Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017.

Hon. Deogratias Francis Ngalawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ludewa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017.

MHE. DEOGRATIUS M. NGALAWA – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kukushukuru wewe binafsi kwa kunipa ruhusa ya kuja kuongelea mambo mbalimbali ambayo Waheshimiwa Wajumbe wameyajadili kuhusu taarifa ya utekelezaji wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, wachangiaji katika Kamati hii, wamechangia Waheshimiwa Wabunge 23. Kwa kuongea wamechangia Waheshimiwa Wabunge 16 na kwa maandishi wamechangia Waheshimiwa Wabunge saba. Napenda niwataje Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamechangia hasa kwa maandishi kwa sababu hawa walioongea wameonekana hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge waliochangia kwa maandishi ni Mheshimiwa Lucia Michael Mlowe, Mheshimiwa Mary Deo Muro, Mheshimiwa Oran Njeza, Mheshimiwa Juma Othman Hija, Mheshimiwa Zainab Mndolwa Amir, Mheshimiwa Rhoda Edward Kunchela na mwisho ni Mheshimiwa Silafi J. Maufi.

Mheshimiwa Naibu Spika, wachangiaji wengi katika taarifa hii ya Kamati walijikita sana kwenye maeneo ya madeni. Walijikita pia kwenye maeneo ya mradi wa umeme wa maji wa Mto Rufiji ambao tunaita Stieglers Gorge, miradi ya REA I, REA II na REA III bila kusahau Densification Project.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile walizungumzia matumizi ya gesi kwa maana ya kuwepo kwa master plan ili kuweza ku-utilize gesi ambayo ipo kwa sasa ambayo inatumika kwa kiasi kidogo. Pia walizungumzia Taasisi ya GST, elimu kwa wachimbaji, ruzuku kwa wachimbaji wadogo, makusanyo ya maduhuli na suala zima la biashara ya Tanzanite.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa kifupi wazungumzaji wengi wameipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa utekelezaji mahiri wa miradi yetu mingi ambayo inatekelezwa sasa na Serikali hii ya Awamu ya Tano. Wachangiaji wengi waliojikita katika madeni hasa ya TANESCO na TPDC ukiangalia lengo lao kubwa lilikuwa ni kuzifanya hizi taasisi mbili ziweze kujiendesha bila kutegemea ruzuku au mkono wa Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hoja zilijikita zaidi katika kuhakikisha kwamba wanayasaidia mashirika haya mawili ya TANESCO na TPDC kuondokana na ule mzigo wa madeni na hasa TANESCO. Kwa sababu deni la TANESCO wadaiwa na wadai unakuta kwamba TANESCO bado anabaki kuwa na deni kubwa. Kwa hiyo, nguvu zilielekezwa nyingi kwa wachangiaji wengi kuona kwamba hili shirika la TANESCO, Serikali iweze kuhakikisha kwamba inalisaidia ili iweze kujiendesha yenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa eneo la TPDC; pia TPDC ana madeni, lakini madeni ambayo TPDC anayo ni madeni machache kuliko madeni ambayo yenyewe inadai. Hata ukijaribu kuiangalia TPDC kwa undani na kwenye maelezo ya taarifa yetu, unakuta kwamba TPDC bado inabaki na hela nyingi kiasi ambacho yenyewe inaweza ikajiendesha. Kwa hiyo, michango mingi ilikuwa inaonesha kwamba TPDC ina mzigo mkubwa na Serikali inatakiwa kuingiza mtaji mkubwa ili kuhakikissha gesi ile ambayo inatumika itengenezewe miundombinu ya kutosha kwa sababu gesi inayozalishwa ni nyingi kuliko ambayo inatumika sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wajumbe wengine walijikita sana kwenye mradi wa umeme wa maji wa Mto Rufiji naamini kwamba hii Mheshimiwa Waziri na baadhi ya Wajumbe waliizungumzia kwa kina kwamba huu mradi siyo kwamba umeanza, ila upo katika maandalizi ya kuanza. Sasa na ni vizuri mara nyingi mradi kabla hujaingia kwenye ile process yenyewe kuufahamu, kabla haujaileta bajeti hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, bajeti itakuja wakati tayari kila kitu kipo kwenye table na vitu hivyo vinakuwa vinaonekana. Kwa hiyo, sisi kama Kamati tunaipongeza Serikali kwa hatua ambazo inazichukua kwa sababu umeme huu wa stieglers Gorge utatuletea Megawati 2100 na vilevile itaendana sambamba na linkage ambayo inawekwa na philosophy ya nchi kwenda kwenye uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kulikuwa na miradi ya umeme wa REA. Wachangiaji wengi wamezungumzia upungufu ambao umefanyika katika mradi wa REA awamu ya kwanza na REA awamu ya pili; na mara nyingi ni kule kurukwa kwa baadhi ya vijiji. Umeme unatoka kijiji hiki hapa, kinaruka unaenda kwenye kijiji kingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukijaribu kuangalia, wengi wameshauri kwamba ule upungufu ambao tayari umeshaonekana katika hii miradi ya REA I na REA II maana yake ni kwamba sasa kwenye REA III yafanyike maboresho. Bahati nzuri Serikali imekuja na utaratibu wa Densification Project ili kuweza ku-clear upungufu wote ambao umefanyika katika REA I na REA II na bahati nzuri baadhi ya Wakandarasi tayari wameshapewa tender na wapo site wanafanya kazi hii ya marekebisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna matumizi ya gesi; wachangiaji wengi wameona kwamba gesi iliyopo ambayo inazalishwa na TPDC ni nyingi. Kwa hiyo, kuna haja sasa ya Serikali kutengeneza miundombinu wezeshi ya kuifanya TPDC iweze kupeleka gesi maeneo mbalimbali na hususan kwenye majumba yetu. Kwa hiyo, hiyo master plan itaonesha maeneo ambako gesi inapita na hata kama wawekezaji watakuja, maana yake watatumia ile master plan ambayo ipo. Vilevile wachangiaji wengine walizungumza kwamba kuna baadhi ya nchi jirani ambazo na zenyewe zinaenda na mifumo hii. Kwa hiyo, maana yake TPDC iwezeshwe ili kuweza kuingia kwenye soko la kiushindani la Kimataifa, kwa sababu gesi iliyopo ni nyingi na watumiaji ni wachache.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia limeongelewa kuhusu Geological Survey of Tanzania (GST) kwamba ndio iwe mtafiti pekee wa madini Tanzania na in case kama kuna wawekezaji wa uchimbaji, basi wapate consent au washirikiane na taasisi hii katika kufanya utafiti huo. Kwa sababu inaonekana baadhi ya taasisi za nje zinafanya hujuma ya kufanya tafiti kwa muda mrefu kiasi ambacho hata zile taarifa nchi inakuwa hazina.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, kwa kuiunganisha na GST kwa kupata consent ya GST maana yake ni kwamba, nchi kwanza itapunguza ule urasimu ambao unafanywa na pia nchi itakuwa na clear picture ya maeneo ambayo yana madini na vilevile itawafanya baadhi ya wachimbaji wetu wadogo na wa kati kutokutumia gharama zao nyingi katika kuwekeza mahali ambako hawana uhakika wa madini ambako yapo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naamini kwamba GST ikishakuwa mbele ya wachimbaji wetu wa kati na wa chini, maana yake ni kwamba mtu ataenda kuwekeza na atakopa mikopo benki kwa ajili ya uwekezaji huu akijua picha halisi na hali halisi ya madini iliyopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia limezungumziwa suala la elimu kwa wachimbaji. Elimu kwa wachimbaji ni muhimu na hata sisi Kamati tumesisitiza hilo kwa sababu kuna athari nyingi ambazo zinatokea kule kwa sababu ya kukosa uelewa na kukosa elimu ya kutosha juu ya maeneo hayo, kunakuwepo na athari nyingi na ajali nyingi, kwa mfano kuangukiwa kwa vifusi na vitu vya namna hiyo. Hayo yameelezwa, nasi kama Kamati tuliona jambo hili ni la muhimu kupewa kipaumbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, lilizungumzwa pia suala la ruzuku kwa wachimbaji wadogo. Hapa pia lilizungumzwa na suala la elimu na ndiyo maana unaona hata kwenye ripoti ya Kamati na Wajumbe walipokuwa wanachangia, kuna baadhi ya pesa za ruzuku ambazo Serikali imepeleka, lakini ilienda kufanya kazi ambayo haikukusudiwa. Watu walienda kuelekeza kwenye maeneo ambayo hawakuyaombea. Kwa hiyo, hapa upatikane usimamizi wa kutosha ili kuhakikisha kwamba hela inayotolewa na Serikali inasimamiwa na inafanya klengo lililokusudiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika upande wa madini kuna makusanyo ya maduhuli. Napenda kuipongeza Wizara ya Madini kwa ukusanyaji wa maduhuli asilimia 84 ya lengo ambalo ni la mwaka mzima kwa kukusanywa ndani ya nusu mwaka. Kwa hiyo, kama Kamati tunaipongeza, iendelee na utaratibu huo. Vilevile wapo walioipongeza Serikali kwa kuchuka hatua kuhusu utoroshwaji na ubadhirifu ambao unapatikana kwenye madini yetu ya Tanzanite. Serikali imeshachukua hatua kubwa ya kujenga ule ukuta na pia kupitia mikataba ambayo inaonekana inaitia hasara nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla, Waheshimiwa Wabunge wengi waliochangia kwenye Kamati yangu wameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi inayozifanya, ni kazi njema, ina nia njema na imeonesha uzalendo mkubwa kwa ajili ya maendeleo ya Taifa hili na maendeleo ya watu wake wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchukua hatua hii kukupongeza wewe, Mawaziri wote, kuwapongeza Wabunge wote waliochangia kwenye Kamati yangu na naomba sasa taarifa hii ya utekelezaji ya Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini ipokelewe na Bunge lako na kuwa ni taarifa rasmi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja.