Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. COSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema na nimepata nafasi ya kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Naomba nitoe pongezi kwa hotuba nzuri na kwa kweli ninaunga mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kumshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kushiriki katika tukio la uwashaji wa Mwenge pale Geita Mjini, nimpongeze sana kwa hotuba yake nzuri, lakini niwapongeze sana Wizara pamoja na watendaji wote ambao tulishirikiana nao kwa kiwango kikubwa na kwa kweli niwapongeze pia wananchi wa Jimbo la Geita Mjini ambao walijitokeza kwa wingi sana na kuvunja record katika siku ile ambapo Mwenge ulikuwa unawashwa na watu wa Geita hatuna cha kuwalipa tunawashukuru sana kwa sababu ni tukio la kihistoria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mliona tulipeleka sherehe zile za kuwasha Mwenge sehemu ambapo ni katikati kidogo ya msitu, lile ni eneo maalum la hekta 12 ambalo tumetenga kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja cha michezo na wananchi wa Mkoa wa Geita kama wangepewa nafasi ya kusema neno moja kupitia mwakilishi wao, basi ombi lao kubwa lilikuwa ni msaada wa kupata namna ya kujenga uwanja wa michezo wa Mkoa wa Geita. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri Mkuu tunaomba sana hilo lisikike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili niende kwenye suala la uvuvi, ninaunga mkono zoezi la kupiga vita uvuvi haramu na tangu nimeanza kuzungumza Bungeni hakuna sehemu niliwahi kukosoa au kuunga mkono uvuvi haramu. Tatizo langu kubwa limekuwa ni approach iliyotumika kupambana na operation yenyewe lakini pia na namna ambavyo huko chini linavyotekezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama unakumbuka katika matukio tulipokuwa hapa Bungeni niliomba mwongozo baada ya majibu ya Mheshimiwa Waziri alipokiri kwamba nyavu ya dagaa ya milimita nane inaweza ikakamata samaki aina ya Sangara ambao wako chini ya sentimita 55 na akakiri kwamba nyavu ya dagaa inaweza ikaja na samaki wadogo wadogo. Naibu Spika baada ya Naibu Waziri kukiri aliiagiza Serikali tangu siku hiyo iache kusumbua wananchi wanaokamatwa hovyo, wanaopigwa faini hovyo kwa sababu ya kukutwa na samaki wadogo wadogo, kumbe nyavu zina uwezo wa kukamata samaki wa aina mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na maagizo hayo ya Bunge hili, wananchi waliendelea kukamatwa, wameendelea kutesema na hali ya maisha ya wananchi wanaozunguka ziwa ni mbaya sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kosa ni moja tu tumefikiria sana size ya samaki wa kuuza nje wanaoanzia sentimita 50 kwenda juu wa sangara tukaacha kufikiri kwamba samaki ni maisha ya wananchi wanaozunguka ziwa. Samaki sangara ambae anauzwa nje anaanzia sentimeta 50 lakini sato ambae hauzwi nje anaanzia sentimeta 25; sasa samaki sangara ambae analiwa Tanzania lazima aanzie sentimeta 50 sawa na anayeuzwa nje kitu ambacho hakiwezekani kwa sababu nyavu zilizoruhusiwa na Serikali zinaweza kukamata samaki size ndogo kuliko ambao wameruhusiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mateso wanayoyapata wananchi ni makubwa sana hivi sasa tunavyozungumza Mtendaji wa Kijiji anakamata samaki, Mgambo anakamata samaki, Polisi anakamata samaki na matukio mabaya kabisa ambayo yanaendelea. Siku moja nilikuwa Geita mama mmoja anakwenda kumsalimia mwanae hospitali ana samaki wanne wamebanikwa amebeba kwenye box ndani ya hiace, ikakamatwa hiace, akakamatwa na mwenye samaki, kosa la mwenye hiace ni kwa nini amesafirisha samaki wanne kwenye box na kosa la mwenye samaki kwa nini amesafirisha samaki wadogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria haisemi hivyo, sheria inataja kama unataka kusafirisha samaki uwe na usafiri maalum wa samaki, lakini samaki wale ni wa biashara siyo samaki wa kula. Kuna matumizi mabaya sana ya sheria. Tulipotunga kanuni za uvuvi tuliweka Sheria ya Adhabu inasema kuanzia shilingi 50,000 mpaka shilingi 2,000,000, Waziri amekwenda amechukua Sheria za Mazingira akaziingiza kwenye Sheria za Uvuvi, akasahau mukhtadha wa uvuvi ni wa watu maskini anapiga faini kuanzia shilingi 50,000 mpaka shilingi 50,000,000, matokeo yake mtu mwenye mitumbwi miwili; mwenye mtaji wa milioni sita anaambiwa faini ya milioni tano, matokeo yake wavuvi wote wamefilisika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbaya zaidi tulikamata nyavu mpya tukazichoma moto. Katibu Mkuu wa Wizara wakati anachoma moto alikuwa anasikitika anasema ninachoma moto huku roho inaniuma nyavu za bilioni mbili. Mimi nikajiuliza, mimi nimesoma Mbegani Fisheries, kwa nini hakuchukua nyavu zile akapeleka chuoni wale wanafunzi wakajifunza kukata, kutengeneza single au akawapelekea Nyegezi Fisheries wakajifunza kutengeneza single ili wawape vijana wafanyakazi za uvuvi. Unachukuaje mtaji wa bilioni tatu unachoma moto nyavu mpya halafu unasikitika huku unafanya unachotekeleza? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu ambacho angefanya angechukua zile nyavu akasema kumbe nyavu iliyoungwa mara tatu inaweza kukatwa ikapatikana single akawapelekea chuoni, akawaambia ninyi chuoni jifunzeni kushona, jifunzeni kukata, wapeni watu wanaohitaji mitaji ingewasaidia. Sasa mtu huyu aliyechomewa nyavu amekubali masharti, amepata hasara. Amendika kibali cha kuomba kuagiza nyavu nje mwezi wa kwanza, leo mwezi wa nne barua zake ninazo hapa hajaruhusiwa, kule wavuvi hawana nyavu, wamekaa, Serikali imekaa, wanaangaliwa tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kambi ilikuwa na wavuvi 50 hakuna mvuvi hata mmoja, viwanda vile vya samaki vya Mwanza vime-paralyze, wananchi wame- paralyze, Waziri hafanyi maamuzi nini tatizo hapa? Maagizo tukilalamika hayachukuliwi hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana inawezekana Waziri hafahamu yanayoendelea kule chini. Alichokisema Mheshimiwa Musukuma hebu tuunde tume tukasikilize watu. Kuna watu wamekufa kwa sababu ya kukimbia, wanawakimbia mgambo wanakufa kwenye maji na huu ni uonevu wa hali ya juu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wa Kanda ya Ziwa maisha yetu ni uvuvi na ufugaji. Kwenye ufugaji kilichotokea mnajua, kwenye uvuvi kilichotokea mnafahamu, tunakwenda wapi sasa? Kwa sababu bahati mbaya sana Waziri wa Kilimo naomba nikuambie hata pamba tuliyokuwa tunaitegemea juzi imeanza kuliwa na wadudu na bahati mbaya sana matunda nayo yanaliwa na wadudu inawezekana isipatikane. Tunawasababishia umaskini Watazania.
Mheshimiwa iti, tunalolisema hili mimi ninazo karatasi hapa za watu walioomba vibali mwezi wa kwanza mpaka leo hakuna kinachoendelea. Inatuuma sana kwa sababu hatukuingia humu kwa bahati mbaya, tuliingia humu kuja kutetea wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala jingine ni suala la Watendaji, nilifunga safari nikaenda kwa Katibu Mkuu wa Utumishi kwenda kumuuliza hivi ni kwa nini tangu mwaka 2004 mpaka leo 2018 walikuwa hawajachukua hatua akaniambia mwaka 2004 ilipotolewa maelekezo na Katibu Mkuu Utumishi tuliwapa miaka mitatu, ilipoisha tukawapa miaka mitatu, ilipoisha waliokuwepo wakakaa kimya. Busara ya kawaida ya waliokuwepo kukaa kimya waliona zoezi hili halitekelezeki, ndiyo maana walikaa kimya kwa sababu kama ingekuwa yule aliyekuwepo wakati ule anajua hili suala ni gumu, tangu mwaka 2010 angeagiza watu wafukuzwe kazi, sasa baada ya hapo watu walipata barua za ajira, watu wengine ni pensionable leo unawafukuza kazi unasema hawa wameiingizia Serikali hasara, hili siyo la kweli na halikubaliki na hatuwezi kulikubali.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jingine ambalo naomba niliongee ni la wananchi wangu wa Geita. Geita tuna mgogoro na watu wa GGM. Tangu miaka mitatu, minne iliyopita Mawaziri walikuja karibu sita, nyumba za wananchi karibu 800 zimepasuka kwa sababu ya milipuko ya GGM, leo ni miaka mitatu Serikali ikitoa maagizo GGM hawatekelezi. Kuna wananchi pale wanakaa ndani ya vigingi vya GGM miaka 18 hawalipwi fidia, Serikali inatoa maagizo hayatekelezwi. Kuna wananchi Nyakabale, kuna wananchi Mgusu, kuna wananchi Manga wako ndani ya vigingi vya GGM hawaruhusiwi kufuga, hawaruhusiwi kulima, wanakamatwa na maliasili, wanakamatwa na mgodi lakini Serikali ilitoa maagizo mgodi hautekelezi. Nilitaka kufahamu ni naniā¦(Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha muda wa Mzungumzaji)