Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia. Kwanza kabisa nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri aliyoifanya. Sisi wananchi tulioteseka na machimbo na wawekezaji wakubwa wa migodi tunamwomba aendelee kukaza buti, sisi tuko nyuma yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwatake Watanzania kuuona Upinzani wetu ulioko Tanzania kuwa ni kama maigizo. Watu wanaingia humu ni kwa sababu tu pengine ya kutafuta maisha, lakini hawana nia thabiti ya kulikomboa Taifa hili. Lingine wajiulize hawa ndio Wabunge wanaowatuma kuja kuwawakilisha, badala ya kushughulika na matatizo yaliyoko kwenye Majimbo yao wanahangaika na kutetea wezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niliwahi kusema kwenye mchango wangu kwamba tunafahamu na wengine tumeshuhudia sikupata nafasi na kuwataja na wakiguna naweza kutaja, kwamba watu walivuna mpunga sasa mpunga ule jinsi ya kuurudisha inakuwa ni vigumu, kwa hiyo wanataka kufa na tai shingoni. (Makofi_

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niseme tu kwamba Mheshimiwa Rais kazi aliyoifanya ni fundisho hata kwa Upinzani. Namshukuru Mama mmoja kule nyuma amesema suala hili liwe la wote. Hata mimi nakubaliana na tumekuwa tukiomba sana sisi Wabunge wa CCM kwamba, tumuunge mkono Rais kwa jitihada aliyoifanya wakawa wanatupinga. Toka mwanzo nilimsifu sana Mheshimiwa Ole-Millya yeye aliunga mkono. Wengine wote humu mlitolewa na Mheshimiwa Ester Bulaya kama watoto wadogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kwa sababu imeonekana na Wazungu wamekubali kutulipa wanakuja humu kupiga makofi na kung’ang’ana na miongozo. Mimi niwaombe tu Wapinzani wa Tanzania mjifunze kwa kuona mfano kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri pia kwamba pamoja na kuhusiana na kodi za makinikia na sisi watu wa Geita GGM imetunyonya vitu vingi sana, tumepiga kelele muda mrefu, tunakosa support na bahati nzuri Mheshimiwa Rais anatoka kwenye Mkoa wetu. Ukiambiwa fedha tulizokwisha kulipwa kwa Geita dola milioni tatu kwa miaka miwili ukiangalia makorongo yaliyoko pale tunahitaji Serikali iunde timu ya uchunguzi kwenye mgodi pia wa GGM ambao upo Geita na watu wa Geita tunasema hatujafaidika kabisa na mgodi ule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu gani tulikuwa hatuna uwezo kama Halmashauri wa kuweza kupiga hesabu na Wawekezaji hawa. Tumekuwa tukilalamika sana, tunapewa pesa kama hisani na mtu anayetupa hesabu ndiyo TMAA ambao ni wezi wameshikwa na Mheshimiwa Rais kwamba hawafai. Kwa hiyo, tunamwomba pia Mheshimiwa

Rais aunde Tume ambayo itaenda kwenye migodi ile kuangalia kwa sababu wale tuliokuwa tunategemewa wanatupa hesabu sahihi ndiyo hao wameonekana kwenye ripoti ya Osoro kwamba hawafai, kwa hiyo, turudie hata mgodi wa GGM.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie tu ninyi ambao hamuelewi migodini baada ya kauli za Rais na yule mkubwa wa Barrick kuja, jana watu wa GGM Geita walituita tukutane wanataka kutupa bomba la maji kwa mpango wa haraka. Tumekataa kwa nini mtupe bomba la maji, tunataka tupigiwe hesabu, haiwezekani Rais anachachamaa kushika wezi sisi tunapewa maji. Tutajitwisha ndoo kichwani tutabanana na Waziri humu, lakini Serikali iunde Tume kwenda kuchunguza mgodi mkubwa wa GGM ambao una mapato makubwa na una dhahabu nyingi kuliko hata Kahama. Kwa hiyo, naomba sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, nampongeza sana Mheshimiwa Rais na Profesa Osoro amekuwa jasiri, amewataja wezi, amewataja watu waliosababisha matatizo mengine tunao CCM. Tufike mahali tuambizane ukweli tuache mizaha. Ripoti imesomwa tumeangalia watu wote wenye Degree ma- Professor na wengine ambao hatukusoma na wananchi wetu kule vijijini. Halafu watu waliotajwa Bunge kutoka CCM wanaanza kuweka kwenye twitter wanasema mimi sihojiwi mpaka nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kweli wezi wana kinga gani? Kama wametajwa ni wezi haiwezekani hata kama yuko CCM. Hili siyo suala ya mzaha kuna maisha ya watu na watu tumeumia. Watu mmetajwa Wabunge wenzangu wa CCM humu halafu mtu anaanza na heshima zake, tunamheshimu kabisa Mzee wetu humu ndani ana-twitt kwenye twitter anasema mimi siwezi kuhojiwa mpaka nipelekwe Mahakamani, yeye ni nani? Kama tunataka kumaliza matatizo haya sisi wengine tuliburuzwa sana, tuliburuzwa sana miaka iliyopita watu wakafunga mikataba wakafungia Ulaya wakagawana hela na bado wanakuja kutuletea upinzani kule kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kama kuna uwezekano wa hawa watu kama ni Mbunge kama ni nani wakamatwe. Wanaotusumbua humu ni hawa ni hao hao wametajwa kwa professa Osoro, katajwa Mheshimiwa Kafumu, katajwa Mheshimiwa Ngeleja, Mheshimiwa Chenge, wana kinga gani kama wezi? Kwani Magereza yamewekwa ya akina Babu Seya peke yake.Tufike mahali tulipiganie Taifa hili, CCM siyo kichaka cha kuja kujificha wezi. Kila mwaka mtu anatajwa, kila tuhuma, yeye ni nani. Tufike mahali tuweserious na suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nimesoma kwenye kitabu cha Waziri, ukurasa wa 55, ukisoma pale kipengele kinasema atatoza kodi ya asimilia tano kwenye dhahabu kwa wachimbaji wadogo. Halafu Mheshimiwa Waziri akasema mwishoni, anategemea kukusanya milioni
88. Hivi anaendaje kufanya pressure ya kuhangaika na wachimbaji wadogo ambao kimsingi huwezi kuishika ile dhahabu. Akiweka haya masharti kuna asilimia nne ya TMAA kuna asilimia tano ya kwake na kuna asilimia moja ya kusafirisha dhahabu, karibia asilimia 10 wakati ukienda Kampala ni one percent. Sasa kwa nini Waziri, Wizara ya Fedha wasiondoe kodi zote za kuingiza dhahabu ili tukapata na watu wanaotoka Malawi, Congo, Zambia, Uganda na Burundi wakaleta dhahabu Tanzania kwa sababu hakuna ushuru, tuka-deal na asilimia moja tu ya kusafirisha tukapata hela.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata Mheshimiwa Waziri aking’ang’ana na hizo kodi zake nilishasema humu ndani, hawezi kumshika msafirisha dhahabu tunajua tunavyobeba, kwa nini asilegeze masharti tukaweka zero halafu hii one percent atapata hela nyingi kuliko hizi milioni 88. Kwa hiyo, nashauri sana Mheshimiwa Waziri ajaribu kufikiria na alione hili suala kwa macho mawili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais na nimekuwa nikifuatilia taarifa zote hata alivyomtumbua Mheshimiwa Profesa Muhongo, sijui kama yumo humu ndani nina hamu naye kweli, alisema niliamini

vyeti, vyeti vimeniangusha! Juzi tena kasema mara tatu PhD 17. BOT hii ndiyo return yake Ma-PhD?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali tuangalie uwezo wa mtu na ikiwezekana hata Mawaziri hawa wawe wanafanyiwa hata interview, haiwezekani unakuwa na watu wana PhD za kutisha, wanapogundua wezi hao wenye PhD wanaanza kututishia sisi ambao hatuna PhD. Hata hivyo, suala hili ni halali, ziko wapi degree tunazozitegemea hapa? Watu wamebeba Dokta, PhD sijui nini, halafu mwisho wa siku tunapopata matatizo wanatutisha wanatupeleka Mahakamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Taifa hili, watu wengi hawana vyeti na watu wengi hawana elimu kwa kuwa Katiba ilisema watu kupata vyeo fulani inataka elimu kubwa wamefoji hizo digrii ambazo input yake tunaiona leo hapa. Kwa nini tusijifunze kwenye nchi zilizoendelea? Kuna nchi ambazo zimeweka watu ambao hawana hizo digrii na zinafanya vizuri. Tuking’ang’ana na hizo degree ndugu zangu tutakuja kupata matatizo, uwezo ni mdogo makaratasi ni makubwa. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nataka kushauri kuhusiana na mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Tano, hata kwenye ushauri wangu nilipochangia mwanzo nilisema…..

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)