Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kuniruhusu na mimi nichangie kwenye Bunge hili la Bajeti na hasa katika Wizara hii ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo. Kwa vile hii ni mara yangu ya kwanza kuchangia katika Bunge hili, kwanza napenda kusema machache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza natoa pongezi kubwa sana kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mambo haya anayofanya. Mimi namchukulia Mheshimiwa Rais kama captain wa meli ambayo ilitaka kuzama. Tanzania kama meli ilikuwa na abiria wa aina mbili, wale ambao walikuwa juu na wale walioko chini. Kawaida daraja la kwanza katika meli wanakuwa juu na daraja la chini wanakuwa chini sasa chakula chote kilikuwa kinakwenda juu. Kwa bahati nzuri walioko chini wakaona matatizo ya njaa wakatoboa meli kwa hiyo meli ingezama, waliokuwa juu ambao ndiyo mafisadi na waliokuwa chini masikini wote wangezama. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais ameliona hilo kwa hivyo anakusanya hela zote na kuzipelekea Hazina halafu azigawe kwa wananchi wote wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichangie machache, juzi niliwaona wenzetu wa UKAWA, katika hotuba yote aliyosema Mheshimiwa Rais pale, pamoja na kupunguza ile Pay As You Earn kidogo wakacheka lakini muda mrefu walikuwa wameangalia luninga iliyokuwa live kwa hiyo kila ilivyopita kamera pale kwao wakajikumbusha wapo Bungeni wakashangilia sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende sasa kwenye suala hili kuhusu bajeti ya Wizara ya Kilimo. Mimi nina imani sana na viongozi hawa aliowateua Mheshimiwa Rais katika Wizara hii hasa Mheshimiwa Mwigulu na Naibu Waziri. Pia nina imani na Baraza zima la Mawaziri ambao watasaidiana kwa pamoja na Mheshimiwa Rais kuendesha Serikali. Kuhusu mambo ya kilimo sasa, nina imani Mheshimiwa Mwigulu atakuja na majibu mazuri kuhusiana na matatizo makubwa waliyonayo wakulima. Napenda sana Mheshimiwa atakapokuja kuhitimisha anieleze upatikanaji wa pembejeo kwa wakulima wetu wote lakini vilevile matatizo makubwa ya wakulima wa tumbaku. Zao la tumbaku Tabora limekuwa na matatizo makubwa na halina mafanikio hata kidogo kwa wakulima wa tumbaku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kabisa Serikali itambue kwamba kazi ya kulima tumbaku ni kazi ngumu (hard labour). Kwa hiyo, napenda Serikali itambue kulima tumbaku ni kazi ngumu kwa hivyo wakulima walipwe mara mbili, kwanza kwa kulima tu tumbaku halafu pia wakiuza tumbaku walipwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ningeshauri Waziri wa Kilimo atakaporudi kujumuisha masuala haya ya Wizara ya Kilimo aongelee kilimo cha mazao mengine katika eneo langu la Tabora Kaskazini. Miaka yote wakulima wa Tabora Kaskazini wanalima tumbaku tu kama zao la biashara lakini inavyoelekea tumbaku inazidi kwenda chini na ukiangalia kwenye jedwali lake Mheshimiwa Waziri ameeleza jinsi kilimo cha tumbaku kinavyokwenda chini, lakini vilevile wavutaji wa tumbaku wanapungua kwa hivyo siyo zao linaloweza ku-sustain baada ya miaka 10 ijayo.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri Serikali ipendekeze zao lingine kule Tabora lakini wakulima wanaogopa kulima zao lingine la biashara kwa mfano ufuta, karanga na alizeti kwa sababu mazao haya hayana soko la uhakika. Nina hakika Mheshimiwa Waziri akija na majumuisho yake awashawishi wakulima wa Jimbo langu kulima mazao mengine waepukane na tumbaku ili waweze kuwa na mazao ambayo yatawapa faida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kujua msimamo wa Wizara ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo kuhusu ujenzi wa Kiwanda cha Tumbaku pale Tabora. Kiwanda cha Tumbaku kilikuwa na uwezo mkubwa wa kusaidia kama kitajengwa Tabora na kupunguza gharama kubwa kwa wakulima. Sasa hivi wakulima wanalipia pia gharama ya kuhamisha tumbaku kutoka Tabora kuja Morogoro ambako tumbaku hailimwi. Vilevile tumegundua makampuni yanayonunua tumbaku ambayo ni matatu tu yamejenga makao makuu yao Morogoro ingawa wananunua tumbaku kutoka Tabora na wakulima wanagharamia kuleta tumbaku Morogoro. Napenda kupata tamko la Serikali inafikiria nini kuanzisha Kiwanda cha Tumbaku pale Tabora?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia Kiwanda cha Nyuzi ambacho sasa kinafugiwa mbuzi mule ndani. Kiwanda kile kina uhusiano wa karibu sana na walimaji wa pamba. Kwa hiyo, napenda Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujumuisha aelezee hatma ya kiwanda kile ambacho kilikuwa ndiyo ukombozi wa wakulima wa pamba katika Mikoa ya Shinyanga na Tabora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipate majibu kutoka kwa Mheshimiwa Waziri au Waziri aje na majibu kwa nini mali za Bodi ya Tumbaku ziliuzwa na zikanunuliwa na moja ya kampuni inayonunua tumbaku na bado usimamizi wa zao la tumbaku likabaki mikononi kwa Bodi ya Tumbaku ambayo sasa haina meno? Usimamizi wa zao la tumbaku hauna mwenyewe, matatizo yote yanayotokea kwenye zao la tumbaku hilo ambalo nalisemea muda wote ni kwa sababu halina msimamizi.
Napenda kujua kwa nini Bodi ya Tumbaku imepewa jukumu la kusimamia tumbaku na wakati haina uwezo wowote kwa sababu mali zake zote zimeuzwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni vituo vya utafiti. Hatuwezi kuendesha kilimo hapa Tanzania bila utafiti. Nimeangalia kwenye jedwali la Mheshimiwa Wiziri ya Kilimo, utafiti umepewa hela ndogo sana na kwa sababu hiyo tunaendesha kilimo ambacho hakina utafiti wa kutosha. Napenda Serikali iongeze fedha kwenye utafiti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia niongelee mambo ya ruzuku. Fedha zinazoletwa kwa ajili ya pembejeo na mbegu wafikiriwe kwanza makampuni yanayotengeneza mbegu na mbolea hapa Tanzania kwa sababu tunayalipa makampuni yanayotoka nje na yakiharibu hatuwezi kuyakamata. Hivi karibuni Kanda ya Ziwa waliuziwa mbegu ya pamba ambayo haikuota na hili katika nchi nyingine unaweza kushtakiwa ulipe gharama ya wakulima kwa mazao waliotegemea kuvuna. Mbegu za pamba zimeuzwa, wananchi wamepanda, wakaweka na mbolea na mbegu hazikuota. Hili ni jambo baya sana na limefanya wananchi wawe na chuki kwa Serikali yetu. Tungependa Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujibu maswali haya aongelee vizuri sana jinsi ya kusimamia ruzuku inayotolewa na Serikali kwenda kwa wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, liko pia suala la pembejeo, pembejeo imekuwa kiini macho inatajwa hapa na kwenye bajeti hela nyingi, lakini gharama ya pembejeo inayofikishwa kwa wakulima kule Jimbo la Tabora Kaskazini ni kubwa mara tatu, nne ya bei ya mbolea hiyo Dar es Salaam. Mbaya zaidi mbolea ya ruzuku kwa mfano ya kupandia inafika katikati ya kilimo yaani kilimo kimeshaisha ndipo mbolea ya ruzuku inafika, mbolea ya kupandia imekuwa ya kuvunia. Vilevile mbolea ile inayotolewa kama ruzuku haiwafikii wananchi inafikia kwa madalali jambo hili limekuwa baya sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda Mheshimiwa Waziri wa Kilimo atakapokuja aje na majumuisho mazuri kuhusu upatikanaji wa pembejeo na hasa mbolea ya ruzuku kwa wakati ili wananchi waiamini Serikali yao. Sasa hivi watu wote ukisema ruzuku ni kama vile wanabeza kwa sababu kwa kweli mbolea ya ruzuku haifiki na mbaya zaidi wakulima hawa maskini wanapata tabu sana kwa sababu mtu aliyetakiwa kupeleka mbolea kwa mfano tani 10, anapelekea tani moja na baadaye anaenda kusainisha vocha kwa watu maskini kwa kuwahonga hela ndogo ndogo halafu yeye analipwa hela nyingi sana, Serikali lazima ihurumie watu wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile yako mambo ya ushirika. Vyama vya Ushirika na Sheria ya Ushirika ni mbaya sana kwa wakulima. Viongozi wa Chama cha Ushirika ingawa wametokana na wakulima wenyewe hakuna anayewasimamia. Vyama vya Ushirika havikaguliwi, vinaiba, vina madeni makubwa wanalipa wakulima. Mbaya zaidi wakulima waaminifu …
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii, ahsante sana.