tano la kuwawezesha Watanzania masikini kwa kuwa na programu ya elimu ambayo inagharamiwa na Serikali, lakini wengine walikuwa wakisema maneno ya kebehi kabisa kama hakuna chochote kilichofanyika. Kwa kweli, kwa dhati kabisa naweza kusema hii si haki hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia katika chain yetu hii tunavyozungumza hivi sasa, tujipime sisi tuko humu ndani ya mamlaka Mwenyezi Mungu ametupa fursa tumeingia humu Bungeni, lakini tuwaangalie Watanzania hao wadogo-wadogo ambao hali yao ni tete, ni taabani, hata ile gharama ya kulipia certificate ya form four wengine walikuwa wanashindwa. Leo hii programu ya elimu bure ambayo takribani shilingi bilioni 18.77 zimekuwa zinatoka, sasa hivi takribani shilingi bilioni 23 kila mwezi zinatoka, halafu kama Mbunge anasimama humu ndani anabeza kabisa kwamba hakuna lolote, nadhani tuna sababu ya kufanyiwa tathmini sisi wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, angalia kazi kubwa iliyofanyika. Ninyi mnafahamu kipindi kirefu tumesema shule zetu za Serikali hazifanyi vizuri, leo hii Wizara ya Fedha na Wizara ya Elimu kwa ujumla wetu katika suala zima la uwekezaji mkubwa tunaofanya katika sekta ya elimu, shule kongwe takribani 89 zote tunaziboresha ziweze kutoa mazingira ya ushindani. Mpaka sasa tunaenda takribani shule 43 ambazo hali yake ilikuwa ni hoi bin taabani. Shule hizi tunabadilisha miundombinu yake lengo kubwa iwe ni miundombinu wezeshi. Katika Mpango huu unaokuja tunaangalia ni jinsi gani tunaenda kukamilisha shule hizi nyingine tupate shule 89 ambazo zitakuwa na level ya kisasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe Waheshimiwa Wabunge, wakati mwingine tupate fursa tutembelee mazingira yetu kuangalia tulipoanzia na wapi tunakokwenda. Nendeni Mpwapwa, Msalato, Mzumbe kwenye hizi shule ambazo Serikali imefanya investiment kubwa ya fedha za Serikali karibu shilingi bilioni moja kila shule. Mimi nimewaambia wazi kwamba lengo letu ni kuhakikisha elimu yetu inarudi katika mstari unaokubalika na haiwezi kurudi bila kuweka mipango na mipango yenyewe ndiyo hii inayojadiliwa humu ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme bahati nzuri Mheshimiwa Mwenyekiti wewe unafahamu shule yetu ya Mpwapwa zamani ilikuwa imechoka kabisa, leo hii ukifika Mpwapwa unashangaa hii shule ya aina gani! Nenda Msalato hapa watoto walikuwa wakifika shuleni wiki moja mtoto anatamani aende nyumbani. Tumeenda na Kamati ya Bunge kutembelea tumekuta watoto 580 wamekataa kwenda likizo wote wame-register kwamba watabaki shuleni kwa sababu wanasema sasa hivi tumekaa shule kama tuko katika hoteli. Hii yote ni investiment kubwa inayofanywa na Serikali. Leo Mheshimiwa Mpango amekuja na Mpango wa jinsi ya kuboresha ili suala la elimu liende mbele zaidi. Naomba niseme wazi, tuwe wazalendo katika kuangalia jinsi gani tunafanya nchi yetu iende mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimesikia na bahati nzuri dada yangu Mheshimiwa Ummy Mwalimu, alizungumza katika suala zima la sekta ya afya, kumbukeni huko tulikotoka na sasa hivi tukoje. Ukiachia bajeti ya dawa Mheshimiwa Ummy amezungumza, lakini ajenda ya miundombinu, ninyi wenyewe mnafahamu huko tulikotoka leo hii kupitia fedha za World Bank, fedha za ndani na fedha kutoka Canada tunafanya investment kubwa katika nchi hii kwa mara ya kwanza haijawahi kutokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni tumepata karibu shilingi bilioni 10 fedha za ziada kutokana na mipango mizuri ya Serikali, mpaka donors countries wanaridhika na utendaji wa Serikali ya Tanzania. Hivi sasa tuna-scale up hiyo programu, tunaenda karibu vituo 216 kutoka 172, hii ni kazi kubwa inayofanyika, lakini kazi hii maana yake ni jinsi gani Serikali imejipanga kutekelza majukumu yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba mimi nimpongeze Mheshimiwa Mpango, ndugu yangu usikate tamaa. Wakati mwingine safari yoyote ukiona unapigiwa kelele ujue kwamba safari hiyo inaenda vizuri, chapa kazi kaka na sisi tuko nyuma yako tunaenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaambie Watanzania, Mpango wetu katika suala zima la miundombinu, bahati nzuri juzi-juzi tulikuwa kule Mwanza World Bank wanatusaidia suala zima la uboreshaji wa miji hii Tanzania. Ukienda Mbeya, Tanga, Arusha na miji yote mikuu tumefanya mabadiliko makubwa, lakini Manispaa zetu tunafanya uwekezaji mkubwa wa kujenga barabara za lami, kuweka taa na kujenga madampo ya kisasa. Mpango huu unaokuja sasa hivi unaangalia ni jinsi gani tunaenda ku-scale up hiyo programu yetu ili kuhakikisha Miji, Halmashauri na maeneo mbalimbali yanaimarika katika miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo yote ni kutokana na sera nzuri ya Serikali inavyofanya resource mobilization na wadau wetu wanaridhika kwamba kazi zinakwenda. Juzi tukiwa Mwanza, World Bank imetoa extension ya mradi wetu wa UGLSP, badala ya kuishia mwaka 2018 sasa wame-extend mpaka 2020, hii ni faraja kubwa kwa Serikali ya Tanzania. (Makofi)

Kwa hiyo, jukumu letu kubwa ni lazima tuwe wazalendo tuone tulikotoka, tulipo na tunakokwenda. Kweli, unaweza ukatoa mawazo lakini siyo kukashifu kwamba hakuna jambo linalofanyika. Ingekuwa nchi nyingine kama Wabunge tungesema wapi kuna gap kidogo turekebishe twende mbele zaidi, lakini sio kukashifu kama hakuna kinachopatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri nimesikia Wabunge wengine walikuwa wakibeza hata suala zima la uchumi wa viwanda. Nimshukuru sana kaka yangu Mheshimiwa Mwijage amefanya kazi kubwa sana na mimi ni Wizara wezeshi ya kumwezesha kaka yangu Mheshimiwa Mwijage instrument yake ifanyike vizuri. Leo hii Mheshimiwa Mwijage na Rais anahangaika ili tuhakikishe tunajenga viwanda ili watoto waweze kupata ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana mimi nikiwa mwenye mamlaka na Serikali za Mitaa, juzi juzi wakati tunawaapisha Wakuu wa Mikoa niliwapa target nikasema Mheshimiwa Mwijage anahangaika na viwanda, lazima kama Wakuu wa Mikoa, leo katika bajeti yetu ya mwaka wa fedha 2017/2018, bajeti ya own source ni karibu shilingi bilioni
61.5. A unit plants ya kiwanda cha kawaida cha kubangua korosho, ukienda Newala, Masasi, ukienda SIDO wanakupatia kiwanda cha shilingi milioni 10. Kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti hapa Singida, uliza zile mashine SIDO zinauzwa kiasi gani, average ni kati ya shilingi milioni mbili na nusu mpaka milioni sita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, own source yangu ambayo ipo katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa, shilingi bilioni 61, hata kama unit plants ya kiwanda kidogo ukiweka shilingi milioni 10 ni sawasawa na viwanda 6,100, ni beyond expectation ya viwanda 2,600 kwa mwaka. Hivi vitu ni just calculation, is just about numbers. Kwa hiyo, sisi kama Wabunge wetu lengo letu kubwa ni jinsi gani tuna-play ile leadership position, katika mamlaka zetu jinsi gani tutafanya sasa kuhakikisha tunaweka uwekezaji mkubwa tunaboresha viwanda vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Waziri wa Viwanda na Biashara, juzi wakati tunazindua operation ya viwanda 100, Naibu Waziri pale alitoa sera pana sana ya viwanda. Bahati nzuri mama mwenye Mifuko ya Uwezeshaji, dada yangu Mheshimiwa Jenista Mhagama, ana mifuko 17, tumetoa fursa jinsi gani tutafanya kama Watanzania kwa ajenda ya viwanda ambayo ipo, tukiungana kwa pamoja tunatoka. Tatizo kubwa kuna watu wengine hawataki hili jambo lifanikiwe kwa sababu watasema kuwa Ilani ya Chama cha Mapinduzi imefanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba niwaambie tunaenda kushinda ushindi mkubwa kwa mafanikio makubwa. Kikubwa zaidi kaka yangu Mheshimiwa Mpango chukua yale maoni mazuri ya Wajumbe humu, tuyaweke vizuri tuone jinsi gani tutasonga mbele Mpango wetu uive vizuri. Nikuhakikishie, kwa Mpango huu na juhudi ya Serikali inavyokwenda na naomba niwahakikishie Wizara zote ambapo Wizara yangu ndiyo inakumbatia mambo mengine yote, Wizara wezeshi, tutashirikiana kwa kadri iwezekananavyo Mpango huu na mambo mengine yaende vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, matamanio yangu makubwa wafike watu nchi jirani waje Tanzania kuja kujifunza kupitia kwetu. Kuna watu wengine wanaona kwamba eti kufanya ufahari kwamba lazima uende kwenye kujifunza, hapana tufike muda Tanzania lazima tuache legacy nchi yetu. Leo hii tumepata mfano katika mradi wetu wa DART unaoendelea Dar es Salaam tumeshinda katika majiji duniani. Mwezi wa pili tunaenda New York, Marekani kuchukua tuzo maalum ni Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoenda katika suala zima la utengenezaji wa barabara za mwendo kasi awamu sita tumemaliza awamu moja lakini awamu hizo zote ndizo ziko ndani ya Mpango ambao leo hii ndiyo Mheshimiwa Mpango anau-submit hapa. Si muda mrefu sana tunaenda kuhakikisha tunatekeleza mradi wa barabara ya Kilwa - Mbagala - Gongo la Mboto. Lengo ni kulifanya Jiji letu la Dar es Salaam na maeneo mengine yawe rafiki kwa ajili ya suala zima la kujenga uchumi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Tanzania tumepata ufahari mkubwa, takribani nchi sita na wengine mpaka leo wanazidi kuomba kupitia kwetu TAMISEMI waje Tanzania kujifunza mipango mizuri ya utekelezaji wa miradi yetu. Haya yote yanataka sisi Wabunge ambao ni decision makers ambao tunawawakilisha wananchi hapa tufanye maamuzi mazuri, tushirikiane na Serikali, pale penye upungufu tuboreshe vizuri zaidi nini tufanye ili tuifikishe nchi yetu mahali salama ambapo Watanzania watajivunia kwamba wamepata viongozi ambao wako humu na wamekuja kufanya maamuzi sahihi kwa ajili ya maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika haya yote naomba niseme wazi kwamba tunaenda vizuri. Kikubwa zaidi tutaboresha kwa michango mizuri ya Waheshimiwa Wabunge ndiyo maana ya Bunge lazima Wabunge watoe maoni, maoni yale yakikusanywa tunatengeneza Mpango mzuri lakini Mheshimiwa Mwenyekiti naomba nikuhakikishie kwamba Tanzania ikifika mwaka 2020 kuna watu mpaka wengine wataogopa kugombea humu ndani. Wasipoogopa kugombea basi lazima wata-join na watu ambao wana uhakika wa kushinda, election is not a numbers. Kama
tunaenda katika utaratibu huu mzuri naomba niwaambie hakuna mashaka lazima tutafika mahali muafaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haya niliyoyazungumza, naomba niseme wazi kwamba kama Wabunge tuungane kwa pamoja, tujenge uzalendo wa nchi yetu, tuhakikishe jinsi gani tunafanya na tuweke maslahi ya wananchi mbele. Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania, ubariki Mpango huu, naunga mkono hoja.