Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

Hon. Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana nami kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kuwapongeza Wajumbe wote wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kwa kazi kubwa ambayo wameifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wafahamu ya kwamba Kamati hizi mbili ndizo ambazo zinafanya kazi ya oversight kwa niaba ya Bunge letu, kwa hiyo ni Kamati ambazo taarifa zake ambazo tunazijadili mara moja kwa mwaka na bahati mbaya sana siku hizi kwa siku moja, ni taarifa ambazo ni nyeti mno kiasi kwamba zinahitaji tutulize akili zetu tujadiliane na tuweze kuwa na maamuzi ambayo yatawezesha tuweze kwenda vizuri kwa sababu kazi hizi ni kazi za Bunge, sio kazi za Serikali, kwa hiyo ni lazima Wabunge tuweze kufanya kazi hizi kwa ufanisi na kuweza kufanikisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ambayo ndiyo taarifa zake PAC na LAAC wameleta hapa ilizungumzia mambo mengi sana, miongoni mwa mambo ambayo yalizungumzwa ni suala la Deni la Taifa. Bahati mbaya sana na nadhani hii ni kwa mara ya kwanza tangu PAC itoe taarifa zake kwenye Bunge hii ni mara ya kwanza hatuoni chapter inayohusu Deni la Taifa. Chapter hii ni chapter muhimu ni chapter ya lazima Mama Mwenyekiti mwakani kosa hili lisirudiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ukitazama aliyosema CAG kuhusu Deni la Taifa inaonesha kwamba ndani ya kipindi kifupi sana Deni la Taifa limeongezeka kwa asilimia 168, lakini baya zaidi deni ambalo linatokana na masharti ya biashara limeongezeka kwa asilimia 17 ndani ya mwaka mmoja, madeni yanayotokana na masharti ya biashara, gharama zake ni kubwa sana na inawezekana uwezo wetu wa kuwalipa ukawa na matatizo makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya taarifa hii ya CAG inaonesha kwamba taarifa ambayo Serikali ilitoa kuhusu Deni la Taifa, deni la jumla ya shilingi trilioni 3.2 halikuwamo katika taarifa ya Deni la Taifa. Tulitarajia kwamba leo tungepata maelezo ni kwa nini trilioni 3.2 hazikuhusishwa katika taarifa ya pamoja ya Deni la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, kwa mujibu wa taarifa ya CAG uwiano asilimia 31 ya deni letu la nje ni commercial loans ni madeni ya kibiashara ambapo kama nilivyoeleza hapo mwanzo gharama ni kubwa mno na sasa hivi mwaka jana walikuja Waziri Mheshimiwa Philip Mpango na mwenzake Naibu wake wakaja Bungeni wakaomba ruhusa ya Bunge kukopa dola milioni 700 kwenye bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nilikuwa taarifa ya Wizara ya Fedha kuhusiana na tathmini ya utekelezaji wa bajeti ya Serikali. Taarifa inasema katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imepanga kukopa dola za Kimarekani milioni mia saba zile walizoruhusiwa na Bunge. Taarifa hiyo inaendelea, Serikali imekamilisha majadiliano na Taasisi za kifedha kwa lengo la kukopa kiasi cha dola za Kimarekani bilioni 1.5 maana yake ni bilioni 1.46. Kwa ajili ya kugharamia mradi wa ujenzi ya reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge kutoka Morogoro hadi Makutupora (Makofi).

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa Serikali inakamilisha taratibu za kusaini mikataba. Waziri Mpango ruhusa uliyopewa na Bunge dola za Kimarekani milioni mia saba. Ni wapi ulipata ruhusa ya kwenda kujadiliana kukopa ziada ya
1.5 bilioni? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wote ninyi ni mashahidi, kila siku tunaambiwa tunajenga standard gauge kwa fedha zetu za ndani. Leo Serikali inasema tunakopa kwa nini tunawalaghai wananchi, kwa nini hatuwaelezi wananchi ukweli kwamba hatuna uwezo wa kujenga kwa fedha za ndani, lakini tunakopa kuna ubaya gani? Maana yake kukopa siyo dhambi hamna mtu ambaye hana mikopo hapa, kwa nini tusiwaambie wananchi ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tunamuacha Rais anasema kwamba tunajenga kwa fedha zetu za ndani halafu tunakuja humu Bungeni taarifa za Serikali zinasema tunakopa mnamuaibisha Rais. Kwa hiyo, kuna haja ya kupata maelezo ya Serikali kuhusu masuala haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili Taasisi ya Kupambana na Rushwa PCCB imeundwa kwa mujibu wa sheria. Sheria Sura Na. 329, kifungu cha 47(2) cha sheria ile, kinaitaka PCCB kila mwaka ifunge mahesabu yake yakaguliwe na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, yapitiwe na PAC yaletwe Bungeni. Toka mwaka 2016 PCCB haijafunga mahesabu yake ya mwaka, haijakaguliwa, hawa ndiyo watu ambao wanapambana na rushwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi wamemshtaki Mhasibu wao kwa wizi wamejuaje ameiba wakati hawana audited accounts? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji maelezo ya Serikali, Taasisi hii ni special kiasi gani. Jeshi linakaguliwa, Mwamunyange alikuwa anakuja kwenye Kamati ya PAC na Makamanda wenzake wote kuelezea mahesabu ya Jeshi, kwa nini PCCB haikaguliwi? Naomba tupate maelezo ya kina kabisa ya Serikali kuhusiana na jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu Mama yangu Conchesta amelizungumza, LAAC wametoa taarifa nzuri sana ambayo inaelezea tatizo la asilimia 10. Waheshimiwa Wabunge tusidanganyane humu ndani, sote humu tumekuwa Wabunge wale ambao wamekuwa Wabunge sasa wana miaka kadhaa, wale ambao wamekuwa Wabunge muda mrefu wanajua, asilimia 10 kwa mazingira ya sasa hivi haitekelezeki. Waheshimiwa Wabunge fedha hizi za asilimia 10 siyo ndogo ni fedha nyingi ukiangalia bajeti ya ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ambayo tumepitisha hapa ndani ya Bunge hii inayotumika sasa, jumla ya fedha ambazo Halmashauri zetu zinakusanya kwa mwaka ni bilioni mia sita themanini na saba (bil. 687), asilimia 10 yake ni bilioni sitini na nane, 10 percent hizi kama alivyosema mama yangu Mheshimiwa Conchesta tuzibadilishe. Tuanzishe benki na Halmashauri ziingize hizi fedha kwenye ile benki vijana na wanawake wakachukua mikopo kwenye ile benki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina hakika fedha hizi kwanza zitapelekwa kwa sababu wale mameneja wa matawi ya benki watahakikisha zinapelekwa lakini pili wananaochukua watalipa. Tutaokoa fedha nyingi sana na tutaweza kuleta maendeleo makubwa sana katika Nchi (Makofi).

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa tumepewa amri au maelekezo ya kwamba tuweke viwanda 100 kila Halmashauri kila Mkoa sijui kila Halmashauri au kila Mkoa. Serikali Kuu haina ardhi, ardhi ni ya Serikali za Mitaa, kosa kubwa tutakalolifanya ni kwenda kunyang’anya watu wetu ardhi walipwe fidia kidogo watu waje waweke viwanda, watu wale watapata hela kwa muda mfupi watazitumia zitakwisha. Hebu tubadilisheni kifikra, ardhi ya mwananchi inayotolewa kwa ajili ya uwekezaji iwe land for equity. Wananchi wapate hisa itawalipa ile kwa muda mrefu zaidi na itakuwa na mafanikio makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo wamefanya, Mkoa wa Kigoma tumefanya Mji wa Ujiji City tumeingia mkataba na kampuni kutoka China 20 percent. Mradi mmoja wa hospitali utatupa five billion mapato ya ndani kwa mwaka mmoja. Sasa hivi mapato yetu ya ndani ni bilioni moja tu. Kwa hiyo napenda nishauri tulitazame hili, Waziri wa TAMISEMI aangalie namna ambavyo atalileta kisheria ili tulinde watu wetu tusiwafanye waje kuwa manamba wa wawekezaji bali wafaidike kutokana na uwekezaji ambao utakuwa unafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono taarifa zote hizi mbili na nina maazimio ya marekebisho kidogo kwenye taarifa moja ya LAAC.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.