Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DEVOTHA M. MINJA: Nakushukuru Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kunipa nafasi. Kutokana na muda mfupi, naomba nianze kwa kupongeza taarifa za Kamati zote mbili, tumefatilia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niwapongeze waandishi wa habari kwa kazi ambazo wanaendelea kuzifanya. Waandishi wa habari kwa sasa wanafanya kazi katika mazingira magumu sana, hilo lazima tuseme. Wanafanya kazi katika mazingira ya kutishwa, vitisho vikali, lakini sisi tunaendelea kuwaeleza waendelee kupambana kwa ajili ya Taifa hili. Zipo nchi nyingi zimepata uhuru kutokana na waandishi wa habari kufanya kazi yao vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunawapa moyo na tunawaambia, ukweli utaendelea kuliweka huru Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia sana taarifa hii ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Maendeleo ya Jamii. Waandishi wakiwa katika kundi hili, kuna mambo ambayo nimeona hata Kamati haikuwatendea haki. Katika taarifa nilitegemea kuona taarifa ya hali halisi za waandishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza leo Mwandishi Azory Gwanda wa Mwananchi, ana siku ya 79 hajaonekana, hajulikani alipo. Gazeti la Mwananchi limekuwa likiandika kila siku mtu huyu yuko wapi na hatuoni juhudi zozote. Tulitegemea Kamati ingeelezea kuhusu wadau hawa muhimu kwenye tasnia hii, waandishi hawa ambao wamepotea, ambao wametekwa, taarifa zao ikiwemo ile ya kina Roma Mkatoliki ambapo Mheshimiwa Waziri alituahidi hapa kwamba ataleta taarifa kamili kwamba tukio lile lilitokeaje? Tulitegemea kuyaona hayo ndani ya Kamati hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na muda, naomba nizungumzie suala la press card. Nimesoma taarifa hii inaeleza kwamba waandishi 54 ndio wamepata press card na kati ya hao 14 ni waandishi wa nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa nini waandishi? Sheria inawatambua waandishi, inatambua taaluma ya uandishi wa habari, wanashindwa kupata press card. Press card ni shilingi 50,000. Mwandishi wa habari shilingi 50,000 kwa mwaka; driving licence ni shilingi 40,000 kwa miaka mitatu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Serikali isione umuhimu wa kuhakikisha waandishi wa habari wanapata press cardkwa bei nafuu? Passport hizi ambazo tunatumia, ambazo zinakwenda kwisha muda wake, ni shilingi 50,000 ndani ya miaka 10, lakini mwandishi wa habari anakuwa na press card ambayo atalipa 50,000 ndani ya mwaka mmoja. Huu ni uonevu na tunasema, labda watuambie kama TRA imeahinisha press card ni moja ya vyanzo vya mapato, ndiyo tunaweza tukawaelewa. Vinginevyo kwa kuwa taaluma hii imeshafahamika, wapewe nafuu ili waweze kutambulika na wawe na vitambulisho vya kueleweka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze kuhusu Habari Maelezo. Habari Maelezo imegeuka kuwa wahariri, wametoka kwenye majukumu yao ambayo yameelekezwa na sheria tuliyoipitisha, hivi sasa ndio wanaofanya editing kwenye vyombo vya habari. Hivi karibuni Habari Maelezo imeiandikia Gazeti la Tanzania Daima barua lijieleze ni kwa nini lina-cover story za Kinondoni za upande wa upinzani peke yake? Hiyo siyo kazi ya msingi ya Habari Maelezo. Kwa nini Habari Maelezo isiiandikie Gazeti la Uhuru kwa nini linaandika habari za CCM? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, magazeti binafsi yanaangalia story zinazouza, yanaangalia yaandike nini ambacho kitauzwa ili wafanye biashara. Kuwalazimisha kwamba waweke front page habari za CCM na wasipouza, mbona gazeti la Uhuru haliuzi? Lina nakala ngapi hivi sasa na linatembea wapi? Kwa hiyo, watu wanaangalia, watu wanataka nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya Habari Maelezo kwenda kusimamia kuhakikisha Tanzania Daima inaandika habari za uchaguzi siyo; kwa sababu kwa mujibu sheria, wakati wa uchaguzi vyombo vya habari vinakua chini ya Tume. Ilikuwa ni jukumu la Tume kusema kwa nini chama hiki kinakosa fursa kwenye gazeti? Siyo kazi ya Habari Maelezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba Habari Maelezo wafanye kazi zao na siyo kuhakikisha wanafuatilia magazeti mengine kwa maana kwamba inatupelekea kuona kama kuna maelekezo fulani ambayo hatuyaelewi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kuyafungia magazeti. Magazeti yameendelea kufungiwa kila kukicha. Naomba kufahamu na Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujumuisha atueleze; anatoa wapi mamlaka hii ya kufungia magazeti?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya Vyombo vya Habari tuliyoipitisha hivi karibuni, haijampa mamlaka Waziri kufuta magazeti. Haijampa mamlaka hayo na atueleze ni kwa kutumia Kanuni zipi na Kipengele kipi? Kwa sababu tulisema mwamuzi wa mwisho atakuwa ni mahakama. Mahakama itakuwa na room ya kusikiliza upande huu na upande huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya hapo sheria baada ya kusainiwa, kanuni zipo tayari, walitakiwa kuandaa yale mabaraza matatu ambayo kazi yake ilikuwa ni kushughulika endapo kuna mwandishi amepotosha, kuna mtu ambaye amekwenda kinyume na maadili. Kwa nini Serikali inaona kigugumizi kuunda mabaraza haya ikiwemo Baraza la Ithibati?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisema unaadhibu gazeti kwa kulifungia, ni sawa na kusema kwamba eti unaifungia hospitali kutokana na daktari mmoja kuua mgonjwa. Huwezi kuifungia hospitali kwa sababu ya daktari mmoja; badala yake uta-deal na yule daktari. Ndivyo ilivyo kwa waandishi wa habari. Kama utalifungia gazeti, wapo wafagizi, wapo maafisa masoko, wapo watu ambao wao ni makarani na wahasibu; chain zaidi ya watu 300. Mtu mmoja kweli akoseshe watu 300 ajira? Haiingii akilini.