Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Julius Kalanga Laizer

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Monduli

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya mimi kusema katika hotuba ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze katika hili suala la watumishi walioachishwa kazi, hasa wale watendaji wa vijiji, wa kata na madereva. Mimi naomba tu Waziri atuambie; hivi utu wa kibinadamu katika jambo hili umezingatiwa kwa kiwango gani? Kwa sababu kama Waziri ambaye anasimamia sekta hii na anayesimamia utaratibu huu anajua kabisa kwamba watumishi hawa waliajiriwa na Serikali miaka hiyo kwa sababu kulikuwa kuna uhitaji wake, lakini kwa sababu Serikali sasa imeona labda hawahitajiki tena imeamua kuwa-dump na kuwatupa kama watu ambao hawajawahi kulitumikia taifa hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnatengeneza visa na chuki ambazo ni janga katika Taifa letu na kwa kweli hii laana ya watumishi ambao mliwachukua kwa uhitaji wenu, kwamba njooni fanyeni kazi mkiwa darasa la saba, mkiwa kidato cha nne, hawajaweza kujiendeleza kwa sababu ya mazingira pia, halafu leo mnawaondoa kazini na vilevile hamlipi stahiki zao wala hamsemi, kwa kiburi hiki, hakuna ambaye atabaki salama kwenu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ni muhimu mkatuambia hawa watumishi wanastahili au hawastahili. Kwa sababu mliwaajiri ninyi kwa sababu mlikuwa mna uhitaji, mlijua viwango vyao vya elimu na baadhi yenu hao madereva wa darasa la saba mliowaondoa waliwaendesha ninyi katika kutimiza majukumu yenu. Lakini leo kwa sababu mmepata uhitaji mmepata wengine mmewaacha hata hamtaki kulipa stahiki zao mnaamua kujadili siku mnayotaka; tunataka Serikali ituambie maslahi ya watumishi hawa walioondolewa kwa sababu ya kiwango cha elimu, maslahi yao na stahiki zao wanapewa lini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, acheni uonevu kwa sababu hawa mliwachukua ninyi kwa sababu mlikuwa mnawahitaji. Leo mnawaondoa hata pensheni zao hamtaki kuwapa, leo mnawaondoa hata kuzungumza nao hamtaki kwa sababu mmemaliza kazi, mmewatumia halafu baada ya kuwatumia mmeamua kuwatupa na hili mmefanya hivyo makusudi kwa sababu mnafikiri mna dola, mna nguvu ya kuwatumia na kuwafanya mnavyotaka. Ni muhimu mkasema kama wana haki wapewe na kama hawana haki basi muwaambie kuliko kufanya kama hisani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hili nawashangaa katika Hotuba hii ya Waziri Mkuu anasema Serikali inaendelea kutatua migogoro katika sekta binafsi na katika maeneo mbalimbali. Mnapata wapi moral authority ya kutatua migogoro kama ninyi mnafukuza kienyeji bila kufuata utaratibu? Unakwenda kumsuluhisha nani wakati wewe mwenyewe hufuati utaratibu huo katika kufukuza watu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ni muhimu mkaelewa kwamba ninyi mmekosa uhalali wa kusuluhisha migogoro katika nchi hii kwa sababu hata ninyi hamfuati sheria na utaratibu katika kuwaondoa watumishi kazini. Watumishi wa Umma hawa mnawanyima ruhusa kwenda kusoma lakini mnataka muwaambie wajiendeleze, wajiendeleze kwa namna gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu sio ubinadamu na wala haufai kabisa, Waziri ambaye na wewe ni binadamu na una watoto unadiriki kushiriki katika dhambi ya namna hii ya kudhulumu watu jasho lao walilotumikia nchi kwa zaidi ya miaka 15 eti kwa sababu ni darasa la saba, lakini waliwaendesha katika mapori mkitafuta kura na vilevile mkifanya majukumu yenu, leo mnawaondoa bila kuwazingatia, huu si ubinadamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu la pili, ukisoma katika Hotuba ya Waziri Mkuu ukurasa wa 35, imezungumzwa habari ya ujenzi wa viwanda na hili ni jambo jema sana na mimi napenda kulipongeza kama ni la ukweli. Hata hivyo mnavyozungumza viwanda mnasema mmejenga viwanda 3,306 lakini ukiwauliza hawa Wabunge ni Mbunge gani hata mmoja anaweza akasimama, hata kumi kuonesha viwanda vilivyojengwa kwenye maeneo yao? Hakuna hata mmoja. Hivi viwanda mnajenga wapi? (Makofi/Kicheko)

T A A R I F A . . .

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hii angenipa Mbunge wa kawaida ningeweza kumuelewa, yeye anatetea nafasi yake na taarifa hii haieleweke kwa sababu nchi hii si Mkuranga peke yake. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasema haya kwa ajili ya lengo la kujenga nchi yetu, tunataka Serikali ituonyeshe viwanda hivyo 3,306 viko wapi kwa majina na vinanzalisha nini ili sisi Wabunge tuweze kushuhudia Serikali katika hili jambo, ndiyo dhana yetu.

Lakini la pili tunataka viwanda vioanishe na maisha ya Watanzania, unajenga viwanda lakini unasema hakuna masoko wakulima hawa hivyo viwanda mnalisha nini kama malighafi haitokani na Watanzania wanaofanya kazi? Ni muhimu mkatuambia ni zao gani leo ambao mmezalisha viwanda zao hilo limepata soko na wakulima wamefaidi nchi yao kwa sababu viwanda vimechukua zile malighafi, mnatengeneza viwanda vya white elephant alafu baadae nchi yetu ibadilike kuwa dampo la bidhaa kutoka kwa ajili ya kulisha viwanda vya ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu Serikali ituambie viwanda hivyo vimejengwa wapi msituambie hii habari, nimesikia jana mtu anasema eti mashine ya kukoboa na kusaga mahindi ni kiwanda, mnasema brenda ni kiwanda, mnasema cherehani tatu ni kiwanda naona Mheshimiwa Naibu Waziri ananipiga taarifa lakini kwa wakati wake ana nafasi ya kujibu…

T A A R I F A . . .

MHE. JULIUS K LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba muda wangu ulindwe na Mawaziri mvumilie mtajibu, kwa nini mnakosa hata Wabunge wakuwatetea subirini mtajibu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme kwamba lengo letu ni jema tu, tunataka viwanda hivi visaidie unafuu wa maisha ya Watanzania tunataka mtuambie hiyo sera inayosema ina categorization viwanda mlete categorization ya viwanda hivyo kulingana na sera mnayosema, tatizo liko wapi? Kama cherehani ni kiwanda semeni, kwa sababu mnasema eti ikiwaajiri watu watatu ni kiwanda, cherehani kuna yule anayekata nguo na anayeshona ni kiwanda tayari mtuletee hizo categorization. Tunataka viwanda vya nchi vioanishe na maisha ya Watanzani ili malighafi tunayozalisha sisi tupeleke kwenye viwanda vyetu, leo mnazungumzia kwenye... (Makofi/Kicheko)

T A A R I F A . . .

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ulinde muda wangu. Mimi siweze kushabikia, kwanza ni kiwanda cha kutengeneza kansa kwa wananchi halafu kiwanda ni cha zamani, ni sawa sawa umejenga shule ukijenga darasa jipya unaona umefanya maendelezo mapya unafungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri tukaelewa, ukizungumza taarifa hii Wizara ya Mifugo, sekta ya mifugo imezungumzwa chini ya maneno 100, sekta ambayo inagusa asilimia kubwa ya Watanzania, imezungumzwa kwa kiwango ambacho nusu page halafu imezungumzwa kupiga chapa hivi ng’ombe ni chapa? Nchi ya pili Afrika kwa uzalishaji wa mifugo unazungumza habari ya chapa, ndiyo sera ya Serikali inakuja kuzungumza kwenye taarifa ya Mheshimiwa Waziri Mkuu?

T A A R I F A . . .

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwelekeo ndio chapa? Nimesema taarifa iliyozumnguzwa huko unazungmza habari ya chapa hivi mwelekeo ya Wizara ya Mifugo kwetu sisi wafugaji ni chapa? Ndiyo mwelekeo Mheshimiwa Waziri Mkuu ametuelekeza, chapa ndicho tunachosema katika eneo hilo hatujatendewa haki kama sehemu ya ufugaji wa nchi hii. Tunamahitaji mengi hakuna maeneo ambayo imeelekeza tufanye nini, mnatuambia chapa, milioni mbili sijui ngapi, mnaharibu ngozi, mmeleta sheria halafu mnazungumza badala ya kutusaidia tupate malisho, maeneo ya nchi hii ni mapori mmeshindwa kutupa ameneo mnazungumza chapa, halafu tupige makofi, hatuwezi kupiga makofi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nasema jambo langu la mwisho, kuhusu upatikanaji wa fedha katika miradi ya maendeleo na hili ni muhimu sana Serikali ikajua Wabunge tunataka nini. Mimi nafikiri ni muhimu kwa sababu mmeshindwa kupeleka fedha za miradi ya maendeleo, tuchague vipaumbele vya miradi michache halafu tukaitekeleza tukawa na miradi ya mfano, hutasikia tukigombana kwenye hili Bunge kama kila Mbunge atasema mlikuwa mmependekeza kutengeneza mradi wa maji na akauona mradi wa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnaleta hapa figure za maneno ili kuionesha nchi mnayo fedha, lakini kwenye maendeleo ya miradi yetu hamtuletei fedha, miradi imebaki viporo. Tunaomba kama Serikali ina nia ya kusaidia wananchi tuangalie vipaumbele vya kila Halmashauri halafu tupeleke fedha hata kama ni mradi mmoja, lakini ukakamilika ukawanufaisha wananchi. Lakini zaidi ya hivyo mkiwa mnaongeza kila kitu trilioni hizo trilioni za kwenye karatasi hazitusaidii sisi, tunayo...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)