Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Mbaraka Kitwana Dau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa fursa hii. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba hii nzuri leo asubuhi, nielekeze pia na pongezi zangu kwa Mheshimiwa Rais kwa namna anavyokitendea haki Kiti chake nasi Watanzania tunampa pongezi nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu Septemba, 2016, alifanya ziara katika Kisiwa cha Mafia, ziara yake kwa kweli imetuletea faraja kubwa sana na changamoto nyingi sana ambazo zilikuwa zinatukabili katika kisiwa chetu aliweza kuzifanyia kazi na kuzitatua. Hata hivyo, alipoondoka aliacha viporo kama vitatu, vinne hivi na tukakubaliana kwamba atatuita Ikulu twende tukaongee kuyamaliza haya mambo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa nianze kwa kumkumbushia Mheshimiwa Waziri Mkuu viporo hivyo. Suala la kwanza leo asubuhi lilizungumzwa hapa. Suala la tatizo la X-Ray la Kisiwa cha Mafia unaingia sasa mwaka wa sita Mafia hakuna X-Ray na unaingia sasa mwaka wa pili toka Mbunge wa Mafia anayeongea sasa hivi alete X-Ray yake mwenyewe mpya ambayo haijafungwa mpaka leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri asubuhi hapa ameliambia Bunge lako kwamba Kampuni ya Philips italeta mashine za X-Ray kwa ajili ya hospitali za mikoa mwezi Juni na wao ndiyo wanawajibika katika kuzi-maintain kwa maana ya kufanyia matengenezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nisingetaka kwenda mbali sana, namwomba sana Mheshimiwa Waziri badala ya kusubiri hizo X-Ray za ku-import kutoka nje awaambie Philips kwanza wakatengeneze X-Ray ya Mafia mwaka wa sita huu haijatengenezwa. Hili halihitaji kusubiri Juni kama wao wapo hapa basi waende wakaitengeneze X-Ray ya Mafia, kwa sababu imekuwa haifanyi kazi kwa miaka sita na mimi leo ndiyo mara yangu ya mwisho kulisema hili jambo ndani ya Bunge hili, nitakachokifanya baada ya hapa nakijua mimi mwenyewe. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo Mheshimiwa Waziri Mkuu tulimfikishia kilio chetu ni tatizo la mgogoro baina ya hifadhi ya bahari ya Mafia na Halmashauri ya Mafia. Ningeomba sana ndugu yangu Mheshimiwa Ulega nilimwona Mheshimiwa Waziri Mpina ametoka, lakini Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Abdallah Ulega namwona naomba anisikilize vizuri kwa sababu alikuja Mafia ameliona hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Mafia ni Halmashauri ndogo sana na maskini, ina vyanzo vya mapato vichache sana, kuna Taasisi inaitwa Hifadhi ya Bahari. Ni taasisi ambayo staffing yake haizidi hata watu 15 lakini wanakusanya mapato kwa maana ya maduhuli kutokana na watalii wanaokuja kutembelea Kisiwa cha Mafia zaidi ya milioni 700 kwa mwaka na Halmashauri ya Mafia tunapewa asilimia 10. Halmashauri ya Mafia yenyewe kwenye vyanzo vyake vingine vyote inakusanya shilingi milioni 600. Utaona pana tatizo hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taasisi ndogo tu ambayo staffing yake haizidi hata watu 15 inakusanya shilingi milioni 700 lakini Serikali kwa maana ya Halmashauri ya Wilaya ya Mafia ambayo ndiyo inawajibika na shule, inawajibika na Zahanati, inawajibika na Hospitali na wakati ule barabara na mambo mengine maji na vitu kama hivyo tunakusanya shilingi milioni 600. Eneo la utawala la Mafia limepunguzwa na Taasisi ya Hifadhi ya Bahari ya Mafia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunachokitaka na bahati nzuri Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuja tuliliongea hili na akaahidi kwamba tutakutana Ikulu pale tuliongee tulimalize pamoja na Mawaziri wanaohusika. Ningeomba kwa namna ya kipekee sana hatuombi jambo kubwa, tunachoomba kwamba ule mgao basi angalau uwe wenye kufanana. Sisi ambao tuna mambo makubwa ya kuendesha tupate mgao mkubwa tupate asilimia 60 na hii hifadhi ya bahari ipate asilimia 40, kwa sababu kuna hatari Halmashauri ya Mafia ikapelekwa kule kwa Mheshimiwa Ungando, Kibiti kwa sababu hatuwezi kufikia malengo ya kukusanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pesa zote zinakwenda kwenye Taasisi ya Hifadhi ya Bahari ambao hawawajibiki na jambo lingine lolote la maendeleo ya Mafia zaidi ya uhifadhi na Halmashauri nayo pia inafanya kazi ya uhifadhi. Ningeomba kwa namna ya kipekee sana kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu suala hili la kikao kile, tukutane ili tuliweke sawa na suala la kanuni wala siyo suala la sheria ni Waziri mwenye dhamana ya uvuvi na mifugo abadilishe kanuni tuanze kupata sasa Halmashauri asilimia 60 na Hifadhi ya Bahari asilimia 40. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lingine, tulilalamika kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu kuhusu Hifadhi ya Bahari wanaacha kazi yao msingi ya uhifadhi na wameiingia katika masuala ya kuuza na kumiliki maeneo na wameuza visiwa. Kisiwa cha Shungimbili kimeuzwa na sasa pale kuna hoteli ya nyota saba kwa usiku mmoja ni dola elfu kumi (10,000). Kwa taarifa kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, Halmashauri ya Mafia haipati hata single cent kwenye mapato haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ndiyo mambo ambayo tungependa tukae na Mheshimiwa Waziri Mkuu tuyaongee, haiwezekani wao kazi yao kuhifadhi badala ya kuhifadhi wanauza maeneo na wanapouza maeneo hata huo mrabaha sijui kitu gani ambacho pengine Halmashauri tungestahili kupata hatupati hata kitu kimoja. Huu sasa unafika mwaka wa pili toka uwekezaji ule ufanywe pale na Halmashauri ya Mafia hatujapata hata senti tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulitoa kilio chetu cha usafiri Mafia kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu na naamini Waziri Mbarawa sijamwona lakini nimemuona Mheshimiwa Injinia Nditiye hapa. Nilikwenda kwake, tuna dhiki ya usafiri katika kisiwa cha Mafia, maeneo mengine tunaona watu wanajengewa vivuko na Serikali, tumejitahidi sana kuishawishi private sector watuletee boti zao binafsi hawajavutika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaiomba Serikali kwa namna ya kipekee kabisa ichukue nafasi yake watutengenezee chombo, kule tuna sege tuko kama kwenye cage hatuwezi kutoka lazima tuvuke bahari. Hata hivyo, wanawajengea vivuko watu wengine sitaki kuwataja hapa wanajenga vivuko maeneo mengine ambayo yanapitika kwa barabara, sisi hatuna namna ya kutoka au kuingia Mafia lazima tupite kwenye kivuko, kivuko ambacho kinagharimu bilioni mbili mpaka tatu, hawataki!

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri Mbarawa ameniahidi kwamba kwenye bajeti hii ataingiza hilo. Sasa nataka atakapokuja kujibu hotuba hii aniambie na Mheshimiwa Nditiye nimemwona watuambie watajenga kivuko mara hii au hawajengi na Mheshimiwa Waziri wa Fedha atusaidie katika hilo kwa sababu imeshafika wakati sasa ni wakati wowote kule ni kama timing bomb, yale magogo tunayosafiria yale ambayo siyo salama wakati wowote yatazama na watu watapoteza maisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifikia hapo tunasema Mheshimiwa Nditiye, Mheshimiwa Mbarawa, Waziri wa Fedha mtakuwa masuulu, masuulu ni neno la Kiarabu, maana yake mtakuwa responsible na hiyo dhambi, kwa sababu wanawapandisha watu katika magogo, pesa wanatenga katika maeneo ambayo hayana ulazima wa kupata vivuko vya kisasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo lingine pale, Mafia ni eneo dogo sana, kuna viboko wametoka kwa Mheshimiwa Ungando wamekuja Mafia pale, wameshafikia 40 sasa hivi. Kilio hiki tumekisema toka alipokuwa Waziri Mheshimiwa Maghembe, wanakula mipunga ya watu, wanakula mazao ya watu na kilio tumekileta Wizarani.(Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kibaya zaidi wiki mbili zilizopita, Mwenyekiti wangu wa Kata wa CCM, Kata ya Ndagoni ameuawa na kiboko. Tumetoa taarifa mpaka leo wataalam wamekwenda pale badala ya kuwafanya utaratibu wa kuwavuna au kuwafanyia relocation wale kwa sababu Mafia eneo ni dogo hawawezi kukaa. Wapigeni sindano walale muwahamishe muwapeleke huko Rufiji, ndiko kwenye origin yao, pale sisi nafasi yetu ni ndogo. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashangaa wamekuja wataalam pale wameishia kupiga picha, je, nami namwuliza Mheshimiwa Hasunga anasubiri mpaka watu wangapi wafe na viboko ndiyo watakuja kuwaondoa wale viboko pale Mafia. Hili nalo pia na yeye pia utakuwa masuulu. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la umeme na nashukuru nyuma yangu yupo Profesa hapa. Suala la umeme vijijini, Profesa alituahidi lakini leo hayupo, naamini Serikali ni moja. Walituahidi kwamba visiwa vidogodogo vyote vitapata umeme unaotumia nguvu ya jua kwa maana ya solar. Kisiwa cha Jibondo, Kisiwa cha Bwejuu, Kisiwa cha Juani na Kisiwa cha Chole. Mheshimiwa Dkt. Kalemani ahadi hii naye alinihakikishia kwamba tutapata umeme mpaka sasa sijaona dalili zozote, naye pia atakuwa masuulu. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la barabara, Kisiwa cha Mafia siyo kidogo hivyo, kuna barabara ambayo ina urefu zaidi ya kilometa sitini paleā€¦..

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Dau.