Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.

MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kuniruhusu nichangie hoja hii ya Kamati ya Kudumu za Bunge na hasa Kamati hii ya Kilimo, Mifugo na Maji. Maji limekuwa tatizo kubwa sana katika maeneo yetu hasa Majimbo ya vijijini kuliko mijini ambako maji hayapatikani kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli nianze kuishukuru Serikali kwa kubuni Mradi huu wa Ziwa Victoria ambao unakuja kuleta maji katika Jimbo langu la Uyui-Tabora Kaskazini na Tabora Mjini. Ukitoa mradi huu pekee, Jimbo langu la Tabora Kaskazini hakuna maji chini, yako katika maeneo machache tu na ningeomba Serikali itumie uonekanaji wa vyanzo hivi vya maji kuwagawia maji wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, limekuwa tatizo kubwa sana wakati Wizara ya Maji inazo fedha na Halmashauri kupitia Wizara ya TAMISEMI ndiyo nao wanatafuta wakandarasi au wazabuni wa kuchimba maji. Tunaye Wakala wa Maji kama alivyo Wakala wa TBA huyu ni DDCA. Hawa ni wataalam wazuri sana na wana bei chini kabisa lakini Halmashauri nyingi ikiwemo ya kwangu hawawatumii watu hawa, hawatumii wakala huu wa Serikali ambao wangeweza kuchimba maji kwa bei rahisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo mifano miwili. Hivi karibuni wananchi wa Kata ya Ikongolo ambayo ina vijiji vinne vya Majengo, Kanyenye, Ikongolo yenyewe na Kiwembe walitafuta eneo ambalo kiangazi chote wanateka maji pale kama chanzo kikubwa cha maji lakini kukawa na kutoelewana na Halmashauri kwamba watafute mzabuni apime maji pale ikashindikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama Mbunge nalijitolea kutafuta hawa watalaam wa DDCA wakaenda wakathibitisha maji yako pale na vilevile wakatoa na ankara za uchimbaji wa visima vitatu. Bahati mbaya sana mwaka huu wa 2016 wakasema Halmashauri haina fedha, lakini baadaye ilipopatikana fedha kwa kutumia nafasi hiyo wakatangaza zabuni wakati mkandarasi DDCA ameshapeleka bei ya shilingi milioni 15 kwa kisima. Wakatangaza zabuni na wakachimba visima kwingine kabisa kwa bei ya milioni 27 karibu milioni 30 kwa kisima karibu mara mbili ya bei ambayo DDCA alisema, sasa mimi naona hili ni tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshamwona Mheshimiwa Waziri wa Maji, nimeshamwona Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI na nafikiri kama walivyoniahidi watalifuatilia suala hili. Sioni kama ni halali tunaye Wakala wa Serikali na anaweza kuchimba maji kwa bei nafuu kama ambavyo Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli aliamua kuwapa kazi TBA ilitokana na matatizo ya wakandarasi wababaishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri Waheshimiwa Mawaziri wote wawili watakapokuja kufanya majumuisho, waniambie tatizo hili la maji kwa nini hawakutumia DDCA wakatafuta wakandarasi wengine ambao watachimba kisima kimoja kwa bei ya visima viwili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika vijiji vyote vinne vile kisima kimoja hakitoshi. Kwa hiyo, bado tu wataendelea kuchimba kisima cha pili au cha tatu au vinne kwenye vijiji vyote vinne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nihamie kilimo. Kila mtu akisimama humu ndani anajua kwamba asilimia 75 mpaka 80 ya wananchi wanakaa vijijini na kilimo ndiyo msingi wa maisha kule na ndiyo wanaolima tunakula sisi tunaokaa mijini. Hata hivyo, kilimo hakipewi thamani kama vile ambavyo afya ikikosekana mahali tunapiga kelele wote, maji yakikosekana mahali tunapiga kelele wote, usafiri ukikosekana mahali tunapiga kelele wote, hawa watu asilimia 75 hatupigi kelele sana na kuwasaidia wakulima wetu hawa ili Maafisa Ugani wafanye kazi sawasawa na Madaktari wanaotoka kwenye sekta ya afya au wanaofanya kazi kwenye sekta ya barabara yaani sekta hii ya kilimo haiangaliwi na matokeo yake haikui.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na kauli mbili leo asubuhi hapa, kuna kauli iliyosema sekta inakua kwa asilimia 1.2 nafikiri mwaka jana, mwaka huu sekta ya kilimo ambayo ndiyo sekta muhimu sana kinakua kwa asilimia tano, haisadiwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kilimo kimekuwa cha kizamani. Siku za nyuma kulikuwa na vituo vya kufundishia mifugo kufanya kazi ya wanyamakazi, lakini vimetelekezwa. Pale kwangu Upuge kuna kituo kizuri sana alifungua Marehemu Mwalimu Nyerere kimetelekezwa na nimekuwa napiga kelele humu ndani kwa sababu mashine nyingine bado nzima zingeweza kusaidia kufufua utengenezaji wa mikokoteni au vifaa vya kilimo na ufundishaji wa maksai ili kilimo kiwe rahisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye mazao ya biashara. Tumbaku imekuwa issue pale kwetu, sasa hivi kuna mpango wa korosho na sasa hivi korosho imetuaibisha huko nje, watu wasiojulikana wamepakia nusu ya gunia vitu vingine siyo korosho na nusu korosho. Mambo haya yametutia aibu kwenye soko ambalo tulilipata huko Vietnam lakini pia hapa waliopakia mizigo ile wamechukuliwa hatua gani? Serikali lazima ijisafishe iseme kwamba tatizo hilo ni watu wachache siyo Serikali nzima, siyo Tanzania yote tumefanya kosa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupata soko ni kazi kweli kweli lakini siyo kazi kama kulitunza. Sasa kama kuna watu walifanya hivyo miaka iliyopita kwenye pamba, pamba ilituharibikia kweli kweli mikononi mwetu, soko la pamba lilipotea kabisa lakini baadaye limerudi na kwa vile limerudi kwa matatizo makubwa namna hii sasa litunzwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Maafisa Ugani ni muhimu sana wasimamie pamba itoke safi, zamani sisi kule Usukumani na Unyamwezini pamba tuliita dhahabu nyeupe lakini baadaye ikawa takataka, ikatuangukia mikononi. Tunaomba sana sana Serikali itakapokuja hapa ituambie mikakati ya kutunza pamba itoke safi na mikakati ya kutunza korosho zitoke safi ili masoko tuliyoyapata tuweze kuwa nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sipendi kupigiwa kengele mara mbili, naomba niseme hayo ndiyo nilitaka kuwasilisha. Ahsante sana.