Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kidogo katika hoja hii iliyopo mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu nagawana muda Mheshimiwa Heche basi nitachangia point moja tu kuhusu Mfuko wa Wanawake na Vijana wa asilimia 10 ambayo inapaswa kukatwa katika mapato ya own source ya Halamashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya LAAC tumeona kwamba huu Mfuko una umuhimu wake na kwa ujumla wake unaweza ukachochea maendeleo ya vijana na wanawake pale ambapo ukitumika kwa hali inayostahili ili hawa vijana na wanawake waweze kufanikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha zinazotoka own sources ya Halmashauri ni kodi za wananchi. Utaratibu wa kuzitoa kama mikopo kwa vijana na wanawake haueleweki, walengwa ambao wanastahili kupata mikopo hii wengine hawapati kwa sababu gani. Hii ni kwa sababu tumegundua kwamba hata vikundi vingine ambavyo vinapewa hiyo pesa vinakuwa ni vikundi hewa, lakini katika Halmashauri nyingi hakuna hata zile Kamati ambazo zinapaswa kukaa na kutoa pesa hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu cha kushangaza kuna baadhi ya Halmashauri hata Wakurugenzi wengine hawajui component ni watu gani ambao wanapaswa kuwa kwenye Kamati hiyo. Kuna Mkugenzi mmoja alisema kwamba Mbunge ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo ilhali Wakurugenzi ndio Wajumbe, kwa hiyo mnaweza kuona ni namna gani mifuko hii inavyotekelezwa bila hata Wakurugenzi kujali kinachoendelea katika Halmashauri zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia utaratibu wa kusimamia urejeshwaji wa pesa hiyo, hizi pesa tumekuwa tukisimamia kwa karibu Kamati zote, Kamati ya TAMISEMI na Kamati ya LAAC tunasimamia kuhakikisha Halmashauri wanapeleka pesa ya asilimia tano kwa wanawake na asilimia tano kwa vijana katika akaunti zao ili waweze kukopeshwa. Ninachotaka kusema ni kwamba pesa hizi hazirejeshwi, huu mfuko unakwenda kisiasa kabisa, ni kama upo upo tu basi, watu wanapata pesa wanajiondokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukirejea maoni na ushauri au alichokiona CAG katika hesabu zake za mwaka wa fedha 2015/2016 kuna pesa zaidi ya bilioni nne zinadaiwa zipo nje, zipo katika vikundi na hizi pesa ni nyingi. Hata hivyo, ni kwamba hizi pesa ambazo zipo zinatolewa na Halmashauri hazina ukomo. Tunaona kwamba hizi pesa zitolewe halafu hii mifuko iwe na kiwango fulani na pia iwe na ukomo, iwe ni rotation fund yaani tukisema Halmashauri moja inajiwekea malengo kwamba sasa tunakusanya ama tunakopesha mpaka tunafikisha bilioni mbili au tatu basi tunaweka ukomo na pesa zingine zinaendelea kufanya maendeleo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maoni yangu nasema kwamba mfuko huu wa kisiasa tu, pamoja na kwamba ni mzuri lakini malengo yake hayatekelezwi. Sioni sababu mfuko huu kuendelea lakini pesa za wananchi zikapotea ina maana Serikali inataka kutuambia nini. Katika ripoti ya mwaka jana, Kamati ya LAAC tulitoa ushauri kwamba itengenezwe sheria maalum ambayo itaweza kuonesha mfumo thabiti wa kuweza kukusanya hizo pesa, kukopesha na baadaye kuzirejesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haikutoa majibu na wala haikutengeneza sheria hii. Hata mwaka huu tumerudia tena maoni hayo kwamba itengenezwe sheria ili kuwezesha mfuko huu kuwa endelevu na kuweza kusaidia wanawake na vijana kwa malengo ambayo yanastahili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na mapendekezo aliyoleta Mheshimiwa Zitto hapa hata kama ni mapema kwa sababu ilikuwa kwenye mchango wangu, kwamba ingekuwa vema basi kama Serikali ikiona haitaweza kuweka utaratibu mzuri basi ianzishe Benki ya Maendeleo ya Serikali za Mitaa ili kuwezesha Halmashauri kuchangia ndani ya benki hiyo na benki ikakopesha vijana na wanawake ili hizi pesa zionekane zina manufaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachoona kule tunapokwenda kukagua ni kwamba vijana wanachukua pesa, wanawake wanachukua pesa basi imeishia hapo, huu mfuko umekuwa shamba la bibi. Kuna baadhi ya Halmashauri wameamua kuziweka kwenye SACCOS lakini ukifuatilia kuona hata wale walioweka kwenye SACCOS hizi pesa wanaopewa siyo walengwa wenyewe. Ukipeleka kwenye SACCOS wanakopa wale wenye uwezo.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano tumekwenda kwenye Jiji la Dar es Salaam wamepeleka zaidi ya bilioni moja kwenye SACCOS yao, sijui kwenye Benki huko ya Dar es Salaam, lakini hizo pesa hazijarejeshwa mpaka leo, kwa hiyo unaweza kuona kwamba hata Halmashauri zenyewe hazina usimamizi mzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.