Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017

Hon. Abdallah Ally Mtolea

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Temeke

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nakushukuru kwa kunipatia fursa ya kuchangia katika Taarifa za Kamati hizi mbili, lakini nazipongeza sana Kamati hizi mbili, zimefanya kazi nzuri kwa kadri walivyoweza. Wamegusa maeneo mengi ambayo kimsingi yanaigusa jamii yetu kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika hali tu ya kuongezea, nami nina machache ya kuongezea ili tutakapoishauri Serikali, basi tuzidi kuboresha huduma za jamii kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na hii ambayo kwenye Kamati ya UKIMWI umesema ni gender based violence. Vitendo vya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia vimekuwepo kwa muda mrefu. Mtakumbuka Bunge hili na Tanzania kwa ujumla ilionesha kukasirishwa sana na vitendo vile vya uuaji wa vikongwe, mnakumbuka Wanyamwezi walikuwa wanawaua vikongwe huko, sheria ikasimama kwamba watu hao waadhibiwe kiasi kwamba wengine hawatoiga. Pia matukio yale ya kuuawa kwa albino na kukatwa viungo, kama Taifa tuliungana pamoja kulaani vitendo hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna jambo la ubakaji hasa kwa watoto wadogo. Matendo ambayo yametokea mwaka 2017 yametuvunja nguvu sana sisi wapigania haki za watoto na jinsia. Kwanza Serikali ilikataa watoto wa kike wanaopata ujauzito wasirudi mashuleni. Kwetu lilikuwa pigo namba moja, lakini mwisho wa siku Serikali ikaamua hivyo. Kwetu imetunyong’onyeza sana kwa sababu tunaona watoto hawa ambao hawakupata hizo mimba kwa makusudi, zilikuwa bahati mbaya, wanakosa fursa ya kujiuliza tena na kurudi shuleni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi kwenye maadhimisho ya Uhuru wa Tanganyika, ukatoka msamaha kwa Babu Seya na wenzake, watu ambao pasipo na shaka mahakama zilithibitisha kwamba hawa watu ni wabakaji. Sasa tunapokuwa tunasamehe wabakaji, wapi ulinzi wa watoto katika Taifa hili? Tunawafundisha nini? Misingi yetu ya kukomesha vitendo hivi imepotelea wapi sasa? Tunakwenda mbali zaidi, tunawachukua, tunawapeleka Ikulu, tunawapandisha kwenye majukwaa wafanye show, tunawaona kwamba ni kioo cha jamii, wanafundisha nini? Mnataka watoto wajifunze nini kutoka katika hilo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua mamlaka makubwa ambayo Mheshimiwa Rais anayo chini ya Ibara ya 45 ya kuwafutia watu vifungo, lakini kufuta kifungo hakuondoi kuwa wewe ni mkosaji katika kosa fulani na mtatambua mwenye nguvu ya ku-justify kwamba huyu amekosa, huyu ana hatia ya jambo hili, ni mahakama peke yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama ya Kisutu Jijini Dar es Salaam ilithibitisha hilo pasipo na shaka, lakini walikata Rufaa kwenda Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na yenyewe pia ikajiridhisha kwamba hawa watu ni watuhumiwa katika kosa hilo. Wakaenda Mahakama ya Rufaa, Mahakama ya mwisho kabisa katika nchi hii; na yenyewe ikajiridhisha pasipo na shaka hawa ni wabakaji. Leo tunawachukua, tunatembea nao majukwaani. Je, mnataka siku ya mwisho tukiwauliza watoto kwamba ukiwa mkubwa unataka kuwa nani, aseme nataka kuwa mbakaji? (Makofi)

T A A R I F A . . .

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza siyo taarifa, lakini yawezekana humu ndani tukawa tunafana kiumri lakini tukatofautiana sana katika vichwa vyetu. Kwa hiyo, ni lazima haya pia tuyazingatie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie tu mtoa taarifa, siyo nia yangu hata siku moja kuwa kituko ndani ya Bunge hili kama ambavyo wewe unataka niwe. Mimi nimeletwa hapa na wapigakura wa Jimbo la Temeke, moja kati ya Majimbo yaliyo mjini, moja kati ya majimbo ya watu waliokwenda shule, wanaojitambua na wanaojiheshimu.

Kwa hiyo, ninawakilisha group moja tofauti sana na group ambalo labda wewe unakuja kuliwakisha hapa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachosema ni kwamba ni lazima tuwe na jambo linalofanana, tuwe na nia moja. Tunapoamua kupabambana na mambo maovu, tupambane nayo kweli kweli. Mumshauri Mheshimiwa Rais afanye mambo ambayo wananchi ndio wanayataka. Mkipoteza naye anapotea, mnaipoteza Serikali, mnalipoteza Taifa na mnakipoteza chama chenu ambapo kimsingi kimeshapotea. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine...

T A A R I F A . . .

MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa hii. Naomba nisiendelee hapa, panaweza pakamliza mtu, ni kipande kizito sana hiki kukizungumzia hasa sisi ambao tunawajali watoto wa Taifa hili. Naomba niende kwenye mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, limezunguzwa pia suala la utoaji wa huduma hii ya methadone kwa wale warahibu wa dawa za kulevya. Dawa hizi au huduma hii inatolewa kwa ufadhili wa asilimia 100 na siyo kwamba huduma hii inatolewa kwa kiasi ambacho kinaridhasha, bado uhitaji wa huduma hii ni mkubwa kuliko ambavyo huduma yenyewe inatolewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye vituo wanajaribu kuwachuja ili kupunguza wingi wa watu watakaowahudumia. Sasa hivi wanawapa dawa hizi wale tu ambao wanatumia madawa ya kulevya kwa njia ya kujidunga sindano. Zile njia nyingine, yaani kama mtu anatumia dawa za kulevya kwa njia nyingine kama zile za kunusa, kwa maana wanasema sniff au ile cocktail wao wanaambiwa ninyi bado hamjafia katika kiwango cha kupata huduma hiyo. Sasa kinachotokea ni nini? Kwa sababu vijana hao wana mwitikio mkubwa wa kujitoa katika matumizi ya dawa za kulevya, nao sasa wanaruka hizo hatua, wanatoka kwenye cocktail, wanatumia sindano ili wa-qualify kwenda kupata hiyo huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo ni hatari kwa sababu kwenye matumizi ya kutumia sindano ndiyo huko mnakutana na maambukizi ya magonjwa ya UKIMWI pamoja na magonjwa mengine. Sasa ni vizuri Serikali na yenyewe ikatia mkono ili kuifanya huduma hii ili ipatikane kwa kiwango cha kutosheleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimsikia Waziri Mkuu wakati anafungua Kituo cha Methadone pale Hospitali ya Rufaa Mbeya mwezi Juni, 2017 akiziagiza hospitali zote za mkoa ziwe na Vituo vya Methadone; lakini kuviagiza peke yake bila Serikali kutenga fedha, hili agizo litatekelezwaje? Mwenyewe pale akasikia, wanasema kwamba Kituo cha Methadone cha Hospitali ya Rufaa ya Mbeya kitakuwa kinahudumia watu kutoka Njombe, Songwe, Iringa na Ruvuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi mtu anatokaje Songwe, Njombe kwenda kula dawa Mbeya na kurudi kila siku? Kwa sababu hizi dawa hupewi ukale nyumbani, ni lazima ukazilie kituoni na za kila siku. Vituo vinapokuwa mbali, inakuwa ni mzigo sana, hawa watu hawataweza kuzifuata. Ndiyo matokeo yake, wote hawa wanasafiri wanakuja kukaa Temeke sasa, tunaonekana Temeke ndio tuna warahibu wengi. Tusaidiane huu mzigo uweze kupungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni vitendo vya ushoga na usagaji. Hili tatizo linazidi kukua hapa nchini. Kwenye shule za msingi, sekondari za day na za bweni vitendo hivi vinaendelea kinyemela. Watoto sijui wanajifunza wapi, sijui ni mitandao, lakini wanalawitiana kiasi ambacho hawa wanakuja kujijenga kuja kuwa mashoga wa baadae. Vilevile kuna watu wanajitangaza kabisa mitandao na mitaani kwamba wao ni mashoga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi Serikali badala ya kwenda kupambana na watu ambao eti wanavaa nguo fupi au wana-post picha za uchi mitandaoni, kwa nini tusipambane kwanza na mashoga na wasagaji? Tupambane na hawa ambao kwanza wanajitangaza kwa sababu ndio wanatengeneza, wanavutia watoto wengine wadogo waweze kujifunza hayo mambo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunawachukua watoto wa kike kwenda kuwapima mimba randomly kwa kuwashtukiza, tuanze na utaratibu wa kwenda kuwapima watoto wote kama wameshaingiliwa ili watutajie nani kawaingilia tuweze kuchukua hatua. Vinginevyo tatizo hili ninazidi kuwa kubwa nchini na itafika mahali tutaanza kukimbiana hapa. Hali ni mbaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni tatizo hili la kifua kikuu. Ugonjwa huu wa kifua kikuu sioni kama Serikali imeanza kuuchukua kwa nguvu inayostahili, lakini kuna tatizo kubwa la maambukizi ya ugonjwa huu wa kifua kikuu hasa sehemu hizi za mikusanyiko kwa maana ya huko migodini, sehemu za burudani, kwenye viwanja vya mipira ambako mikusanyiko ya watu inakuwa ni mikubwa. Ikiwa kuna watu wawili au watatu wana ugonjwa huu wa kifua kikuu ni rahisi kuusambaza kwa watu wengine. Kwa hiyo, ni vizuri Serikali ikawa na mpango mahususi katika maeneo yote ambayo yana mikusanyiko, tuone ni namna gani tunapambana na ugonjwa wa kifua kikuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, ni kule kuharibika haribika kwa CT-Scan katika Hospitali ya Muhimbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tatizo hili haliishi? Kila wakati lazima usikie CT-Scan imeharibika. Watu wanasafiri kutoka mikoa mbalimbali kupeleka mgonjwa Muhimbili, anafika pale mgonjwa ana hali mbaya, anaambia wiki hii yote CT-Scan imeharibika, kwa hiyo, usubiri. Watu wanapoteza maisha kila uchao. Kwa nini Serikali haiangalii jambo hili? Kama hiyo CT-Scan moja haitoshi, kwa nini tusiwe na nyingine standby? Hebu tutambue kwamba hili tatizo ni kubwa sasa na ifike mahali tuone tuna mkakati mahususi kwa ajili ya kulingamiza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja zote hizi mbili.