Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Vyuo Vikuu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MASUALA YA UKIMWI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa tena nafasi ili niweze kuhitimisha hoja hii ya Kamati. Kwanza napenda kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote ambao wameweza kuchangia hoja yetu ya Kamati na tulikuwa na wachagiaji jumla ya 11.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ambao wamechangia kwa maandishi walikuwa ni watano na waliochangia kwa kuzungumza walikuwa sita. Kwa sababu ya uchache wao napenda kuwatambua ambao walikuwa ni Mheshimiwa Silafu Maufi, Mheshimiwa Lucia Mlowe, Mheshimiwa Mary Muro, Mheshimiwa Rhoda Kunchela na Mheshimiwa Jaqueline Ngonyani Msongozi hawa wamechangia kwa maandishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wapo sita ambao wamechangia kwa kuzungumza ambao ni Mheshimiwa Lubeleje, Mheshimiwa Mwalongo, Mheshimiwa Mtolea, Mheshimiwa Mushashu amepongeza, Mheshimiwa Nuru Bafadhili na Mheshimiwa Bura naye amepongeza. Kwa hiyo, tunawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yenu ambayo kwa kweli michango hii ni mizuri sana na ina tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nawashukuru na Wabunge wote ambao hamkuchangia kwa sababu inaonesha kwamba mmekubaliana na taarifa na mapendekezo na maoni ya Kamati na ninyi pia tunawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Mawaziri wamechangia Waheshimiwa Naibu Mawaziri wawili, Mheshimiwa Naibu Waziri Stella Alex Ikupa pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri Antony Peter Mavunde.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Wabunge hoja nyingi ambazo wamezichangia ni hoja ambazo kwa kweli Kamati iliziona na ilizitolea ushauri na mapendekezo. Kwa hiyo haja zote ambazo zimetolewa hakuna hoja ambayo imepingana na maoni na ushauri wa Kamati katika kuishauri Serikali ili iweze kuboresha huduma hii ya masuala ya UKIMWI na masuala ya dawa za kulevya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, issues kubwa ambazo zilikuwa zimejitokeza wengi wamepongeza, lakini pia wamezungumzia upande wa ajira kwa vijana ambayo Kamati pia imeona ili kuweza kuwapatia activities ambazo zinaweza zikawapa kipato ili wasijiingize kwenye masuala ya UKIMWI na masuala ya dawa za kulevya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia masuala ya lishe ili iweze kupata virutubisho, fedha za UKIMWI kwamba ziwanufaishe wale waathirika siyo kwa ajili ya semina. Issue nyingine iliyoongelewa ni umbali wa vituo vya kutoa dawa za ARVs ambazo pia Kamati tumeiona, lakini kwa sasa hivi tunaipongeza Serikali kwamba vipo vituo zaidi ya 6,000 tukiangalia huku mwanzo ambapo tulianza na vituo 20 na baadaye tukazidi kuboresha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia suala la ushoga na usagaji na lenyewe limezungumzwa kama vinaongeza matatizo ya maambukizo ya UKIMWI. Pia na madawa ya kulevya na Kamati pia imeliona hilo na tumeshauri Serikali katika kuweza kuwa-empower hawa vijana ili waweze kujitambua na kufanya shughuli halali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, dawati la kijinsia imependekezwa kwamba zile kesi ziende haraka, pia Kamati iliona na tumeshauri Serikali kusimamia vizuri hili dawati, bajeti ndogo pia hata Kamati imezungumzia. Sera ya UKIMWI kwamba imepitwa na wakati na yenyewe Kamati imezungumzia imetoa ushauri kwamba sasa irekebishwe na kuweka program mashuleni pamoja na ndoa za utotoni
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hii ni michango ya jumla ambayo Waheshimiwa hawa Wajumbe 11 wameweza kuchangia kwa maandishi au kwa mazungumzo. Kwa hiyo hoja zao zote kwa kweli ukiangalia ni hoja za msingi kwa sababu hazitofautiani na ushauri na mapendekezo ya Kamati. Tunawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge ambao mmeweza kusisitiza umuhimu wa kuweza kuboresha areas hizi ambazo nimezitaja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shukrani za pekee sasa nizipeleke kwa upande wa Serikali ambapo Waheshimiwa Naibu Waziri Stella Ikupa pamoja na Naibu Waziri Mavunde wameweza kutoa michango yao. Kwa upande wa Mheshimiwa Naibu Waziri Ikupa yeye alijikita kwa upande wa UKIMWI, kwa hiyo utakuta mambo aliyoyazungumzia tunashukuru kwamba mmeweza kuchukua ushauri na mapendekezo ya Kamati, tunawashukuru sana, kwa sababu Kamati ilikuwa imesisitiza kwamba UKIMWI upo na kila mtu anatakiwa awe balozi kujilinda yeye na kumlinda mwingine, tunashukuru kwa Serikali kuliona hili naamini kwa njia hii fedha zitatengwa ili kutoa elimu zaidi na watu waweze kujitambua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Naibu Waziri Ikupa alizungumza kuhusu suala la sera kupitwa na wakati, amelitolea ufafanuzi tunashukuru sana kwamba mchakato unaendelea. Vyanzo vya uhakika vya Mfuko wa AIDS Trust Fund Serikali imelipokea kwa sababu sasa hivi kwa upande wa UKIMWI tunategemea asilimia 90 fedha za wafadhili, wanatumia karibu bilioni 200 kwa mwaka kununua dawa za ARV.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku wakikata ule uzi, nafikiri mnajua shughuli itakavyokuwa. Kwa hiyo, ni vizuri sasa Serikali kuanza kujiandaa mapema kuwa na chanzo cha uhakika kama tulivyosema kule kwenye Mfuko wa REA au Mfuko wa Barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali inaendelea kuchangia kweli tumeona zaidi ya bilioni moja na zaidi zimetolewa, tunapongeza sana Serikali kwa upande huu wa Mfuko wa UKIMWI, kuna wakati kulikuwa na malalamishi mengi kwa ajili ya ukosefu wa dawa hizi za septrine kwa ajili ya magonjwa nyemelezi. Hata hivyo, tunashukuru sana tulimweleza Mheshimiwa Waziri Jenista akaipokea hoja yetu Serikali imetoa milioni 600 kuweza kununua hizi dawa, tunapongeza sana Serikali kwa kuweza kupokea ushauri wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia suala la Njombe limezungumzwa Serikali imetoa ufafanuzi kwamba kulingana na survey iliyofanywa mwaka huu ilizinduliwa juzi tarehe Mosi Desemba kwamba ni kweli Njombe bado kuna tatizo. Kwa hiyo, tunapenda sana wenzetu wa Njombe kuweza kuendelea kutumia afua mbalimbali ili kuweza kupunguza UKIMWI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri Antony Mavunde alijikita kwa upande wa madawa ya kulevya. Naye amekiri kwamba bajeti ni ndogo, ambayo Kamati pia imeona kwamba bajeti ni ndogo. Pia amekiri kwamba Sera ya Taifa ya Dawa za Kulevya inatakiwa haraka sana na ametuhaidi kwamba mchakato unaendelea. Tunakushukuru sana Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuweza kuongea na Waziri wa TAMISEMI kwamba sasa zile Kamati za UKIMWI kwenye Halmashauri ziweze kuingiza dawa za kutibu waathirika wa dawa za kulevya ni vizuri sana kwa sababu kule ndiko kwenye watu. Tunashukuru pia Serikali kusema itaendelea na mkakati wa kuongeza vituo vya methadone katika Mikoa hiyo mitano ya Arusha, Kilimanjaro, Pwani, Morogoro na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru na hii ya Dodoma kwa sababu tayari ipo tayari na Mwanza basi kama mtafanya haraka tutashukuru sana itasaidia kwa sababu waraibu wa dawa za kulevya ni wengi mno.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia limezungumziwa suala la unyanyapaa kwa waraibu wa dawa za kulevya. Tunashukuru Serikali kwamba sasa Dodoma kituo hiki kitamalizika ili kuweza kutoa elimu ya ufundi. Kwa sababu changamoto kubwa wale waraibu wakishapata ile tiba wakawa vizuri, wakiwa idle hawana kitu cha kufanya, watarudia tena kule walikotoka. Kwa hiyo, tunashukuru sana Serikali kwa kuweza kufikiria kutoa elimu hii, lakini pia kuhakikisha kwamba kila Mkoa kutakuwa na dirisha maalum kwa ajili ya kutolea dawa hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawapongeza sana kwa kuongeza ile ceiling ya dawa kutoka kilo 120 hadi 300. Kwa kweli tunawashukuru sana sana kwa hii inaonesha kabisa nia ya dhati ya Serikali ya kutaka kuweza kupambana na majanga haya mawili UKIMWI pamoja na dawa za kulevya, naipongeza sana Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati yetu wameniomba nimweleze Mheshimiwa Waziri Jenista kwamba wamefurahi sana kufanya kazi na yeye, kwa sababu akija pale jinsi anavyopokea ushauri, tunashauriana mwisho mambo mengi wameyatekeleza kama Serikali, tunashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niwapongeze kwa sababu suala la UKIMWI na dawa za kulevya ni masuala mtambuka siyo ya Wizara moja, lakini nawapongeza pia Waziri wa TAMISEMI kwa kukubali sasa kwamba Kamati zile za UKIMWI ziweze kuingiza na madawa ya kulevya lakini pamoja na kutekeleza afua nyingine. Nampongeza sana pia Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa sababu kutokana na ripoti ya MSD ni kwamba dawa za UKIMWI zinapatikana asilimia mia moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli Waziri wa Afya ni mchapakazi na mara nyingi tukimpa ushauri huwa anapokea tunakupongeza sana. Pia shukrani za pekee ziende kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, walikuja kwenye ripoti yao walikuja na Jeshi la Magereza kwa kweli hili Jeshi linatakiwa liigwe, Kamati tumefanya ziara Arusha, Manyara, Njombe na Iringa, lakini ukienda kwenye vituo vya kazi unakuta kwenye Halmashauri unaoneshwa wale watu wa hali ya chini ambao wametoka tu huko kwenye mitaa kwenye vijiji na kadhalika, lakini utaambiwa tu kuna watumishi wanapata hiyo lishe nini lakini hatujawaona watumishi ambao wamejitokeza wazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, walivyokuja Jeshi la Magereza ile ripoti yao karibuvituo vingi vya Magereza kuna watumishi ambao wamejitokeza wengine zaidi ya 100, ile inaondoa unyanyapaa hata wale wafungwa mahabusu wanajiona kwamba siyo wao peke yao hili suala ni la watu wote. Tunashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Kamati tunapenda kuwapongeza Wakuu wa Taasisi hizi mbili Tume ya Kudhibiti UKIMWI na Mamlaka ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya, wanafanya kazi sana sana na wanapenda kuchukua ushauri, tunawashukuru sana. Kwa mfano, Mamlaka ya Dawa za Kulevya ni hivi karibuni tu kama sikosei Kamishna alianza kazi yake Februari, lakini ndani ya mwaka mmoja mambo yaliyofanyika katika kudhibiti dawa za kulevya ni makubwa mno utafikiri kama ni kipindi cha miaka mitano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tuchukue suala ambalo lilisumbua muda mrefu vijana wetu suala la viroba, sasa hivi vijana wako vizuri, ajali zimepungua watu huko wanasema MB zinasoma sasa! Anajitahidi sana lakini wengi wamekamatwa, wengine wamekimbia, kidogo mambo yanaenda vizuri. Tunammpongeza sana, isivyokuwa kama tulivyoshauri Serikali sasa taasisi hizi mbili mzipatie fedha za kutosha za matumizi ya kawaida na za maendeleo ili waweze kuboresha mikakati yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza Wajumbe wa Kamati kwa kazi nzuri, kwa kweli tunamshukuru sana Mheshimiwa Spika kwa sababu hii Kamati haijakaa muda mrefu, lakini sijui alitumia chujio gani kwa kweli Wajumbe walikuwa commited, walinipa ushirikiano mkubwa sana katika masuala mengi kuhakikisha tunaisaidia Serikali kuboresha mbinu mbalimbali kuhusu kupambana na masuala haya ambayo ni majanga ya madawa ya kulevya pamoja na UKIMWI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufupi ni kwamba dawa za kulevya pamoja na masuala ya UKIMWI kwa kweli ni majanga ya Kitaifa. Serikali inaweza ikatoa hata trillions za fedha lakini kama sisi wenyewe hatutabadili tabia hizi fedha hazitasaidia lolote. Kwa hiyo, lazima tuanze na mtu mmoja mmoja lakini baadaye jamii na Taifa kwa ujumla ili tuweze kupambana na hili janga kwa sababu lina madhara mengi; vifo, yatima wanazidi kudorora kwa uchumi na kadhalika gharama kwa Serikali inaongezeka kama hivi wanatoa billions of money kununua ARVs au kununua hizi Methadone.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru sana kwa Serikali kuweza kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya kupambana na janga hili la UKIMWI ingawa watu huko suala la unyanyapaa ni kubwa sana ndio maana inaweka usiri mkubwa kwa watu kutokupima afya zao. Kwa hiyo elimu ya kutosha inatakiwa kwa kweli itolewe ili watu waondoe ile dhana ya unyanyapaa, kujitambua na kuweza kupima na kutumia tiba ili itakapofika 2030, Tanzania iweze kufikia lile lengo la sifuri. Kwa hiyo, nawashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho labda niseme tu kama tip watu wengi wanasema kwamba mtu akitumia dawa muda mrefu basi hawezi kuambukiza, mimi niwaambie kwa sababu tulikuwa kwenye Kamati ya UKIMWI siyo kweli, ila ni kweli vidudu vinafubaa vinakuwa sio vingi, kwa hiyo chance ya kuambukiza inakuwa ndogo. Mimi siyo mtaalam sana lakini bado ukichukua damu yake na kadhalika unaweza ukapata UKIMWI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kitu cha msingi wengi kwa mfano, Wachungaji anaenda kupima viral load vile vidudu vikiwa chini sana haviwezi kuonekana, wanasema not detected anawapeleka watu anasema unaona hakuna, mimi sina UKIMWI kumbe ni vichache kwenye viral load, akipima CD4 itaonekana kwamba ziko kwenye normal range, atasema unaona CD4 zangu mimi ni nyingi zinatosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipimo kizuri cha kuhakikisha na kujua huyu mtu ni positive au ni negative ndiyo hicho uende ukapime status ya kujua kwamba huyu mtu kinga yake ina- react kama ni positive au ni negative tusi-rely kwenye viral load na CD4 kwa sababu zile zitaonesha kwamba mtu hana lakini vile virusi anavyo ingawa ni vichache, kwa hiyo vikipata mazingira mazuri bado vitaendelea kusambaza UKIMWI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naliomba Bunge lako Tukufu sasa liridhie taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Kamati ya Masuala ya UKIMWI, maoni na mapendekezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.