Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kiembesamaki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HASSANALI MOHAMEDALI IBRAHIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Kwanza sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunifikisha hapa Bungeni salama nikiwa na afya nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri aliyowasilisha leo asubuhi hapa Bungeni. Kabla sijakwenda huko, kwanza nitakuwa mwizi wa fadhila kama sijachukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli. Haya tunayozungumza hapa Bungeni kujadili bajeti mbalimbali za Wizara zote, huu ni mkakati ya Mheshimiwa Rais kwa kukusanya kodi. Ndiyo maana leo tuko hapa kifua mbele kuzungumzia bajeti zetu za Wizara mbalimbali ikiwepo bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kumwambia Mheshimiwa Rais kwamba sisi Wabunge wa CCM tuko nyuma yake na tutakuwa nyuma yake mpaka atakapomaliza kipindi chake 2025. Nasema hivi kwa sababu gani? Sisi wote hapa ni mashahidi wa Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli anapofanya kazi kwa bidii, upendo na uzalendo katika kuwasaidia Watanzania waliokuwa wanyonge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda kwa sababu siwezi kuyataja mambo yote, nitaje mambo mawili matatu ambayo Mheshimiwa Rais katika kipindi kifupi alichokuwa madarakani ameweza kununua ndege ATC, ameanza vilevile kutujengea reli ya SGR (Standard Gauge Railway); ukusanyaji wa pesa wa mapato ambayo ni historia katika nchi hii katika awamu zote zilizopita, Awamu hii ya Tano, kwa kweli pesa zinazokusanywa na TRA kwa sababu mwenyewe Mheshimiwa Rais anafuatilia hilo suala, limekuwa historia ya TRA wanakusanya pesa kwa wingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika ujenzi wa bomba la mafuta, tumeona Mheshimiwa Rais alivyojitahidi na vilevile ufuaji wa umeme ambapo hata juzi hapa Mheshimiwa Rais amekwenda kuzindua Kinyerezi ambayo tutapata megawati 2,500. Hayo ni baadhi ya mambo tu, siwezi kuyataja yote lakini nampongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mambo haya anayofanya naweza kuwaambia Wapinzani 2020 Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli hana upinzani nchi hii. Kwa utabiri wangu huu Waheshimiwa Wabunge wa CCM watakuja kuniambia, Mheshimiwa Raza kweli asilimia ambayo Mheshimiwa Rais atapata ni zaidi ya 90. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, mambo anayofanya Mheshimiwa Rais, vilevile nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kumteua ndugu yangu Mheshimiwa Kassim Majaliwa kuwa Waziri Mkuu wa Awamu hii ya Tano. Niseme kwa sababu gani nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kumteua Mheshimiwa Waziri Mkuu; kwanza Waziri Mkuu wetu masha Allah ni handsome. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua Mheshimiwa Waziri Mkuu ana hadhi ya kipekee ninapokwenda popote, basi huna haja ya kumwambia mtu huyu ndio Waziri Mkuu wa Tanzania, anajulikana tu. Sifa nyingine ambayo Waziri Mkuu anayo, kwanza ni mtu makini sana, mwenye busara, mwenye upendo, mchapa kazi, kwa ufupi tunaita kwa kizungu all- rounder. Mheshimiwa Waziri Mkuu hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze vilevile dada yangu Mama Mary kwa kukupata mtu kama wewe, hii pia ni sifa kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tuje katika bajeti hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Nimefuatilia bajeti hii, nimeona ni bajeti ambayo ni ya matumaini na hususan Mheshimiwa Waziri Mkuu nakupongeza kwa kusimamia masuala ya mbolea na mbegu bora. Kama tunavyojua, nchi yetu ya Tanzania asilimia kubwa sana ni wakulima na wafugaji. Kwa hiyo, naomba vilevile haya masuala ya upatikanaji wa mbolea yawe ni endelevu kwa sababu tukiwa na mbolea nzuri na mbegu nzuri, tutapata matunda mazuri na wakulima watapata nguvu na watakuwa na imani na Serikali yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nataka nipongeze kwa kuongezwa bajeti kwenye Wizara ya Afya kwa kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu. Hapa nimesoma na nimeona kwamba imeongezwa mpaka kufikia shilingi bilioni 269. Hii inaonesha Serikali ilivyokuwa makini katika kuwasaidia Watanzania ambao ni wanyonge na maskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upatikanaji wa umeme, napongeza vilevile kwa sababu umeme ni kitu muhimu sana katika nchi hii. Bila umeme hakuna viwanda, hakuna chochote. Kwa hiyo, Mheshimiwa Rais anapokwenda na speed hii na naamini Mheshimiwa Waziri Mkuu yuko nyuma yake kumsaidia ili kuona kwamba baadhi ya vijiji ambavyo havijapata umeme, natumaini mpaka mwaka 2020 hivyo vijiji vitafikiwa na umeme ili wananchi wetu nao wapate kumwona Mheshimiwa Rais angalau katika kuangalia TV zao na kusikiliza redio zao. Hiyo ni moja katika maendeleo ya nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jiji la Dar es Salaam, naweza kusema ni kioo cha Tanzania, kwa sababu watalii wote, wafanyabiashara wakubwa wote wanakuja katika Jiji la Dar es Salaam. Leo Mheshimiwa Waziri Mkuu kuna baadhi ya sehemu Dar es Salaam huwezi ukapita usiku kama hujaziba pua. Kwa sababu kuna watu wanalala, kuna watu wanaoga, kuna watu wanafanya choo hapo hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninao ushahidi kwenye simu yangu kwamba watu katika mitaa fulani Dar es Salaam wanachafua mazingira kabisa, yaani mazingira yanakuwa machafu sana. Sehemu hiyo siyo kwamba wanalala watu wawili au watatu, wanalala watu 50 na kuendelea. Ushahidi huo ninao kwenye simu yangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, Jiji letu la Dar es Salaam liangaliwe kuhusiana na mazingira yetu kwani haya mambo yamepita kiasi. Watu wanaoga kabisa, wanachukua maji wanachota wanaoga hapo hapo, wanafanya haja zao; haileti picha nzuri sana. Naona iko haja kwa Mkurugenzi wetu wa Jiji Dar es Salaam kuliona hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais kama atanipa nafasi kuwa Mkurugenzi wa Jiji wa Dar es Salaam kwa muda wa wiki mbili au tatu, nitafanya kazi hiyo kwa wiki tatu na mtaiona Dar es Salaam itakavyokuwa safi. Naamini huyu Mkurugenzi aliyekuwepo sasa hivi, baada ya kusikia maneno haya, atajirekebisha na atafanya yale ambayo yanastahiki katika jiji letu la Dar es Salaam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo mengi ya kuzungumza…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MHE. HASSANALI MOHAMEDALI IBRAHIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.