Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017

Hon. Vedastus Mathayo Manyinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017

MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nichukue nafasi hii kwanza kukushukuru kwa kuweza kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia kwenye hili suala linalohusiana na Kamati ya Kudumu ya Bunge inayoshughulika na masuala ya UKIMWI pamoja na Kamati ya Huduma za Jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wengi lakini vilevile na watu wengi tumekuwa haturidhiki sana na maendeleo ya nchi hii kwa maana ya mafanikio yanayopatikana. Na mimi hili limekuwa likinisumbua sana kujua hivi shida ni nini, hasa ukiangalia kwenye hii Awamu ya Tano, ni awamu ambayo kila mmoja anakubali kwamba ukusanyaji wa mapato umeongezeka, lakini vilevile kumekuwa na nidhamu ya matumizi. Hata hivyo, bado kila ukiangalia kila upande, upungufu upo, kwenye upande wa elimu, upungufu upo; afya, upungufu upo; maji, upungufu upo; na kwenye huduma zote za jamii. Ukija kuangalia upande mwingine wa bajeti, ukiangalia awamu iliyopita na awamu hii, fedha zimeongezwa maeneo mengine zaidi ya asilimia 300, mfano kwenye afya, tulikuwa tunazungumzia chini ya shilingi bilioni 50 kwa mwaka lakini leo tunazungumzia zaidi ya shilingi bilioni 200. Hizo ni fedha ambazo zimeenda kwenye afya, lakini bado kwenye elimu na kwenye maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utafiti wangu kuna jambo ambalo nimeona kama hatujalitambua wala hatuli- address ambalo nadhani kama tusipolizungumza basi tutaendelea kuathirika. Hayo maendeleo tutayategemea na bado hatutayaona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wangu ninaona kama tunahitaji ku-address suala la uzazi wa mpango. Tunahitaji ku-address suala la uzazi wa mpango kwa nini? Nitoe tu mifano michache; nakumbuka mfano mwaka 2016 pale kwenye Jimbo langu kulikuwa na uhaba wa madawati, tukatengeneza madawati yasiyopungua dawati 3,000, lakini mwaka 2017 tu mwishoni tunaambiwa kulingana na wanafunzi ambao wameendelea kujiunga, bado hizo dawati tunaambiwa tena zinatakiwa karibu dawati 3,000 nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi, kwenye shule yangu moja tu nakumbuka kule nakotoka, shule ya Nyakato, lile darasa la kwanza peke yake wamejiunga wanafunzi 800 kwenye darasa la kwanza. Kwa hiyo, ukiangalia kutokana na ongezeko la watu kila mwaka, kwa hiyo, ni kwamba chochote kile tunachokifanya lazima upungufu uendelee kuwepo. Kutokana na hali hiyo, ndio maana najiuliza, labda Mheshimiwa Waziri atatusaidia kwamba hivi ni kwa nini hili suala la uzazi wa mpango hatutaki kuli-address?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata ukijaribu kuangalia katika nchi za wenzetu, ukitafuta nchi yoyote ile ambayo inaonekana imepiga hatua au inaendelea, unakuta watoto wadogo wanaozaliwa ni wachache kuliko watu wazima. Kwa hiyo, ndiyo maana nasema kwamba nadhani tukiendelea na hali hii na kwa kutambua kwamba nchi ni ile ile, maeneo ni yale yale, kwa hiyo, kila siku itakuwa tuna upungufu mkubwa, pamoja na juhudi za Serikali ambazo itakuwa inafanya, lakini bado shida yetu itakuwa iko pale pale na bado changamoto zitaonekana kuwa bado ni kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nilidhani Serikali inahitaji ilifanye ni suala la bima ya afya. Ukiangalia hasa katika nchi nyingine za kiafrika, mfano ukienda hata Rwanda hapo, suala la bima ya afya ni compulsory.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali inajitahidi kupeleka vituo vya afya na zahanati, lakini kulingana na idadi kubwa ya watu tulionayo, kila leo zile huduma za afya unakuta ni mbovu, na kwa sababu ni mbovu ndiyo maana sisi kama Waheshimiwa Wabunge na wananchi wa kawaida tunaendelea kuona tu kwamba hakuna ambacho hii Serikali ya Awamu ya Tano inafanya, kwa sababu bado upungufu ni mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii nadhani watu wengi zaidi sasa tumejitahidi kuongeza kuzaa, kwa sababu leo una uhakika kwamba mama akipata ujauzito hata chandarua atapata bure kule kwenye zahanati. Akishajifungua mpaka miaka mitano mtoto atatibiwa bure. Akitoka hapo, kule shule ataenda atasoma bure. Kwa hiyo, mzazi kama mzazi wala haoni shida yaani anaona jukumu lake yeye ni kuzaa tu, akishazaa, Serikali itaendelea.

Kwa hiyo, ndiyo maana nasema lazima tufike mahala tuamue na tuone kwamba ni kwa kiasi gani tunaweza kuendelea. Ahsante.