Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Hawa Abdulrahiman Ghasia

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mtwara Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uhai na afya na kuweza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu ili niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwanza napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri ambayo ameitoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo najielekeza katika masuala matatu, Suala la kwanza ni suala la Hospitali ya Rufaa kanda ya kusini, ambayo tayari ujenzi wake ulishaanza, mapokezi tayari, OPD umeshakamilika, ukuta umejengwa lakini kwa zaidi ya miaka miwili mfululizo pesa zinawekwa kwenye bajeti lakini hazitolewi. Sasa kama makusanyo ni matatizo basi wote tugawiwe sawa, sio wengine wanapewa asilimia 80, wengine asilimia 60, wengine sifuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala la pili ambalo nataka kulizungumzia ni suala la uwanja wa ndege wa Mtwara. Kwa zaidi ya miaka mitatu umekuwa ukisindikiza viwanja vingine. Tumekuwa tukiwekewa pesa tukiambiwa kwamba utawekewa taa na utafanyiwa ukarabati kwa sababu upembuzi yakinifu umekamilika, lakini kila mwaka pesa ile inatengwa na inatoka sifuri. Kwa hiyo, nataka niombe kama hakuna pesa ambayo inatakiwa kupelekwa katika kitu chochote aidha hospitali au uwanja wa ndege wasituwekee kiini macho halafu hatuwekewi kitu chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu ambalo ndio ningetaka nichukue muda mrefu ni suala la pembejeo la zao la korosho. Korosho kwetu sisi wananchi wa Mtwara, Lindi na Ruvuma, ni uchumi lakini pia ni siasa. Katika miaka mingi iliyopita katika mkoa wetu wa Mtwara tumekuwa na
utaratibu wa kuwa na Mifuko yetu ya ngazi ya Wilaya na Mikoa kwa ajili ya pembejeo za mazao yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2017 Mheshimiwa Waziri wa Kilimo akaja akawatangazia wananchi kupitia mkutano wa wadau wa korosho kwamba pembejeo zinatolewa bure na akaelekeza wale ambao waliokuwa wamechangia kupitia katika Mifuko yao werejeshewe zile pesa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna Mbunge ambaye aliomba tupewe pembejeo bure na hata kwenye kikao vya wadau baadhi ya wananchi walikuwa wanapinga wakiamini kwamba suala hili halitakuwa endelevu. Cha kusikitisha mpaka sasa hivi hatujui pembejeo za korosho zitapatikana kwa utaratibu upi mpaka dakika hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, upuliziaji wa zao la korosho unatakiwa kuanza mwezi wa tano mara nyingi na kila baada ya siku 21 na unatakiwa urudie mara tano mfululizo kila baada ya siku 21 na ukichelewa mara ya kwanza maua yanapotea na uzalishaji unashuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, ametuambia hapa kwamba kwa mara ya kwanza kilimo kimeongezeka kwa asilimia sita ukuaji wa pato linalotokana na kilimo imekuwa kwa asilimia 3.6, kwa mara ya kwanza. Kilichochangia ukuaji huo ni zao la korosho, kutokana na uzalishaji kuongezeka lakini pia kutokana na bei ya korosho kuongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku zote tumekuwa tukisema kwamba uchumi wa nchi unakua kwa asilimia saba mfululizo kwa zaidi ya miaka 10, lakini ukuaji ule hauonekani kwa wananchi kwa sababu sekta zinazokuwa si sekta ambazo zinaajiri wananchi wengi na sekta inazoajiri wananchi wengi ni kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uelewa wangu na kwa ufahamu wangu na kwa uchumi wangu ambao niliusomea, nilitegemea Serikali yangu kwa kuwa zao la korosho mwaka jana lilifanya vizuri, kwa hiyo, mipango ya pembejeo na maandalizi mengine yangefanyika mapema na wakulima wangekuwa na uhakika kwamba kwenye pembejeo za korosho wanazipata kwa utaratibu upi na wanazipata lini. Sasa zao ambalo limezalisha vizuri ndio ambalo mwaka huu tumeamua hatutaki kuwekeza kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli nioneshe masikitiko yangu. Zao la korosho na mazao mengine tulipitisha sheria hapa tukaanzisha Mifuko ya kuendeleza mazao yakiwemo korosho, kahawa, pamoja na pamba na mazao mengine. Mfuko wa Korosho mpaka sasa hivi tunavyozungumza una zaidi ya bilioni 88 za msimu 2016/2017 kwa ajili ya kuendeleza zao la korosho, ikiwa ni pamoja na ubanguaji, utoaji wa miche bora, suala la pembejeo na suala la utafiti katika kituo chetu cha Naliendele, lakini pesa hizo mpaka sasa hivi hatuelewi. Pesa hizo tulitunga sheria hapa ya mwaka 2009 na marekebisho yake ya mwaka 2011. Sheria haijafutwa na Bunge hili, tunaanzaje kuzuia pesa hizo wakati sheria hatujabadilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, msimu wa mwaka 2016/2017 zao la korosho, korosho zilizalishwa tani 265,237,845 zenye thamani ya Sh.871,462,989,287. Msimu wa 2017 uzalishaji umeongezeka mpaka tani 313,530,700 zenye thamani ya shilingi trilioni moja, kutoka bilioni 871 mpaka trilioni 1.189. Wananchi wamepata zaidi ya trilioni moja, hiyo trilioni moja imeenda kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa mkoa wa Mtwara peke yao wamepata bilioni 705,399,000,000. Halmashauri msimu wa mwaka 2017 zimepata bilioni 8.2, msimu 2016/2017 walipata bilioni 11 kwa sababu viwango vya tozo vimepungua. TRA yenyewe ilipata msimu wa 2016 zaidi ya bilioni 103 kwenye zao la korosho. Hivi kwa mafanikio haya nilitegemea Serikali yangu itumie kila aina ya juhudi kuhakikisha kwamba zao hili sasa linawezeshwa ipasavyo ili kuhakikisha kwamba uzalishaji unaongezeka mwaka hadi mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nioneshe masikitiko yangu, tangu mwaka 2017 mwishoni mwezi Desemba, tumeenda kumtembelea Waziri wa Fedha Wabunge wote wa Mtwara zaidi ya mara mbili. Tumeenda kwa Katibu Mkuu, mara ya kwanza wakatuambia kwamba pesa zipo msiwe na wasiwasi tatizo ni kwamba hii sheria tangu imetengenezwa haina kanuni. Tumekaa tukapitisha kanuni. Tukaambiwa Bodi hawana mpango kazi wala mpango wa manunuzi, wametengeneza imeenda. Sasa hivi tunaambiwa inatoka milioni kumi na bilioni kumi yenyewe kizungumkuti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri Mkuu ametoka kwenye korosho, anaijua korosho naomba korosho isimfie mikononi mwake. Anafahamu katika utaratibu wa kawaida sasa hivi meli za kuleta pembejeo zinapaswa kuwa zimefika. Hata hivyo, ninachoomba Waziri wa Kilimo na Waziri wa Fedha waende Mtwara, waende Lindi, waende Ruvuma wakawaambie wananchi kwamba pembejeo mwaka huu hawatapata kwa sababu walituahidi watazitoa.