Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi)

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika hotuba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuwashukuru wanawake wa Mkoa wa Ruvuma kwa kuniamini na kunipa kura za kishindo. Nawashukuru pia wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kwa namna ambavyo wamekipa Chama cha Mapinduzi kura za kishindo na hata Majimbo yote sasa ya Mkoa wa Ruvuma ni ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende moja kwa moja kwenye Benki ya Kilimo. Nachukua nafasi hii kuipongeza sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kuona umuhimu wa kuanzisha Benki ya Kilimo ili kuweza kuchochea hali ya kilimo katika nchi yetu na kuwafanya wananchi wake waweze kujiwezesha kwa ajili ya kukopa na kuendeleza kilimo mmoja baada ya mwingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na shughuli hiyo inayofanyika kwa maana ya kilimo, naomba niseme tu kwamba katika Mkoa wetu Ruvuma kuna mazao mengi ambayo yanalimwa katika Mkoa huo, lakini leo hii naomba Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya Kilimo, aone umuhimu wa kupeleka Benki hii ya Kilimo sasa katika Mkoa wa Ruvuma kwa sababu Mkoa wa Ruvuma ni Mkoa ambao katika shughuli zake asilimia 90 wananchi wote wanategemea kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana Benki ya Kilimo ipelekwe huko ili iweze kuwarahisishia wananchi kuweza kukopa na kuendeleza shughuli zao za kilimo, wakiwepo wanawake ambao ni wakulima na wafugaji wanaotokana na Wilaya ya Mbinga, Wilaya ya Nyasa, Wilaya ya Songea Vijijini, Wilaya ya Namtumbo na Wilaya ya Tunduru. Hawa wote wanahitaji wapate pesa kwa ajili ya kuendeleza shughuli za kilimo bila kusahau Halmashauri ya Madaba, nao pia kuna wanawake ambao wanahitaji wapate pesa kwa ajili ya shughuli za kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nisingependa kusema sana kwenye eneo hili, lakini naomba tu endapo Waziri mwenye dhamana atanikubalia kupeleka benki hii kule katika Mkoa wa Ruvuma, azma yangu ya kuondoa shilingi katika bajeti hii nitaiondoa. Vinginevyo nitaondoa shilingi ili anihakikishie kwamba benki hii sasa inakwenda kuhakikisha kwamba wale ambao ndio wanashughulika na shughuli za kilimo, ndio ambao wanasogezewa mahitaji haya. Kwa sababu Benki hii katika Mikoa mitano ambayo ni ya mfano ambao wameanza nayo ni pamoja na Mkoa wa Njombe.
Sasa jamani Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana, hivi kutoka Njombe na kufika Songea mbona ni kama pua na mdomo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, pamoja na kazi nzuri anazozifanya, wananchi wanatambua na wana imani kubwa sana na wewe, hasa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma, wanawake wa Ruvuma, naomba sana jambo hili ungelitilia mkazo ili tuweze kupata benki na wananchi waweze kufanikiwa kwa ajili ya mahitaji hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wetu wa Ruvuma pia tunalima mahindi, kahawa na korosho, ndiyo maana ninaona umuhimu wa kusisitiza, kwa maana mazao yote haya ndiyo yanayoipatia pato kubwa sana nchi yetu ya Tanzania. Kwa hiyo, umuhimu wa kupeleka benki ni mkubwa mno.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende kwenye suala la zao la tumbaku. Zao la tumbaku ni shida; kila mmoja ameongea hapa! Maeneo mengi sana ni wahanga wa jambo hili. Hata kwetu katika Mkoa wa Ruvuma katika Wilaya Namtumbo kuna shida hiyo. Tunaomba sasa kuhusu gawio ambalo linagawiwa na Wizara kupeleka maeneo ambayo watu wanalima tumbak, basi na Wilaya ya Nambumbo ipewe kipaumbele ili waweze kupata gawio.
Mheshimiwa Mwenyekiti, halikadhalika, kwa kuwa mahitaji ya tumbaku duniani yameshuka, ni vizuri sasa Serikali ikajipanga kuhakikisha kwamba zao hili la tumbaku linalimwa hapa hapa ndani ya nchi yetu na wanunue zao hili ndani ya nchi yetu, badala ya kununua tumbaku hii nje ya nchi, kwa mfano, sasa hivi inanunuliwa maeneo mengine ya nje ya nchi ikiwemo Uganda; naomba sana kwa kuwa eneo hili mahitaji yameshuka, basi mazao yatakayozalishwa juu ya suala la tumbaku, nadhani yatakidhi haja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye suala la mawakala wa pembejeo za kilimo. Kwanza kabisa naipongeza Serikali kwa kuona umuhimu wa kupeleka huduma hii ya voucher kwa wananchi wetu, baadhi yao wananufaika na wengine hawanufaiki, lakini najua Serikali yetu ni sikivu, wataona umuhimu wa kufanya marekebisho juu ya jambo hili ili wananchi wote mwisho wa siku waweze kufikiwa na huduma hii. Mawakala wetu kwenye maeneo mbalimbali katika nchi yetu hii ya Tanzania, wamejitoa muhanga kuhakikisha kwamba wameikopesha Serikali kwa kuwapa wananchi pembejeo na baadaye wanakuwa wanaidai Serikali. Wamejitolea!
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kuwapongeza sana. Naomba sasa Serikali na Wizara kwa ujumla mwone mchango mzuri ambao mawakala hao wameutoa ili kuwezesha zoezi la utoaji wa voucher uweze kwenda kwa wakati. Kwa misingi hiyo, naomba niwasemee leo mawakala wa pembejeo za kilimo. Waheshimiwa Wabunge wengi waliosimama hapa, mimi naona wamewasahau kabisa kuwasemea; ni watu ambao wamejitoa, lakini mpaka sasa hivi hawajalipwa pesa zao. Wanadai pesa nyingi na wale ni wajasiriamali ambao wanaendesha biashara zao kwa kutumia mikopo mbalimbali; wanakopa kwenye mabenki, SACCOS na maeneo mengine mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, imefika wakati sasa hivi, wale wajasiliamali wamekauka midomo. Hali ni mbaya na wengine wanadaiwa sana na hatimaye wengine tayari wanaweza hata wakafilisiwa mali zao, ikiwemo hata kuuziwa nyumba zao.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wakati unajipanga vizuri kuhakikisha unatekeleza ipasavyo Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwenye eneo la kilimo, naomba uwatazame kwa jicho la huruma sana wajasiriamali waliopo katika Mkoa wa Ruvuma, katika Wilaya zote zinazojumuisha Mkoa wa Ruvuma, tukianza na Tunduru, tukaja Namtumbo, nikaja Songea na hatimaye Mbinga na hata Nyasa. Wote wanahitaji walipwe pesa zao ili waweze kuendelea kujikimu katika maisha yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii niongelee suala la zao la samaki katika Ziwa Nyasa. Naomba nimwambie tu Mheshimiwa Waziri kwamba katika maziwa yote ambayo yanatoa samaki katika nchi hii, hakuna samaki watamu wanaoshinda Ziwa Nyasa. Ziwa Nyasa linatoa samaki watamu sana na wenye virutubisho sana na ndiyo maana ukimwangalia Mheshimiwa Jenista Mhagama, amenawiri, yuko vizuri; ukimwangalia Sixtus Mapunda naye yuko vizuri hata ukinitama mimi niko vizuri kwa sababu ya samaki wazuri na watamu wanaotokana na Ziwa Nyasa. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Kilimo na Uvuvi naomba uelekeze macho yako katika Ziwa Nyasa. Ziwa hili linatoa dagaa wazuri mno haijapata kutokea! Naomba uelekeze nguvu huko! Naishauri tu Serikali kwamba hebu oneni umuhimu... (Makofi)
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.