Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Magomeni
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JAMAL KASSIM ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ya Kamati ya PAC. Nianze moja kwa moja nami kujielekeza katika masuala manne kama muda utatosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kwanza ambalo nimekusudia kulichangia leo hii jioni ni suala la NSSF. Bahati nzuri Kamati yetu ya PAC tulibahatika kuonana na uongozi wa NSSF, tukabahatika kukagua hesabu zilizokaguliwa za NSSF. Kumekuwa na hoja potofu ambayo baadhi wa Wajumbe wamezungumza na imekuwa inazungumzwa. Nimewanukuu Mheshimiwa Mussa Mbarouk, nimemnukuu Mheshimiwa Catherine Ruge katika michango yao wamesema kwamba kwenye suala la mradi wa Dege, NSSF imenunua ardhi heka moja kwa thamani ya Sh.800,000,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwape challenge, nimepitia hesabu na wao tumepitia pamoja, ukipitia taarifa ya ukaguzi ya CAG, kile kitabu kina kurasa karibia 200 na kitu, hakuna hata sentensi moja iliyoandika kwamba NSSF wamenunua ardhi kwa shilingi milioni 800. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukipitia taarifa za hesabu za NSSF, ukiangalia financial statements zake, hakuna sehemu yoyote ambayo NSSF wameripoti au kurekodi kwamba kuna pesa au miamala ambayo wamefanya ya ununuzi wa ardhi kwa hekari moja shilingi milioni 800. Kwa hiyo, nawaomba wasipotoshe, kama wana ushahidi waulete na nipo tayari hata kujiuzulu Ubunge wangu katika hili. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge waelewe nini hasa kinachoendelea katika mradi wa Dege. Mradi wa Dege ni miongoni mwa miradi ambayo inaendeshwa kwa mfumo wa land for equity na mradi huu sio umeingiwa mara ya kwanza na NSSF, miradi hii imefanywa na National Housing na taasisi mbalimbali za umma na za binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la Dege, mradi wa Dege ni mradi wa ubia baina ya NSSF na Kampuni ya Azimio Limited ambayo imesajiliwa Tanzania. Hawa wawili ndio wabia wa mradi huo. Katika modality ya miradi hii, katika soko yule ambaye anakuja na ardhi kawaida ana- carry an interest of 20 percent ya ule mradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waheshimiwa Wabunge wajue, ukienda Arusha kuna Palace Hotel, ile property ardhi ni ya National Housing waliingia ubia na mwekezaji Palace Hotel Limited, National Housing ina asilimia 20 na Palace Hotel Limited ina asilimia 80. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, isitoshe ukienda Morogoro leo kuna stand kuu ya mabasi eneo lile ni la Manispaa ya Morogoro, NSSF wamewekeza pale, Manispaa ya Morogoro kwa vile ardhi ni yao wame-carry an interest ya ule mradi ya asilimia 23 na NSSF wamebakizwa asilimia 77. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wajue, hiyo hoja ni hoja potofu na sijui waliokuja nayo wana malengo gani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile hili suala lilianza kwenye taarifa ya CAG ya mwaka 2014/2015 ambayo bahati nzuri mwaka jana tuliichambua na tukabahatika kutoa mapendekezo, niwapongeze Serikali kwa hatua mbalimbali ambazo wamezichukua, lakini kubwa niwaombe mradi ule NSSF imeingiza takribani bilioni 219, pesa hizi ni pesa za wanachama wananchi wa Tanzania ambao Serikali yetu hii ndiyo trustee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe sana mradi ule ukiendelea kukaa vile ulivyo, hauna tija kwa Taifa letu. Tumewekeza pesa nyingi, ipo haja sasa ya ule mradi kuhakikisha unatoka pale na unaenda kwenye level nyingine ambayo tumekusudia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naitaka Serikali ikae na mbia ambaye Azimio Housing Limited kuhakikisha yale makubaliano ambayo yameanza basi yanafikia tamati mapema na ule mradi unaendelea na kuleta tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulivyoenda NSSF Dege bahati nzuri wenzetu Management team ya NSSF walitueleza mipango mizuri kabisa juu ya huu mradi. Kwanza, walituambia zile nyumba kwa bei ya mwanzo kabisa zitauzwa kwa takribani dola 120,000 na wametoa fursa kwamba Watanzania na mwananchi yeyote anaweza kununua nyumba ile kwa muda wa miaka 15 bila kupitia benki. Kwa hiyo, hii ni fursa pekee ambayo makampuni yote yanayo-deal na property business hakuna hata moja inayofanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kidogo nichangie eneo lingine la pili eneo la Mlimani City. Kwa upande wa Mlimani City nami niungane na maelezo ya Kamati na mapendekezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo haja mkataba wa Mlimani City ukapitiwa upya.