Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

Hon. Omari Mohamed Kigua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa jioni ya leo niweze kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita zaidi kwenye ripoti hii ya PAC kwa sababu mimi ni Mjumbe kwenye Kamati hiyo. Yamezungumzwa mengi na kuna dosari nyingi sana lakini yote yameainishwa katika ripoti nisingependa kuyarejea. Kikubwa ambacho nataka nikizungumze ni juu ya ushauri kuhakikisha kwamba yale maoni ambayo yametolewa na Kamati yetu ya PAC yanafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yamezungumzwa mengi juu ya dosari katika Mkataba wa Mlimani City, Mkataba wa Dege Kigamboni. Nadhani Serikali imefanya jambo kubwa na imeshaanza kuchukua maamuzi, niipongeze sana Serikali kwa sababu baadhi ya viongozi walishasimamishwa na hii ni kuonesha kwa dhati kabisa kwamba tayari Serikali ilishaona upungufu na imechukua uamuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo nina ushauri mdogo, katika ripoti ya CAG imezungumza juu ya upungufu wa Benki ya Kilimo. Benki hii bado haijapewa nguvu, pesa au mtaji ambao Benki yetu ya Kilimo imepewa ni ndogo sana. Nashauri Wizara ya Fedha pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo wakae chini waone namna ambavyo wanaweza wakaiongezea mtaji kwa sababu sehemu kubwa ya maisha ya Watanzania yanategemea kilimo na nina imani kwamba uanzishaji wa benki hii ulikuwa na lengo la kuwasaidia Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo liko sambamba na hilo ni juu ya suala la Mkaguzi wa Mahesabu (CAG), yote haya tunayoyaona kwenye Kamati za PAC na LAAC yametokana na ripoti ya CAG ambayo ndiyo jicho la Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Lazima tukubali kwamba CAG anafanya kazi kubwa sana, lakini anakwama kwa sababu hawezeshwi pesa nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano tu kwamba, katika kazi yake ya auditing (ukaguzi) performance auditing ndiyo kazi ambayo inaonesha mapungufu mengi sana, lakini ukikaa na CAG anakwambia pesa anayopewa ni ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu unaojionesha katika miradi mingi ya maji, miradi ya barabara ambayo inatokea katika Halmashauri zetu inaonekana kutokana na ripoti ya CAG. Nadhani muda umefika sasa wa kuhakikisha kwamba tunamsaidia CAG ili aweze kuwa na nguvu na ili aweze kutoa ripoti nzuri.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu miradi ya maji, nimepitia taarifa hapa ya LAAC imeonekana miradi mingi ya maji haiko vizuri. Lakini nina ushauri mmoja kwa Serikali kwamba Wizara ya Maji na wenzetu wa TAMISEMI waweke utaratibu na kuunda kikosi kazi cha kuhakikisha na kuangalia kwamba miradi hii inafuatiwa na kukaguliwa ili kuangalia ile value for money inapatikana, vinginevyo malengo tunayokusudia malengo ambayo Serikali wanayokusudia hayatafikiwa kwa sababu maeneo mengi miradi hii iko chini ya kiwango. Mimi nashauri tuangalie namna ambavyo suala la ufuatiliaji wa miradi linakuwa ni suala muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nina ushauri juu ya makusanyo ya mapato katika Halmashauri zetu. Tumeona Serikali imeweka utaratibu wa kukusanya mapato kwa kutumia njia ya kielektroniki kwa maana TAMISEMI wanaona moja kwa moja Halmashauri fulani inakusanya kiasi gani, lakini bado utaratibu huu haujakaa vizuri, zipo baadhi ya Halmashauri ambazo bado mapato hayakusanywi sawasawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshauri Waziri wa TAMISEMI aangalie namna ambavyo anaweza akaongeza udhibiti, au kwa kuongeza mafunzo kwa watumishi wetu wa TAMISEMI ili nia thabiti ya Serikali ya kukusanya mapato katika Halmashauri zetu ifikiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo napenda kulizungumzia ni juu ya suala la Mlimani City. Mlimani City imezungumzwa sana juu ya mkataba ule. Ushauri ninaoutoa ni kwamba upungufu huu Serikali ichukue hatua haraka sana kwa sababu tunapoteza mapato mengi, hata taarifa hii nina uhakika haijamaliza mambo mengi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, nataka kushauri kwamba taasisi ambayo ilikuwa inasimamia mkataba huu ni taasisi nyeti. Nina imani kwamba Serikali itachukua hatua za haraka sana kuhakikisha kwamba dosari zote ambazo zimejitokeza kwenye mikataba hii zinafanyiwa kazi haraka sana ili wananchi wa Tanzania wawe na imani kubwa na Serikali yetu na nina imani kabisa kwamba maoni yetu na ushauri wetu utafanyiwa kazi haraka sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.