Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017

Hon. Goodluck Asaph Mlinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ulanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Ahsante sana Mheshimiwa Mwenyekiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze moja kwa moja kwenye mjadala, japokuwa wameni-pre-empt kwa kiasi kikubwa, nitaomba niyarudie yale lakini ni kwa msisitizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu la kwanza ni ushukaji wa elimu kwa shule za Serikali za Tanzania. Kwa muda wa miaka miwili sasa Waziri wa Elimu amedumu katika Wizara hii lakini tumeshuhudia kwa uangukaji mkubwa wa shule za sekondari za Serikali. Mpaka sasa hivi anaweza akajipima yeye mwenyewe ni kwa kiasi gani ni mzuri na kwa kiasi gani ni mbaya. Kwa hili naingiwa hofu, sielewi, sijui Maprofesa wa Tanzania wana tatizo gani? Ingekuwa ushauri wangu kwa Mheshimiwa Rais, angechaguliwa mtu kama Musukuma au Mheshimiwa Lusinde ambao wameishia darasa la saba kuwa Mawaziri wa Elimu kwa sababu wanajua matatizo gani yaliwafanya wasiweze kusoma. Maprofesa wa Tanzania wamekuwa wakiongoza kutoa miongozo, matokea yake elimu zinafeli. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu matokeo ya kidato cha nne shule za Sekondari katika kumi bora hamna na ndiyo tulizoeaga Mzumbe, sijui Kilakala sijui wapi, hazipo. Katika shule 100 bora za sekondari, shule za Serikali ziko nne. Jamani, hii si aibu!

Mheshimiwa Waziri wa Elimu una kitu gani cha kutuambia hapa? Hii ume-prove failure, haiwezekani. Halafu sasa ukija unawapiga vita watu wenye shule za sekondari za private. Sasa kwa mfano hizi shule za sekondari za private tungeziondoa katika orodha ya zile shule 100, wewe si ungekuwa Waziri wa masifuri! (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo, angekuwa Waziri wa masifuri maana yake shule za Serikali zote zimefeli, shule za private ndiyo zinaongoza. Sasa ana nini cha kujivunia? Ukimwuliza tangu aingie madarakani yeye vita yake na shule za sekondari za private. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Waziri wa Elimu amekuja na nyingine, bado anawakomalia, hakuna kukaririshwa madarasa. Sasa unasema watu wasikaririshwe madarasa lakini unaruhusu watu form four wa-re-sit, ungeondoa sasa, hamna watu kurudia mitihani ya kidato cha nne. Hapo tungekuelewa! Unasema wanafunzi wasikaririshwe madarasa, unataka wawahi wapi? Wanakuhusu nini? Tunasema elimu haina mwisho. (Kicheko/ Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nikupe kwa nini wanafunzi wa shule za sekondari za Serikali wanafeli? Mazingira mabovu ya walimu. Leo hii walimu wanadai malipo yao ya muda mrefu, mnasema mnahakiki, mnataka watoe risiti. Mbona sisi Wabunge tukileta madai yetu hamtuambii tulete risiti? Mnawaambia walimu walete risiti, mnawacheleweshea malipo. Walimu mnawapangia maeneo ya vijijini, hajui akaishi vipi, nyumba hakuna, ukienda walimu wanaishi kama makondoo. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, walimu hawana break. Wote mtakuwa mashahidi, ukienda kwenye shule mwalimu anaingia saa moja asubuhi mpaka saa kumi na moja jioni kama mfungwa. Wanafunzi wanaenda break saa nne, walimu hawana. Ule muda wa break ndio anatumia kusahihisha madaftari ya wanafunzi. Hamwangalii hili!

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu udhalilishaji, leo hii mwalimu hana bosi. Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi, Afisa Utumishi, Waziri, wote mabosi zake. Huyo mfanyakazi wa namna gani? Hata sisi tungeweza? Sisi tungeweza kila mtu awe bosi wetu? Spika awe bosi wetu, Rais awe bosi wetu, sijui nani awe bosi wetu? Kwa hiyo, mnawachosha walimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine mwalimu akitaka kuhama ni msala (kazi), anaambiwa atafute mtu wa kubadilishana naye. Hebu niambie mimi nataka kwenda Dar es Salaam, naambiwa nitafute mtu wa kubadilishana Dar es Salaam. Hiyo kazi mimi nitaweza? Hiyo ni kazi ya mwajiri au mwalimu mwenyewe? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuchangishwa michango isiyo ya muhimu. Eti leo hii walimu wanaandikiwa barua na Mkuu wa Wilaya watoe michango ya Mwenge. Jamani! Mshahara wenyewe anaoupata mdogo, halafu mnamwambia atoe mchango wa Mwenge, huu ni uonevu wa hali ya juu. Mbona Wabunge hatuambiwi tuchangie Mwenge? (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, hakuna malipo ya overtime. Mimi nimetoka kwenye semina; kila semina tunayoingia tunaulizia kwanza malipo, lakini walimu wanafanya kazi mpaka weekend, lakini hawapati malipo yoyote, jamani huu ni uonevu. Halafu elimu inashuka, Mheshimiwa Waziri anakazana na shule za private badala akazane na shule zake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nihamie upande wa NHIF. Kamati imezungumzia suala la huduma za Bima za Afya kwa watu wote. Mheshimiwa Waziri wa Afya ukija naomba uniambie, NHIF haiwezi ikatoa huduma kwa watu wote, kama mashirika ya umma yenyewe ambayo yanatakiwa kisheria yajiunge kule hayajajiunga, tunawang’ang’aniaje watu wa mtaani ambao kwenye sheria haiwahusu? Tuanze kwanza na hilo. Kwa hiyo, akija Mheshimiwa Waziri wa Afya naomba aniambie, mpaka leo hii mashirika mangapi ya Serikali ambayo yameingia?

Mhshimiwa Mwenyekiti, nina taarifa za kiintelijensia kuwa BoT baada ya mimi kuongea Bungeni kuwa mashirika yote yanatakiwa yahamie NIHF wamesaini mkataba wa siri na Jubilee Insurance wa miezi mitatu, ili tukiliamsha huku Bungeni waseme mkataba unaisha keshokutwa. Kwa hiyo, sasa hivi wanasaini mikataba ya miezi mitatu mitatu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri akija naomba aniambie. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala ambalo alizungumzia Mbunge mwenzangu kuhusu vitendo vya ushoga. Jamani vitendo vya ushoga vimeshamiri katika nchi yetu. Sasa basi ubaya unaokuja, watoto wadogo wa kiume wanavyokua wanajua ushoga ni fashion na hii inayoharibu yote ni mitandao ya kijamii. Wanajitangaza sasa hivi kwenye mitandao ya kijamii, Mawaziri mnawaangalia. Sasa sijui mnataka wafanyaje? Mbona wengine wanaotukana wanawakamata, lakini wanaojinadi katika mitandao ya kijamii mnawaachia? Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Afya ukija naomba mtujibu, mmechukua hatua gani kuhakikisha ushoga hauendelei katika nchi yetu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala lingine nilikuwa sijalimalizia, Mheshimiwa Waziri hajatuambia, vile vitabu vibovu tulivyovizungumza vilivyokuwa vimeandikwa mbele nyuma na nyuma mbele, vimeishia wapi? Hatujapewa majibu na Serikali hii kuwa wale watu wamechukuliwa hatua gani? Vile vitabu vimetengenezwa vingine au vinaendelea kutumika vilevile? (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache, naomba niishie hapo kwa leo.