Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, lakini na mimi napenda kupongeza mzungumzaji aliyetoka kuzungumza sasa kwa kutimiza wajibu wetu kama Wabunge kwa kuwa ni muhimili unaojitegemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia hotuba ya Waziri Mkuu cha kwanza tunaangalia uhalisia wa Watanzania. Tukitazama uhalisia wa Watanzania tumeangalia jambo la msingi ambalo ni maisha ya kawaida wanayoyaishi kila siku. Maisha waliyonayo Watanzania hayaendani na hiki kilichosomwa au kilichoandikwa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, hali ya maisha ni ngumu sana. Tunapozungumza kwamba hali ya uchumi ni nzuri wakati Watanzania hali yao ni mbaya, tunaomba hayo maandishi yaende kwenye uhalisia kwa Watanzania, hali ya maisha haifanani na kile kilichoandikwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia ajira mpya tunatazama vijana wengi ambao wamemaliza vyuo wapo mtaani. Leo vijana wetu wanajiingiza kwenye vitendo mbalimbali ambavyo si makusudi yao, ni maisha. Leo tumetazama taarifa mbalimbali hasa kwa jana, yaani imefikia mahali mpaka makanisani sadaka zimeanza kuibiwa. Hatutasema ni vijana peke yao ndio wanaoiba, lakini ni vyema Serikali ikajielekeza kwa kuangalia kundi kubwa la Watanzania ambalo ni vijana linawapeleka wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi viongozi wetu wapo Segerea, tumeenda kutazama kule robo tatu ya wafungwa waliopo kule ni vijana, na hapo inajidhihirisha kabisa kwamba Tanzania suala la ajira imekuwa ni kidonda ndugu sasa. Ni vyema kama tunategemea kuleta amani tunayoizungumza kwenye Taifa letu tukatazama kundi kubwa la Watanzania na tukatafuta suluhu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natoka kwenye Mkoa wa Rukwa ambao tunategemea kilimo, kilimo hicho ninachokizungumza ndicho ambacho Watanzania wengi tunategemea kuendesha Taifa. Leo wamesimama Wabunge wengi wakazungumzia kuhusu ununuzi wa ndege, si jambo baya, lakini ni wakati gani umenunua na je ndio uhitaji mkubwa wa Watanzania? Watanzania wangapi ambao watafaidika na hiyo ndege? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati anaulizwa Mkurugenzi wa ATCL leo amesema nje ya kupanda ndege Watanzania watanufaika kuuza vipuli; mambo haya ni fedheha kwa Watanzania. Ni kweli ndege ingenunuliwa lakini kwa kuangalia kipaumbele cha Taifa letu ni ndege? Ni kweli taifa letu kipaumbele cha kwanza ni ndege?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapouzungumzia Mkoa wetu wa Rukwa ukiacha suala la usafiri wa anga kuna usafirishaji wa majini. Amezungumza Keissy pale kuhusu meli, hiyo meli imekuwa ni wimbo. Meli ile ingewasaidia Watanzania wa kawaida hata kufanya biashara, kutoa mazao yao Mkoa wa Rukwa na maeneo mengine kupeleka hata nchi ya Congo; lakini leo ni Mtanzania gani wa Rukwa atakuja kupanda ndege hiyo iliyoletwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mkumbuke unapozungumzia ndege huzungumzii wananchi wa Dar es Salaam, unazungumzia wananchi wa Taifa la Tanzania na hizo ni kodi za Watanzania wote. Tungeomba mambo ambayo tunakuwa tunazungumza kama Wabunge yachukuliwe kama vile tunavyozungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inafikia mahali tunapata shida sana, kwamba hivi tunazungumza kwa kutimiza wajibu au tunazungumza kama mhimili ambao tunatakiwa tuisimamie Serikali? Kwa sababu yale tunayozungumzia hayawezi kwenda kama vile tunavyozungumza na mnakuja hapa matokeo yake sasa watu wamejaa hofu. Niwaombe Mawaziri, hata Mungu ni mkubwa lakini ana washauri wake ambao wako chini sana, Malaika; kaeni na Mheshimiwa Rais mumshauri uhalisia wa Taifa letu na Watanzania wanakabiliana na nini. Mkiwa waoga tukija hapa tutazungumza kumbe mkifika kule mnakuwa na hofu mnashindwa kutimiza wajibu wenu wa kumshauri Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumza hivi, kabla hatujapitisha bajeti tayari bei ya petrol imepanda, bei ya mafuta ya taa imepanda, bei ya dizeli imepanda. Sasa unaanza kujiuliza huu uchumi uliokuwa ina maana shilingi ya Tanzania imeshuka thamani. Sasa hii tunayozungumza hapa Mheshimiwa Waziri Mkuu, najua hata mama yangu ameondoka lakini yupo Naibu Waziri pale; tunapozungumza kama Wabunge angalau basi muwe mnafungua masikio mnatusikiliza tunachokizungumza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulisema hapa, tulizungumzia mambo ya petroli hapa, tulizungumza mambo ya mafuta ya taa; hivi leo ukipandisha bei kwenye petroli unategemea Watanzania wangapi wanaoathirika? Hiyo inakwenda kuwaathiri moja kwa moja Watanzania wa chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wajibu wa Serikali kuhakikisha Watanzania wanaishi vizuri kwa kupewa mambo yao ya msingi. Mlipo kuja hapa mkazungumza, Mheshimiwa Waziri Mkuu alisimama kama Waziri, kama Kiongozi wa Serikali akazuia wakulima wasipeleke mazao yao nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli ni haki yenu na ni wajibu wenu kama Serikali kuhakikisha taifa lisipate njaa, lakini kama unaweza kupata nguvu ya kuzungumza kuzuia kwa nini usipate hiyo nguvu ya kuhakikisha Watanzania wanapata soko la uhakika la kuuza mazao yao? Kama hatujui pembejeo zao, yaani mpaka Mheshimiwa Rais anaweza kuzungumza kwamba sasa mnataka mbolea ziende wakati Waziri wa Kilimo yupo, tafsiri yake ni nini? Waheshimiwa Mawaziri wote mmeshindwa mpaka yeye aseme? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima hawa tumeenda kuwahamasisha, Mheshimiwa Rais amezungumza watu wafanye kazi, tumeenda kuwahamasisha wafanye kazi, wamekwenda kuchukua mikopo benki, wamezalisha kilimo cha kisasa, wakazalisha kwa wingi. Matokeo yake hivi ninavyozungumza kuna wakulima wameuziwa nyumba zao, kuna wakulima wanadaiwa na benki kwa sababu ya uzembe wa Serikali. Kwa sababu ni wajibu wa Serikali kuhakikisha wakulima wake wanapata masoko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Mtanzania wa kawaida amekwenda kuathirika kwa uzembe ambao umetokana na Serikali yenyewe. Kwa nini msiwasimamie wale mnaowalipa mishahara, mnawasimamia hawa ambao hatujui wamepataje pembejeo, hatujui wamefanyaje kuweza kupata hicho chakula? Hata viwanda tunavyoviimba ni viwanda ambavyo vitabaki kwenye historia tu kwenye maandishi, huwezi kuzungumzia viwanda wakati umeshindwa kuimarisha kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia viwanda ni lazima leo kama Serikali mjiwekeze, mhakikishe kabisa kwamba kipaumbele cha sasa ni kilimo, hivyo tutabadilisha wakulima wetu kwenda kuweka kilimo cha umwagiliaji, waachane na kilimo cha mazoea. Leo unasema asilimia kumi ndiyo mliyopeleka, huu ni utani, utani sana tu. Na tunapozungumza tukizungumzia Serikali tunazungumzia Chama cha Mapinduzi, ndicho chenye Serikali na Wabunge wanaposimama kuzungumza lazima wajue chama chao ambacho kinaongoza Serikali kimesababisha maumivu makali kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la uvuvi, yaani leo ikitokea kipindupindu kimetokea kwenye Mkoa wangu wa Rukwa, Wilaya ya Sumbawanga Vijijini, wakulima pamoja na wavuvi wameenda kuchomewa nyavu zao pamoja na makazi, yaani leo hakuna njia ya kudhibiti kipindupindu mnawachomea watu makazi yao. Serikali ya Chama cha Mapinduzi imewafikisha Watanzania mahali hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nani alikwambia kudhibiti kipindupindu ni kuchoma makazi? Yaani leo mmekosa kabisa njia mbadala ya kuzuia kipindupindu mnawaondoa watu wakawe maskini? Haya mambo ikifikia mahali kuna watu hawawezi kusema, sisi tuliotumwa leo kama wawakilishi wao kusema tukisema msiposikia kuna wakati mwingine watasema kwa milango ambayo hamtajua wanasemea wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi kwenye utawala bora na unapozungumzia utawala bora lazima uzungumzie utawala wa sheria. Leo unapozungumzia Mbunge wa chama cha upinzani ni kama unazungumza mtu ambaye ni adaui wa Taifa. Msajili wa Vyama vya Siasa kazi yake ni kulea vyama vya siasa, leo amekuwa muuaji wa vyama vya siasa. Katiba mpya imeelekeza maandamano ni haki ya Kikatiba, yeye anapaswa kuwaambia kwamba mnataka kuandamana kwa sababu gani, ameona kuna mvurugano wa vyama asimame katikati kuhakikisha vyama vinakwenda salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo CHADEMA wanaandamana, anasema ni kwa nini nisiwafutie usajili, na anajua Katiba inaelekeza kwamba maandamano ni haki ya msingi. Mbona wale wanaoandamana kumsifia Rais hawaambiwi waondoke nchini? Ila wewe ukiandamana kwa kutaka kumkosoa Mheshimiwa Rais wewe ni adui wa Taifa hili. Utawala bora bado kwa Tanzania ni jambo ambalo… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.