Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kigoma Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. PETER J. SERUKAMBA - MWENYEKITI KAMATI YA HUDUMA NA MAENDELEO YA JAMII: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Nimesimama mbele ya Bunge lako Tukufu niweze kutoa baadhi ya maelezo na niweze kuhitimisha hoja yangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge, Wabunge waliochangia humu ndani kwa kuongea ni Wabunge 21 na Wabunge waliochangia kwa maandishi ni Wabunge 15. Nawashukuru sana mmefanya kazi kubwa ya kusaidia kuboresha report yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo makubwa yaliyoongelewa nitaomba nianze kwa sababu tuna Wizara tatu nitaanza na suala la Wizara ya Elimu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ina mambo makubwa matatu:-
(1) Mitaala
(2) Ubora wa Elimu (quality assurance)
(3) Examiner (Mtahiniwa mwenyewe)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema haya kwa sababu kila Wabunge waliochangia hapa ndani wameeleza matatizo tuliyonayo kwenye elimu na sisi kwenye Kamati tumeeleza baadhi ya mambo ambayo tunayaona yapo kwenye elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa mitaala maana yake huko utaongelea Walimu, majengo, vitabu, vifaa vya kufundishia, muda wa kusoma na wanafunzi wenyewe. Pia kwenye quality assurance ni suala la ukaguzi na baadaye tunakuja Baraza la mitihani ambalo kazi yake ni kutunga na kusahihisha mitihani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nimeanza na hili? Nimeanza na hili kwa sababu kwenye ripoti yetu tumeonesha hali ya ufaulu nchini Tanzania. Ukiangalia hali ya ufaulu kwa Tanzania kuanzia mwaka 2013, division one ilikuwa ni asilimia 2.8; mwaka 2014, division one ilikuwa asilimia 4.2; mwaka 2015; asilimia 3.0; 2016, asilimia 3.7; na 2017, asilimia 3.5.
(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia division two tulianza na asilimia 8.0; tukaja asilimia 14; tukaja 11 au 12 na sasa ni 14.9. Kwa hiyo, unachokiona kwa miaka hii yote, watoto wetu wanafaulu kwa division one mpaka three hawajawahi kuzidi asilimia 30.
Waheshimiwa Wabunge kwangu mimi hili ni kubwa sana, tunafanya nini sasa kama Taifa? Huko nyuma tulitoa maelezo sasa tuna shule za binafsi, tuna shule za Serikali. Kuna watu wamechangia hapa ukiangalia matokeo ya mwaka huu shule za Serikali katika shule 100 ni shule nne, naimi nataka nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kuleta elimu bure. Ameamua, ni uamuzi mkubwa kuleta elimu bure maana yake wazazi wa Tanzania wamepewa uchaguzi, wamepewa choice. Ukiwa mzazi una watoto wako, upande mmoja Serikali inasema zaa unavyoweza tutakusomeshea mpaka darasa la 12, upande mwingine una watoto wako unaweza ukasema mimi watoto wangu kwenye bure siendi nakwenda kuwasomesha kwa kuwalipia, ni choice Watanzania wamepewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sisi Kamati tunataka tuiombe Wizara ya elimu, Wizara ya Elimu inaboresha shule zake ni jambo jema sana. Sasa kwa wale ambao wameamua wao wenyewe, kwa mapenzi yao kuwapeleka watoto wao kwenye shule za private, wakifika pale wanasainishwa mikataba kwamba bwana wewe umemleta mtoto wako hapa, masharti yetu sisi ni haya, mtoto wako asipofaulu kwa kiwango hiki hapandi darasa, lazima alipe school fees kiasi hiki. Sasa anakuja mtoto, wazazi watoto wake amefukuzwa tunakimbilia Wizara ya elimu kuomba msaada.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilidhani Wizara ya Elimu ingesema “Mzee mtoto wako amefukuzwa? Eeeh!, Lakini mbona tuna shule za bure kwa nini usimpeleke kwenye shule za bure?” Why tunataka tuwa-punish hawa wenye shule? Mtanisamehe kwa wale ambao walisoma seminary mimi nilisoma seminary. Seminary sisi tulianza 58, waliomaliza form four ni watu 23, maana yake ni nini? Ni choice, hujapata asilimia 50 hupandi darasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie upande mwingine wa shilingi, wale ambao wanawasimamia hawa watoto ili wasome kwa bidii ndiyo hizi division one tunazoziona za asilimia tatu. Naomba Serikali hili tulitafakari kwa kina, naamini shule hizi zinasaidia Taifa letu. Sasa Serikali ifanye nini? I-set standard, ifanye monitoring, na ifanye followup, lakini Serikali isianze ku-supervise process ya hizi shule. Serikali ijishughulishe zaidi kwenye shule za Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wengi ambao wana umri wa miaka 40 kwenda juu, zamani ilikuwa usipofaulu kwenda shule ya sekondari unarudia ili uende ukasome shule ya Serikali kwa sababu shule za Serikali zilikuwa zinafanya vizuri. Zamani mtoto kwenda shule ya private ulikuwa unachekwa kijijini kwamba wewe huna akili, lakini hali imebadilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali ni muhimu sana kwenye suala la elimu mfanye consultations na hao wenye shule ili kutatua matatizo badala ya kutunishiana misuli ya kuandika waraka kama barua. Nataka niiombe sana Serikali kwenye jambo hili walisimamie vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo tumelisema kwenye Kamati yetu, Baraza la Mitihani kila mwaka wakimaliza kusahihisha mitihani wanaandika ripoti ya watoto walivyofaulu na kila somo. Niiombe sana Wizara ya Elimu na Wizara ya TAMISEMI, ripoti hizi zikisambazwa kwenda kwenye Halmashauri zetu mhakikishe zinasimamiwa zinakwenda kwa kila Mwalimu Mkuu ili aangalie hali kwa nini watoto ili mwaka ujao tuongeze idadi ya watoto waliofaulu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichopo ripoti zile kila mwaka zinaandikwa tuna-shelf kwa sababu ukienda mwaka ujao, matatizo yaliyosemwa mwaka huu, mwaka kesho yanasemwa hayo hayo. Niiombe sana Serikali hasa Idara ya Ukaguzi, wanaosimamia quality assurance report hizi ni muhimu sana ili mwaka ujao tujue tunafanya effort wapi ili watoto wetu waweze kufaulu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo tumelisema kwenye Wizara ya Elimu; narudia tena tulilisema mwaka jana na mwaka huu tumelisema, naombeni sabna Serikali mlitafakari. Umefika wakati watoto wetu wanaofanya vizuri sana darasani Mataifa yote yanatoa scholarship; Kenya kuna President Kenyatta awards, ukienda Uganda ipo, ukienda Rwanda ipo kwa nini Tanzania nchi kubwa na uwezo wetu wote huu hatuna Presidential awards? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, faida ya kuwa na Presidential awards unawafanya watoto wasome kwa bidii wakijua kwamba nikipata point three, point nne, point tano Serikali yangu itanisomesha na wenzetu wamekwenda mbali zaidi, ukienda hizo Tiger countries; China, Malaysia, Singapore watoto wote waliofanya vizuri sana wanapelekwa kwenye Western countries, kwenye heavy league universities, maana yake ni nini kule watakwenda kupata degree, watakwenda kujifunza na culture, wakirudi wanakuwa ni vijana, lakini hata wasiporudi hawa atafanya remittance nyumbani kwao. (Makofi)
Mhesimiwa Mwenyekiti, mtoto aliyemaliza degree Harvard akapata kazi Wall-street ni uhakika kama ni mtoto wa Kalinzi kijijini kwetu atajenga nyumba kijijini hata akiwa Harvard. Niwaombe sana Serikali mlitafakari angalau tuanze na watoto hata 100 huko nyuma ilikuwepo, kumetokea nini mwaka huu tumeamua kuiondoa? Baada ya kazi hii nzuri, Rais Magufuli anasomesha bure, nina hakika Serikali mkimuambia hawezi kuacha kuweka Presidential awards kwa watoto waliofanya vizuri sana regardless ni mtoto wa tajiri ama ni mtoto wa maskini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la MSD; Waziri amesema kuhusu MSD wanafanya kazi nzuri sana, ningeomba suala la MSD, sasa kazi imekuwa kubwa. Kwenye zile hospitali ambazo hasa Muhimbili na hospitali hizi kubwa za rufaa waachiwe wanunue madawa wenyewe ili MSD wahangaike zaidi na hospitali za Mikoa, za Wilaya na zahanati mpaka kwenye vituo vya afya, nina uhakika wakifanya hivyo tutaweza kufanya vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo wachangiaji wengi wamesema ni kuhusu suala la NHIF. NHIF Serikali imesema wataleta Sheria, nampongeza sana Waziri lakini Sheria hii ni muhimu ije haraka sana. Dunia ya wenzetu kwa sababu matibabu ni gharama sana kinachosaidia ni kuwa na insurance. Nadhani umefika wakati tuweze kuwa na insurance.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la kuimarisha huduma za Mama na Mtoto wanasema wao wanatafuta fedha tunawapongeza ni vizuri waendelee kufanya suala hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la kupata wahudumu; Madaktari, Manesi na Walimu. Niombe sana Wizara ya ya Utumishi suala la kuajiri watu hawa ni muhimu sana kwa sababu hali vijijini kwetu kwenye hospitali zetu za vijiji, vituo vya afya na wilaya hali ni ngumu sana. Nadhani umefika wakati tuhakikishe watu wetu wanakwenda kufanya huko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo tutachangia na tumelieleza vizuri ni suala la vitabu. Waziri ametuonesha vitabu vilivyotengenezwa, hoja yetu Kamati inasema; kuna vitabu vibovu vimeshasambazwa mashuleni, tunaomba vitabu hivyo vikaondolewe mashuleni, basi, halafu hivi vipya vipelekwe kwa sababu kuendelea kufundishia watoto wetu kwa vitabu vya zamani nadhani siyo jambo zuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali kwa suala la uboreshaji wa Chuo kikuu hasa kuanza ujenzi wa Bweni la tano na la pili ni kazi nzuri sana lakini nimpongeze Waziri kwa kusema amesema hapa hawana mpango wa kuifuta Open University, nadhani ni vizuri sana tuendelee kuinunga mkono ili iweze kusaidia maeneo ambayo tuna hakika yatasaidia kwenye elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la TBC, niiombe sana Wizara iendelee kusaidia TBC ili iweze kufanya vizuri zaidi na TBC kinachotakiwa ni uwekezaji. Naombeni, hiki ni chombo chetu, Serikali iwekeze kwenye jambo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Sheria ya BMT ni muhimu sana Sheria ya BMT ije kwa sababu ni Sheria toka mwaka 1971, haiwezekani leo miaka 47 baadaye bado tunatumia Sheria ya mwaka 1971 kwa sababu mambo ya michezo yanabadilika sana huko duniani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge, michango ilikuwa ni mingi kwasbabu ya muda siwezi kuieleza yote, lakini kwa hakika niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yenu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho hasa ambalo liko tulilisema mwaka jana naomba tulirudie, naamini umefika wakati Serikali tukatafakari tulete, tuunde Tume ya Elimu. Nasema hili la elimu kwa sababu moja tu, elimu ndiyo uhai wa Taifa lolote. Tutajenga viwanda, tutajenga barabara, tutafanya kila kitu kama Taifa letu watoto hawajaelimika tutakuwa hatujafanya jambo lolote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naamini umefika wakati twende tukaangalie mfumo wetu wa elimu in totality hata haya tunaanza kubishana private schools ni kwa sababu tu, nadhani tukishaungalia mfumo wetu katika mapana yake tunaweza kujua tunakwenda wapi kwa sababu watu wamechangia hapa tuna watu wengi sana ni unskilled labour, tunafanyaje kupata skilled labour ili kufanya hiyo kazi kwenye viwanda ambayo mmeanza nayo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili la kuanzisha Tume ya Elimu siyo la kwanza. Mwaka 1981 Rais Regan alianzisha Tume ya Elimu baada ya kuona Marekani inafanya vibaya sana kwenye elimu. Ukienda ku-google iko report tena jina lake inaitwa “A Nation at Risk” ilielezea hali ilivyokuwa mbaya inakwenda huko Marekani kwa suala la elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wao walifikia point mpaka ku-test output, watoto waliomaliza degree wanawa-test wameelimika hawa? Wakakuta asilimia 60 ya watoto waliomaliza degree hawakuelimika. Kwa hiyo na sisi leo tukiamua ku-test output yetu, ndugu zangu tutashangaana watoto wetu wengi wanamaliza kweli lakini output siyo tuliyoitarajia. Nadhani umefika wakati kama nchi tuamue kuweka Tume ya Elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba sasa nitoe hoja kutaka Bunge liweze kuyakubali na kuyapitisha yale yote tuliyoyaleta kwenye Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.