Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Same Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kupata nafasi hii ya pili kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na Ofisi yake. Nitachangia maeneo matatu tu. Nitaanza na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, nitakuja Wizara ya Afya na mwisho nitamalizia Ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili nitakalolizungumza, nafikiri ni jambo ambalo linamgusa kila Mbunge hapa ndani na nina uhakika linamkera kila Mbunge hapa ndani; suala la kuchoma nyavu za kuvulia samaki. Kwanza naomba niipongeze Serikali sana. Serikali inafanya kazi nyingi, inafayanya kazi nzuri sana na Watanzania wanaridhika na mwenendo wa ufanyaji kazi, kwa jinsi ambavyo Serikali inafanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala la uvuvi haramu, linanipa taabu kidogo. Wavuvi ni wafanyabiashara. Wanapokwenda kuvua na nyavu zao, mtaji wao ni nyavu zao. Suala linalonisumbua kwenye Serikali, jamani Serikali naomba mnisaidie, wavuvi hawa wananunua nyavu madukani. Wao ndio watumiaji wa mwisho. Wanapotumia kuvua wanakamatwa na zile nyavu ambazo zinazaa uvuvi haramu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu najiuliza kila wakati, kwani hizi nyavu wamezipata wapi? Suala linalonisumbua, hizi nyavu wamezipata wapi? Kikatiba Serikali Kuu ndiye anayetakiwa asimamie maendeleo ya wananchi. Aangalie wananchi wanavyopambana katika kujitafutia maendeleo. Serikali Kuu inatakiwa ihakikishe wakulima wanapata pembejeo, wanapata mbolea lakini mbolea sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inashindwaje kutafuta chanzo cha nyavu hizi ambazo ndizo zinazozaa uvuvi haramu? Swali liko hapo, kwa sababu mvuvi yule kwa ufahamu wangu mdogo, maana yake kule kwetu Same sisi hatuko kama watu wa kwenye Ziwa Victoria. Nina imani kwamba mvuvi anakwenda kununua nyavu, lakini nina uhakika Serikali inapaswa kuangalia zile nyavu kama ambavyo inaangalia pembejeo na mbolea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inanisumbua. Inakuwaje Waziri wa Mifugo anakwenda Ziwa Victoria, anakuta nyavu zilizotumika Ziwa Victoria asilimia 90 ya nyavu zile eti ni haramu? Zinatoka wapi hizi nyavu? Hawa wavuvi wanatengeneza wenyewe? Ndiyo kitu kinanisumbua. Naiomba Serikali sasa kwa sababu hili la kuchoma nyavu za wavuvi, kwanza tunachoma mtaji wa mvuvi yule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mfanyabiashara, ukinichomea mtaji wangu unaniua mimi. Naiomba Serikali ifanye kila njia idhibiti nyavu hizi ambazo ndiyo zinazaa uvuvi haramu. Iangalie hizi nyavu kule zinakotengenezwa; ina maana Serikali haijui nyavu zimetoka wapi? Kama zinaingia kwenye nchi kutoka nje, kwa nini inaruhusu nyavu ambazo zitazaa uvuvi haramu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naona tusikimbilie kuchoma hizi nyavu zikiwa kwa mtumiaji wa mwisho.
Tuziwahi hizi nyavu zinapoingia nchini. Nafikiri Serikali imenielewa. Tutamwonea mvuvi, unless kama hawa wavuvi wana viwanda vyao wenyewe vya kutengeneza hizi nyavu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali itakapokuja kutujibu, itoe jibu ambalo litatatua hili tatizo. Mwisho kabisa, tusisikie nyavu zinachomwa. Tusikie huko kwenye viwanda vya hizo nyavu au huko bandarini, nyavu zinarudishiwa huko huko. Nimeeleweka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili linahusu Wizara ya Afya. Mimi ni mwanamke ambaye nimepata watoto mara nne. Nashukuru kwa Sheria ya Nchi yangu kila nilipopata mtoto nilipata Maternity Leave ya siku 84. Namshukuru Mungu kwamba nilizaa watoto wangu salama. Sasa sheria ya nchi hii kwenye Maternity Leave iko sahihi, unajifungua mtoto, unapata siku 84 za kumwangalia mtoto mpaka anapata nguvu na wewe unarudi kazini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii sheria iangaliwe upya, kwa sababu kuna mwanamke anazaa watoto wawili, kuna mwingine anazaa pacha watatu, kuna mwingine anazaa pacha wanne, kuna mwingine bahati mbaya anazaa mtoto mwenye kichwa kikubwa, kuna mwingine anazaa mgongo wazi, watoto hawa wanahitaji uangalizi wa zaidi ya siku 84. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu aliyepata mtoto mmoja, tena mwenye afya ni tofauti sana na mtu aliyezaa kitoto njiti. Ni tofauti na mwanamke aliyezaa mtoto ambaye mgongo uko wazi. Ni tofauti na mwanamke aliyezaa mtoto mwenye kichwa kikubwa, anahitaji uangalizi wa zaidi ya siku 84. Naiomba Serikali ikaingalie hii sheria upya kuliko inavyo- generalize kwamba kila mwanamke akijifungua, 84 days anapumzika. Je, wale waliozaa njiti? Je, ambaye Mungu amempa watoto wanne? Je, ambaye amepewa watoto wawili, wameungana na wana matatizo kichwani? Siku 84 hazitoshi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali, turudi tuangalie hii sheria upya tena kwa uharaka, maana yake juzi nimemwona yule mwanamke aliyetoka pale Aga Khan, amejifungua watoto watatu na ameajiriwa na Serikali hii iliyopo madarakani, hii Serikali yetu. Hivi huyu siku 84 na watoto watatu hawa zinamtosha? Hapo nitaomba Serikali iangalie vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nirudi kwenye Wizara ya Ardhi. Hapa nazungumzia Kata ya Ndungu. Hii kata iko Wilaya ya Same. Mimi naishi next door na Kata ya Ndungu. Kata ya Ndungu ni kata yenye population, tukienda kwenye sensa ya mwaka 2012, population yake ni wananchi 16,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii kata, nakwenda kwenye ardhi kwa sababu kwa vipindi viwili nimekaa hapa Bungeni nikitetea wananchi wa Jimbo la Same Mashariki. Hili suala nilikuwa naliongea, kwamba nusu ya ardhi ya Kata ya Ndungu, ardhi yake ina mwekezaji sijui wa mkonge lakini ule mkonge hauendelezwi. Nililalamika hapa Bungeni, Waziri wa Uwekezaji wa kipindi kile Mheshimiwa Mama Maria Nagu, akaja akaona ile shida, akaona kwamba kwa kweli pale kuna tabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, asilimia 60 ya wananchi 16,000 ni vijana, hawana ardhi, hawana mashamba, hawana makazi, ardhi yote iko kwa mwekezaji ambaye ule mkonge hauendelezi, upo tu. Namsihi Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, yupo Mheshimiwa Mama Angelina, aje Ndungu akaione ile ardhi ambavyo iko pale, hakuna kinachotokea, vijana wa Kata ya Ndungu hawana nyumba, wanaishi na wazazi wao. Anaoa mke, anakaa na mama yake na baba yake. Ndoa itavunjika ile; gubu la mama mkwe! Anataka ajenge nyumba yake, hana mahali pa kujenga. Mkonge umekufa, nusu ya ardhi ya Kata ya Ndungu. Nafikiri Serikali imenisikiliza. Sikuwa mtata sana, nimeeleweka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja.