Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Makete
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. PROF. NORMAN A. S. KING: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nachukue nafasi hii kumshukuru Mungu kwa kunipa heshima ya kuchangia nafasi hii muda huu. Jambo la pili, kama wenzangu walivyosema, nachukua nafasi hii kumpongeza Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kwa kazi kubwa na nzuri anayoendelea kufanya kwa ajili ya Taifa letu hili. (Makofi)
Tatu, namshukuru Waziri mwenye dhamana hii ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, rafiki na ndugu yangu Mheshimiwa Mwigulu Nchemba kwa kazi kubwa ambayo ameendelea kufanya na wasaidizi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama kwa masikitiko makubwa sana, pamoja na kazi kubwa anayoifanya Waziri wetu, niliposikiliza pamoja na kusoma kitabu cha hotuba yake hii sijaona akisema chochote kuhusu Shamba la Mifugo la Kitulo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwalimu Nyerere pamoja na Mzee wetu Karume, mara baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kazi kubwa waliyoifanya ni kuhakikisha uchumi wa Tanzania wanaugawanya kufuata mahitaji. Moja ya walichokiamua ni kuanzisha shamba maalum la mifugo Kitulo, Wilaya ya Makete ili kusaidia wakulima wetu kuachana na kuchunga ng‟ombe, waanze kufuga, wameamua hilo mwaka 1965.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali zilizofuata ni masikitiko makubwa, hazijapeleka mkazo kwenye shamba hili. Kumbe waasisi wa Taifa hili waliona kwamba ni vigumu sana kutenga eneo la wachungaji, wakasema ili tubadilike ni lazima tuanzishe kituo cha kujifunza kufuga na shamba hili liko Kitulo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama shamba hili lingepewa haki, kwa maana ya kupelekewa fedha kwa ajili ya kuendeleza, ni wazi kabisa kwamba uchumi wa Watanzania kama walivyo wote maana Mikoa inayochunga ng‟ombe, Kanda ya Kati na Kanda ya Kaskazini wangeenda kujifunza Makete jinsi ya kufuga. Ng‟ombe mmoja wa maziwa, ni wazi fedha anazozalisha ni zaidi ya mara 20 ya ng‟ombe wa nyama kama ukithaminisha gharama za kuchunga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wafugaji na Waheshimiwa Wabunge wengine wako hapa wanajua, ng‟ombe mmoja kwa kawaida ili avunwe anachukua kati ya miaka mitatu mpaka saba. Ukichukua wastani wa miaka mitano ili umuuze, ambapo ng‟ombe wengi wanauzwa kati ya shilingi 300,000 mpaka shilingi 1,000,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikichukua bei ya wastani wa shilingi 500,000, kama ukimuuza baada ya miaka mitano, ni kwamba huyo mchungaji alikuwa analipwa shilingi 8,333 kwa mwezi, kwa miaka mitano yote aliyokuwa anachunga ng‟ombe huyo. Amemuuza ng‟ombe baada ya miaka mitano, lakini akimuuza kwa shilingi 500,000 maana yake kila mwezi alikuwa anapewa ujira wa shilingi 8,333. Ikitokea msimu ng‟ombe amedhoofu kidogo ukamuuza kwa shilingi 400,000 maana yake alikuwa anapewa mshahara wa shilingi 6,666.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi na ni lazima tufike mahali kama Serikali tuamue kwamba majibu ya kujenga uwezo wa wachungaji wa mifugo ni Shamba la Kitulo lililopo Makete. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, nyie mnafahamu, hata kama ukisema kwamba mchungaji huyu yeye kipato chake ni dola moja, yaani shilingi 2,200 basi kwa miaka hiyo mitano atatumia shilingi 5,600,000 lakini atakuwa amepata fedha ambayo ni shilingi 400,000 mpaka shilingi 500,000 kwa huyo ng‟ombe mmoja. Huyo ng‟ombe amekula shilingi 5,600,000 au shilingi 3,600,000 lakini amepata kati ya shilingi 400,000 na shilingi 500,000 kwa miaka mitano kwa ng‟ombe mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, amekula shilingi 5,600,000 au shilingi 3,600,000 lakini amepata kati ya shilingi 400,000 na shilingi 500,000 kwa miaka mitano kwa ng‟ombe mmoja. Ombi langu kwa Serikali, ifike wakati sasa ione umuhimu wa kuendeleza shamba la Kitulo, sambamba na kujenga miundombinu inayofanya shamba la Kitulo liweze kufanya kazi. Namsifu rafiki yangu Mheshimiwa Mwigulu, tulipomwomba aje kwenye shamba hili la Kitulo alishangaa sana, maana ni shamba ambalo lina ekari 12,000, ng‟ombe waliopo ni 750, shamba lina uwezo wa kuwa na ng‟ombe 4,500 na kama hii ikifanikiwa ni kila nyumba ya Nyanda za Juu Kusini itakuwa ina uwezo wa kuzalisha maziwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, chonde chonde naiomba sana Serikali, lazima tuone umuhimu wa kuenzi waasisi wa Taifa hili kwenye vitu ambavyo vinaleta uchumi chanya kwa wananchi wetu, badala ya kuenzi wakubwa hawa kwa vitu ambavyo kimsingi you can not quantify in terms of economic benefits. Ni muhimu sana! Mojawapo ni shamba la Kitulo la Makete, ardhi ipo ni mali ya Serikali, tatizo ni nini? Wanahitaji shilingi bilioni 7.7 ili shamba hili lirudi asilimia 100 kwa full fledged ni shilingi bilioni 7.7
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii pia kuchangia upande wa mbolea. Moja ya mkakati ambao hatujautekeleza vizuri, kama Serikali ya Chama Tawala ni upande wa mbolea ya ruzuku. Naomba sana badala ya kuendelea na mpango huu, ni vizuri Serikali yetu iamue kujenga Kiwanda cha Mbolea, mifuko iandikwe kabisa Not For Export, iuzwe locally kwa bei ya shilingi 10,000, kila mtu mwenye uwezo wa kulima anunue, bila kubagua nani apewe na nani asipewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mtu binafsi anajenga Kiwanda cha Minjingu pale Manyara, kwa nini Serikali isifanye hivyo? Tunajenga kiwanda kama Serikali, lakini mifuko inaandikwa Not For Export.
Kwa hiyo, kila mkulima mwenye uwezo, anakuwa na uwezo wa kununua. Utaratibu uliopo sasa unamfanya mwenye uwezo wa kulima sana asipewe. Maana Kanuni inasema, anayetakiwa kupewa ni mwenye ekari moja au mbili; ninalima ekari 500 then sistahili kusaidiwa. Sasa swali ni hili, nani ananufaisha uchumi wa Taifa hili? Bila shaka ni yule mwenye ekari nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hili, naomba niseme kidogo upande wa watendeji wetu yaani Maafisa Ugani. Vijiji vyetu vina Maafisa Kilimo, utaratibu uliopo sasa haufanyi maafisa hawa wawajibike kwa wakulima wetu.
Ombi langu kwa Serikali, Afisa Ugani wajibu wake mmojawapo uwe kuwatembelea wakulima na kujua kwamba ametembelea wakulima wangapi, atoe hesabu hiyo ngazi ya Kata mpaka Wilaya ili tuwe na hakika wakulima wangapi wamefikiwa na wataalamu wetu. Vinginevyo mtu anaweza akaajiriwa leo na asitoe ushauri kwa mkulima yeyote, bado akapata mshahara wake. Ni lazima aseme amemshauri nani? Ametembelea wakulima wangapi? Tukifanya hivyo, nchi yetu itabadilika na itafanikiwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba sana, ukitaka kufanikisha kilimo, ukitaka kufanikisha ufugaji, jibu ni shamba la Kitulo lililoko Makete. Liwe Shamba Darasa la Tanzania nzima. Mungu awabariki sana, Amina. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.